Utata Katika Uainishaji wa Tanzu za Fasihi

Kitabu juu ya meza


Fasihi Simulizi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni: M.M. Mulokozi (1996) anasema, Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.

TUKI (2004) wanasema, fasihi simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.

Balisidya (1983) anasema, fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.

Wanjara (2011) anasema, fasihi simulizi ni sanaa ambayo vyezo kuu ya utunzi, uwasilishaji na usambazaji wake ni sauti pamoja na vitendo. Fasihi simulizi ni sanaa inayotumia mazunguzo na vitendo kisanii ili kuwasilisha maarifa au ujumbe Fulani kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Kwa ujumla, fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutolewa kwa njia ya mdomo kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Aina hii ya fasihi, huhifadhiwa kwa njia ya kichwa, japo kutokana na mabadiliko ya teknolojia, uhifadhi wa asili umeanza kuchukuluwa na vifaa kama: Kompyuta, vinasa sauti, kanda za video na intaneti.

Tanzu za fasihi simulizi ni aina mbalimbali ya kazi za kifasihi simulizi. Tanzu za fasihi simulizi zimeanishishwa na waandishi wengi kama tanzu hizo zilivyo nyingi.

Miongoni mwa waandishi walioanisha tanzu za fasihi simulizi ni pamoja na:

Mulokozi ameanisha tanzu sita za fasihi simulizi kama ifuatavyo:

         i.            Mazungumzo

       ii.            Masimulizi

      iii.            Maigizo (drama)

     iv.            Ushairi

       v.            Semi

     vi.            Ngomezi (ngoma)

Mazungumzo ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi mazungumzo ili yawe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani na uhalisia baada ya kuunakili. Mfano, tanzu zinazoingia katika fungu la mazungumzo ni kama hotuba, malumbano ya watani, ulumbu, soga na mawaidha.

Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulani. Mulokozi (1989) anasema, kuwa masimulizi ni fasihi ya kihadithi na fani zake huwa na sifa kama kuelezea tukio katika mpangilio Fulani mahususi, huwa na wahusika yani watendaji. Katika Mulika 21 Mulokozi amegawanya fasihi simulizi katika tanzu zifuatazo za kihadithi ambazo ni; ngano, visakale, tarihi, istiara, mbazi na kisa.

Semi ni tungo au kauli fupifupi zenye kubeba maana Fulani au mafunzo muhumu katika jamii, Mulokozi ameanisha tanzu semi kama ifuatavyo; methali, mafumbo, vitendawili.

Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na vina ushairi una ufasaha wa maneno au muktasari wa mawazo na maono ya ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu. Ushairi hupambanuliwa na lugha ya kawaida kwa kutumia lugha na mbinu za kimuktadha. Mulukozi (1989), amegawa ushairi katika mafungu mawili ambayo ni nyimbo na uwasilishaji.

Maigizo (drama) ni sanaa inayotumia watendaji kuiga tabia au matendo ya watu na viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani. Maigizo ni sanaa inayopatikana katika makabila mengi. Mulokozi anasema drama (maigizo) ya kiafrika huambatana na ngoma mtambaji wa hadithi au matendo ya kimila.

Ngomezi ni midundo Fulani wa ngoma kuwakilisha kauli fulani katika lugha ya kabila hilo mara nyingi kauli hizo huwa ni za kishairi au kimafumbo.

Mtaalamu mwingine aliyeainisha tofauti na uainishaji wa Mulokozi ni Wanjara (2011) ambaye anaainisha tanzu mbalimbali za fasihi simulizi ambazo ni zifuatazo:

         i.            Hadithi za kihistoria

       ii.            Hadithi za kubuni

      iii.            Ushairi (nyimbo)

     iv.            Semi

       v.            Maigizo

     vi.            Mazungumzo

    vii.            Ngomezi.

Wataalamu wengine ni Ndungo na Wangali, wao wanaziainisha tanzu tano za fasihi simulizi wanaanza na:

         i.            Hadithi

       ii.            Ushairi na nyimbo

      iii.            Sanaa za maonyesho

     iv.            Methali

       v.            Vitendawili.

Nao wataalamu Njogu na Chimera (1999) wanaainisha tanzu zifuatazo:

         i.            Hadithi

       ii.            Nyimbo

      iii.            Methali

     iv.            Vitendawili

Hivyo basi, kuna utata mkubwa unaojitokeza katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi. Maelezo haya, yanaeleza sababu za utata wa uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi:

Sababu ya kwanza inasababishwa na wataalamu wenyewe. Kila mtaalamu ameainisha ajuavyo tanzu za fasihi simulizi. Kwa mfano, Mulokozi anataja: mazungumzo, masimulizi, maigizo, ushairi, semi na ngomezi. Wanjara anaongeza kitu kipya ambacho ni hadithi za kihistoria. Ndungo na wangali hawaonekani kuzikubali semi zote, wao wanataja methali na vitendawili pekee. Nao Njongu na Chimera hawaonekani kuyatambua maigizo kama utanzu wa fasihi, wao wanataja hadithi, nyimbo, methali na vitendawili. Hivyo, mtazamo wa wataalamu na namna wanavyoainisha tanzu za fasihi simulizi unasababisha utata kwani tanzu zao hazifanani.

Pia, Utata unatokea kutokana na kutofautiana kwa vigezo vinavyotumiwa na wataalamu mbalimbali katika ugawaji huu, kwani kila mtaalamu hutumia vigezo vyake kulingana na matakwa ama mtazamo wake. Kukosekana kwa kigezo maalumu kilichokamilika cha uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi ni chanzo kingine cha utata. Hakuna kigezo kimoja kilichokamilika ambacho kingeweza kutumiwa na waandishi ili kuainisha tanzu za fasihi simulizi. Sababu hiyo imepelekea kila mwandishi kutumia kigezo na msingi anaoufahamu yeye na hii kusababisha utata. Hii ndiyo sababu, japo wataalamu wanazungumzia tanzu za fasihi simulizi, kila mmoja ana tanzu zake kulingana na msimamo wake.

Utata mwingine unasababishwa na fasihi kubadilikabadilika katika fani. Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu zinazoingiliana.

Sababu nyingine ya utata ni wataalamu kutumia vigezo vyenye mapungufu. Vipo vigezo ambavyo vina mapungufu makubwa na ni vigumu kuainisha tanzu fulani bila kusababisha utata. Kwa mfano, kigezo cha unguli (protagonist of the tale), katika kigezo hiki kunajitokeza ngano zihusuzo wanadamu, ngano za wanyama, ngano za vichimbakazi, na ngano za miungu. Hata hivyo kigezo hiki kinaonyesha kuwa na matatizo makubwa yanayoendelea kusababisha utata.

Sababu nyingine ya utata ni uchanga wa fasihi simulizi. Fasihi simulizi ni change siyo kwa sababu imeanza miaka ya hivi karibuni, ni change kwa sababu kusomwa kama taaluma imeanza miaka ya hivi karibuni. Hivyo basi, tafiti nyingi hazijafanywa jambo ambalo linasababisha utata. Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni sababu inayopelekea utata.

Kukosekana vitabu vilivyoandika kwa undani kuhusu fasihi simulizi kumesababisha utata katika uanishaji wa vipera vyake. kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan kinachoitwa Oral Literature in Africa (1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987) Mulika namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi. Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya uimbaji.

Hivyo basi, utata katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi unasababishwa hasa na uchanga wa taaluma ya fasihi simulizi na changamoto zingine kama kukosekana kwa kigezo kilichokamilika. Katika lugha, kutofautiana kwa wataalamu si jambo baya, ni mwanzo mwema wa kukubaliana na kukua kwa taaluma. Wataalamu wasichoke kuchunguza na kuja na kigezo kimoja ambacho kitatoa tanzu zinazokubalika na kukosa utofauti. Hata hivyo, Mulokozi anaonekana kukubalika zaidi katika tanzu alizoainisha. Pamoja na kukubalika, tanzu zake zina mapungufu mengi kama mapungufu yanayoonekana kwa wataalamu wengine.

MAREJEO

Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M. (1989). Tanzu za fasihi simulizi. Mulika. 21:1-24. Dar-es-salaam.

TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.  (Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press  
       na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).

Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi.

Wamitila, K W (2003), Kichocheo cha fasihi simulizi: Focus Publications Ltd. Nairobi


Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne