Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Kwanza

Mwanamume katika giza.

Nilipita siku ya Jumatatu huko Mwananyamala katika nyumba za ndani sana. Baada ya kuvuka mitaro mitatu, nikaona nyumba iliyokuwa na baraza kubwa. Hapo barazani alikaa binti mrembo sana ambaye kwa uzuri wake angetosha kushtua, kuchanganya na kupunguza ufanisi wa akili ya mwanamume yeyote. Binti huyu aliyekuwa na sura iliyochongeka kwa mfano wa umbo la yai, alivalia dela lililoficha umbo lake.

Nilitembea hata nikawa mkabala na mahali alipokaa, nikaporomosha salamu huku nikipunga mkono, “Habari.”

“Nzuri,” msichana alijibu akibadili mkao, nami nikaendelea na hamsini zangu.

Nilipita siku ya Jumanne huko Mwananyamala katika nyumba za ndani sana. Baada ya kuvuka mitaro mitatu, nikaona nyumba iliyokuwa na baraza kubwa. Kama jana, binti yule alikaa, nami nikaporomosha salamu, “Habari.”

“Nzuri,” msichana alijibu akibadili mkao, nami nikaendelea na hamsini zangu. Lakini wakati nikitembea, nilisikia vishindo vikija. Nilipogeuka, niligongana uso kwa uso na msichana niliyemsabahi.

“Kaka…” aliita akitazama chini kwa aibu. “Naomba nisaidie elfu moja.”

Sikufikiria mara mbili, nilitoa mfukoni noti moja ya shilingi elfu moja nikampa. Kisha nikatoa kikaratasi na kalamu, nikaandika 1,000/=.

Nilipita tena siku ya Jumatano eneo hilohilo. Baada ya salamu, binti alinifuata akaniomba elfu moja, nikampa kisha nikaandika katika kikaratasi changu.

Nilipita kwa mara nyingine eneo lile siku ya Alhamisi. Binti akaomba elfu moja. Nikampatia kisha kama kawaida nikaandika katika kikaratasi. Sasa hesabu jumla ilisomeka shilingi za Kitanzania elfu tatu.

Basi nilivutiwa na upitaji wa njia ile, Ijumaa nayo nikapita. Kama kawaida binti akaniomba elfu moja, nikampa kisha nikaandika kwenye kikaratasi changu. Wakati nataka kuendelea na hamsini zangu, alinidaka mkono akaniomba tukae kibarazani kwa muda.

“Huwa unaandika vitu gani ukinipa hela zako?” msichana aliuliza akinitazama bila aibu, huenda alikwisha nizoea.

“Huwa naandika hela ninazokupa. Sasa zimefika shilingi elfu nne,” nilijibu nikitabasamu.

Binti aliangua kicheko, kisha akasema, “Mwanaume bahiri wewe, sijawahi kuona… jina lako nani wewe?”

“Naitwa Mako.”

“Oooh… kumbe!”

“Unafanya kazi gani bwana wewe?”

“Sisi wengine kazi zetu huwa hazitajwi,” nilijibu kisha msichana akacheka tena.

“Ukipita hapa huwa unakwenda wapi?”

“Huwa nakwenda maeneo tofauti, leo nakwenda Kibo Peak kutuliza kichwa.”

“Oooh, nikipata nafasi ya kutoroka nitakuja… Usiondoke mapema,” kabla hajaendelea, vilisikika vishindo vikija kutokea ndani.

“Babuu anakuja, kimbia haraka asikuone,” alinisisitiza, nami nikakimbia kwa kasi kumshinda mwanariadha Usain Bolt. Njiani niliwaza mambo mawili: Babuu ni nani? Na huyu msichana niliyeongea naye jina lake nani? Nilipata kona nzuri nikajificha, nikatazama ili nimuone huyo Babuu, hakuwa mzee kama lilivyo jina lake, alikuwa kijana au mwanamume wa makamo makadirio miaka arobaini mwisho hamsini. Alivaa mavazi chakavu, juu kichwa kipara na chini alikuwa na kandambili. Sikutaka kuchunguza sana, nikaondoka.

Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Pili

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne