Jinsi ya Kuwafanya Wanafunzi Wapende Kusoma

Vitabu chai na mkono

Tumezungukwa na wanafunzi wanaotamani kufaulu lakini hawapendi kusoma. Wengine huomba kufundishwa mada za muhimu zitakazowafanya wafaulu mitihani yao, ukiona hivyo, tambua mwanafunzi huyo hapendi kusoma. Pia, hakuna mada za muhimu na zisizo za muhimu. Mada zote ni za muhimu na huenda zikawa na maswali katika mtihani. Mwanafunzi anayefaulu ni yule anayesoma, iwe kwa kupenda au kutopenda, ni lazima usome kwani mtihani hupima yale uliyoyaweka kichwani kwa kusoma.

Walimu wamekuwa wakiniuliza swali juu ya namna ya kuwafanya wanafunzi wao wapende kusoma. Makala hii ni jibu kwao. Hata wale wanafunzi wasiopenda kusoma, makala haya yatawasaidia. Yafuatayo ni mambo yanayoweza kuwafanya wanafunzi wapende kusoma:

1.   Onyesha faida ya kile unachowafundisha

Kama unachofundisha hakina faida kwao, wanafunzi hawawezi kupenda kusoma. Taja faida ya somo au mada katika maisha yao. Mimi nifundishapo mada mpya katika somo la Kiswahili huanza kwa kusema:

“Mada ya leo inaitwa Utumizi wa Lugha. Mada hii ni muhimu sana kwenu kwa sababu inawafundisha namna sahihi ya kutumia lugha. Ipo siku humu ndani, mtakuja kuwa viongozi, mtatakiwa kutumia lugha vizuri ili mnaowaongoza wawaelewe. Wengine mtakuja kuwa wasemaji wa serikali na taasisi mbalimbali, pote mnahitaji matumizi mazuri ya lugha. Jambo zuri zaidi ni kwamba, hata usipopata nafasi ya cheo kikubwa, bado nina uhakika utakuja kuwa japo msemaji wa familia yako. Unahitaji kuyafahamu matumizi ya lugha. Hivyo, mada hii ni muhimu kwa kila mmoja wetu.”

Utangulizi huo unamvutia mwanafunzi na kumfanya apende mada, somo na mwalimu wake. Unamfanya aone kumbe hayupo darasani kupoteza muda, bali kujipatia maarifa yenye faida lukuki katika maisha yake.

2.   Washawishi wapate muda wa kusoma peke yao

Washauri wanafunzi wakae wasome peke yao, wajulishe kuwa, wasomapo, wawe na yale yanayohusiana na masomo pekee. Simu na vifaa vingine visivyo muhimu waviweke mbali.

3.   Washauri wanafunzi wafundishane wenyewe kwa wenyewe

Kupitia kufundishana wenyewe kwa wenyewe, watafurahia somo. Wataona kama wanaofahamu zaidi hata kupata hadhi ya kuwa walimu. Si hivyo tu, mwanafunzi anayefundisha wenzake, hukumbuka zaidi na kuelewa masomo kuliko yule anayefundishwa pekee. Katika kukumbuka, tunakumbuka 10% ya yale tunayosoma, 20% tunayosikia, 30% tunayoona, 70% tunayojadiliana na wengine, na tunakumbuka 95% ya yale tunayowafundisha wengine. Hivyo basi, mwanafunzi anayefundisha wengine, ananafasi ya kukumbuka zaidi masomo.

Mwalimu asikate tamaa, awe mpole kwa wakati wote na ajitahidi kuwasaidia wanafunzi kupenda kusoma. Kuwafanya wanafunzi wapende kusoma, ni jambo gumu, linalohitaji muda, upendo na bidii.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie