Uradidi Unavyojitokeza Katika Lugha ya Kiswahili
Onesha
kwa mifano ya kutosha onesha namna uradidi unavyojitokeza katika lugha ya
Kiswahili.
Ili
kutimiza mahitaji ya kila siku ya wanadamu, wanahitaji kuwasiliana, hata hivyo
ipo changamoto ya msamiati. Changamoto hiyo ni kukosekana kwa msamiati unaohitajika
ili kutaja kila dhana. Kutokana na upungufu wa msamiati unaohitajika kutaja
kila dhana, watumiaji wa lugha hutumia mbinu mbalimbali za kuboresha msamiati
uliopo ili ubebe dhana za ziada. Miongoni mwa mbinu zitumiwazo ni uradidi.
Uradidi ni dhana inayojitokeza katika lugha nyingi kwa lengo la kuboresha
msamiati uliopo ubebe dhana za ziada. Katika lugha ya Kiswahili, tukiacha dhima
nyingi nyingine kama zile zilizobainishwa na Ashton (1944:316-318), uradidi
unaweza kutumika katika mosi: kuimarisha au kudhoofisha maana, pili, kuongeza
na kupunguza msisitizo wa dhana inayozungumziwa. Kwa hiyo, wakati mwingine
mtumiaji wa lugha ya Kiswahili hulazimika kutumia mbinu ya uradidi ili
kuwasilisha dhana ambayo ama haina msamiati unaojitegemea au mzungumzaji hajui
msamiati unaofaa kutumika katika muktadha unaohusika. Dhana hii ya uradidi hujitokeza zaidi katika
lugha ya mazungumzo ambapo wazungumzaji wanakuwa huru kutumia mbinu zozote
wanazozijua ili kuwezesha mawasiliano yafanikiwe kwa kiwango kinachostahili.
Katika makala haya, tutaonesha namna uradidi unavyojitokeza katika lugha ya
Kiswahili.
Kwa
mujibu wa Rubanza (1996), anafasili uradidi kuwa ni njia ya kuunda maneno mapya
katika Kiswahili, kama ilivyo katika lugha zingine ni kurudufu au kwa maneno
mengine ni kurudia maneno. Neno lote zima linarudiwa au sehemu ya neno
linarudiwa. Linaporudiwa neno zima kitendo hicho huitwa urudufu kamili na
linaporudiwa sehemu ya neno ni urudufu nusu.
Kwa
mujibu wa Matinde (2012), uradidi ni utaratibu unaotumika katika kuunda maneno
ambayo sehemu ya neno lote hurudiwa na kuunda neno au msisitizo fulani. Fasili
ya Matinde ina upungufu katika kufasili hasa nini maana ya uradidi kwani si
lazima neno lote lirudiwe, huweza kuwa sehemu tu ya neno.
Hivyo
tunaweza kusema kuwa, uradidi ni kanuni au utaratibu katika lugha wa kuunda
neno/maneno mapya kwa namna ya kurudia sehemu ya neno au neno zima. Ili hali
sehemu ya neno ikirudiwa huitwa urudufu nusu na ikiwa ni sehemu nzima ya neno
hujulikana kama urudufu kamili.
Katika
lugha ya Kiswahili, uradidi unajitokeza katika namna zifuatazo:
Kwanza
uradidi hujitokeza kama uradidi kamili. Uradidi kamili ni uradidi ambao neno
zima hurudiwa. Uradidi huu hutumia kanuni ya neno jumlisha neno kuleta neno
jipya.
Kanuni:
Neno + neno = Neno jipya.
Peta +
peta =
petapeta
Pole +
pole =
polepole
Haraka + haraka
= harakaharaka
Cheka
+ cheka = chekacheka
Pilika
+ pilika = pilikapilika
Pika + pika = pikapika
Shamra
+ shamra = shamrashamra
Cheza +
cheza = chezacheza
Kimbia + kimbia
= kimbiakimbia
Sema+sema=
semasema
Zima+zima=
zimazima
Ruka+ruka=
rukaruka
Pia,
uradidi hujitokeza kama uradidi nusu. Uradidi nusu ni aina ya uradidi ambao
sehemu tu ya neno hurudiwa.
Mifano:
Ki +
zungu + zungu = kizunguzungu
Ki +
wili + wili = kiwiliwili
Ki +
nyume + nyume = kinyumenyume
Ki +
nyevu + nyevu = kinyevunyevu
Ki +
mbele + mbele = kimbelembele
Ki+china+china
= Kichinachina
Ki+baba+baba=kibabababa
Ki+leo+leo=kileoleo
Katika
mifano hiyo tumeona uambatanishaji wa mofimu tatu, yaani mofimu {ki-} na mofimu
huru mbili. Kiambishi awali {ki-} kinadondoshwa katika neno la pili. Kanuni:
{ki} +{m-huru} + {m-huru} = Neno.
Hivyo
ndivyo uradidi unavyojitokeza katika lugha ya Kiswahili. Uradidi ni miongoni
mwa njia ambazo zimekuwa zikitumika katika kuongeza msamiati wa lugha ya
Kiswahili. Mbali na uradidi, zipo njia zingine zinazotumika kuunda msamiati wa
lugha ya Kiswahili. Njia hizo ni: Utohoaji na uambatanishaji.
Marejeo
Massamba,
D.P.B (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa
ya Lugha. Dar-Es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Matinde,
R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na
Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti
Educational Publishers.
Rubanza,
Y. I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili.
Dar-Es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.