Mbinu Saba za Kufaulu Mtihani Wowote Shuleni

Mbinu za kufaulu mtihani.
Namba saba ni namba ya ajabu katika orodha ya namba tulizonazo. Kuna mabara saba, bahari saba, elimu ya msingi ina madarasa saba, upinde wa mvua una rangi saba, tuna sikukuu inaitwa sabasaba, tuna maajabu saba ya dunia, na sasa nakwenda kukueleza mbinu saba za kufaulu mtihani wowote. Tafadhali zizingatie mbinu hizi. Lakini kabla sijaeleza, hebu tafakari japo kwa dakika moja, inakuwaje shule fulani wanafeli wanafunzi wote, yaani darasa zima halikuwa na mtu mwenye uwezo wa kufaulu? Lakini pia, inakuwaje shule fulani wanafunzi wote wanafaulu tena kwa daraja la kwanza, ama unadhani shule hizo zimekuwa zikiiba mitihani, siyo kweli, nimefanya kazi katika shule za aina hii kwa miaka mingi na sijawahi kuona udanganyifu wowote. Tofauti ya shule zinazofaulisha kwa wingi na zile zinazofelisha kwa kiwango kikubwa, ipo katika mbinu hizi saba. Ni mbinu ambazo bahati mbaya wanafunzi wengi hawaambiwi, lakini wewe una bahati, zisome mbinu hizi zaidi ya mara moja na utaweza kufaulu mtihani wowote.

     1.   Fundishwa

Kuwa na vitabu vya somo, kusoma somo hilo peke yako na kuliewa haimaanishi kwamba hutakiwi kufundishwa. Inawezekana unachosoma unakielewa lakini kuna mambo unakosa kwa sababu huna mtu anayefahamu kitu hicho. Hivyo kama unataka kufaulu mtihani wako, tafuta Mwalimu akufundishe. Unapotafuta Mwalimu, tafadhali kuwa makini kutafuta Mwalimu mwenye taaluma na ujuzi. Walimu wengi ni wazuri, lakini bahati mbaya kuna walimu wachache ambao siyo walimu bali ni watu waliovamia tasnia, hivyo kuwa makini katika kumtafuta Mwalimu sahihi.

     2.   Jisomee

Soma yale uliyofundishwa, pia soma ambayo bado hujafundishwa. Hakikisha unakuwa na ratiba ya kujisomea kila siku. Tengeneza ratiba ambayo haitakubana sana, ukitengeneza ratiba ya masomo ambayo inakubana sana, hutaweza kuitimiza na utajikuta husomi kabisa. Hivyo ni vyema kuwa na ratiba ya masomo ambayo unaamini unaweza kuifuata.

     3.   Fanya maswali ya Mwalimu

Mwalimu akikupa maswali lengo lake ni kutaka kufahamu uwezo wako, wapi ulielewa na wapi hukuelewa. Mwalimu hutoa maswali kupima uwezo wako wa masomo pia udhaifu ulionao. Kupitia maswali unayofanya, unamsaidia mwalimu kubadili mbinu ili uweze kuelewa. Usipofanya maswali, mwalimu hataweza kufahamu uwezo wako na namna ya kukusaidia. Hivyo, fanya maswali.

     4.   Fanya mitihani ya mwalimu

Kama yalivyo maswali, mitihani nayo hulenga kukupima uwezo wako pamoja na madhaifu uliyonayo. Faida kubwa ya mitihani ni kukusaidia kufanya mazoezi ya kutosha kabla ya mtihani wako wa mwisho. Mtihani wa mwalimu, ni mazoezi ya mtihani wako wa mwisho.

     5.   Pitia mitihani iliyopita

Pitia mitihani iliyopita hususani mitihani ya NECTA. Katika mitihani hii, utaweza kuona namna mtihani wako wa mwisho ulivyo, utaweza kuona aina ya maswali na mpangilio wa mtihani huo. Huwezi jua, inawezekana baadhi ya maswali yakajirudia katika mtihani wako. Hata hivyo, usitegemee bahati hii, badala yake soma kila kitu.

     6.   Soma vitabu/notes sahihi

Wengi wameshindwa mitihani kwa sababu hawakuwa na vitabu sahihi vya kusoma. Vitabu ni vingi na vinapatikana kila mahali. Vitabu vingine vinapatika mitandaoni, na vingine katika maduka ya vitabu. Bahati mbaya sana, vitabu vingi havijafuata mtaala katika kuandikwa kwake na haijulikani sababu ni nini. Hata uwe na uwezo mkubwa, kitabu kibaya kitakupa matokeo mabaya. Hivyo, tafuta vitabu sahihi.

     7.   Zingatia muda

Weka ratiba na ifuate. Kuwa na muda wa kuongea na marafiki, kutembea, kufanya usafi na mambo mengine mbalimbali. Zingatia na tumia vizuri muda vinginevyo utashangaa tarehe ya mtihani inafika na wewe hujakamilisha maandalizi ya mtihani huo.

Hivyo basi, mbinu saba za kufaulu mtihani wowote shuleni ni: kufundishwa, kujisomea, kufanya maswali ya mwalimu, kufanya mitihani ya mwalimu, kupitia mitihani iliyopita, kusoma vitabu au notes sahihi na kuzingatia muda.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne