Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Pili

Taji la mfalme

Katika kijiji kimoja cha kijani, waliishi watu wenye furaha. Furaha yao ilidumu kwa miaka mingi mpaka walipovamiwa na simba mmoja mzee. Simba huyu mzee, alikuwa katili kwa wanakijiji, kijiji kikakosa amani na furaha yao ikateketea kama fedha za mlevi ziteketeavyo baa.

Simba mzee alianza unyama wake kwa kumuua mzee maarufu wa kijiji aliyependwa na watu wote. Inasemekana kuwa mzee alikuwa katika shamba lake akipalilia mahindi, ndipo alipovamiwa na simba mzee ambaye alimrukia shingoni na kumuua kisha akamla mpaka aliposhiba na kuacha sehemu ndogo ya mwili.

Simba mzee hakuishia hapo, aliwatafuna watoto wawili mapacha waliokuwa wakichoma viazi pembezoni mwa nyumba yao. Basi baada ya tukio hilo, habari ya simba huyo ikaenea kwa wanakijiji na kila mmoja akajifungia katika nyumba yake akiogopa kutoka kwa hofu ya yule simba mzee.

Kwa kuwa wanakijiji walijifungia ndani, simba yule mzee alipohisi njaa, akawinda watu asiwaone, akaanzisha kioja kipya, alianza kubomoa nyumba za watu na kuwatafuna wote aliowakuta humo.

Tukio la kwanza alivunja nyumba ya mganga wa kijiji, mganga alijifungia ndani kwake yeye na wanae, nao wakawa wamewasha moto ili waweze kuonana usiku ule, simba alivunja mlango wao, akaingia na kuwatafuna wote, hata mganga alitafunwa, kweli mganga hajigangi!

Nyumba ya pili ilikuwa ni nyumba ya mpiga ngoma wa kijiji, tukio hili husikitisha sana, kwani mpiga ngoma alikuwa na mke wake, mtoto wake mmoja wa kiume mwenye mwaka mmoja na mama yake mzazi, wote wakatafunwa na simba yule.

Wanakijiji waligundua kuwa, milango yao haikuwa imara kuweza kumzuia simba kuingia atakapo, lakini hawakuwa na namna yoyote ya kufanya, isipokuwa kukaa hivyo wakiomba miungu wasije uawa na Simba mzee. Pia walitamani kupeleka taarifa kwa mkuu wa wilaya ili atume jeshi lije kumwondoa Simba yule, lakini hakupatikana mwanamume aliyeweza kutoka ndani ya nyumba yake kwa hofu ya yule Simba. Basi kijiji kikawa kimya kama hakina watu. Inasemekana kwa sababu ya ule ukimya, hata hatua za sisimizi ziliweza kusikika!

Bwana Mako aliishi katika kijiji hicho, nyumba yake ilijitenga na nyumba za wanakijiji wengine, aliijenga katika kilima. Ungeziona, ungezani nyumba yake ni askari mkuu na zile zingine ni askari wadogo nao wanaamrishwa mguu pande mguu sawa!

Bwana Mako alishtushwa na ukimya wa kijiji, mwanzo alidhani labda shughuli zimewachosha hivyo kwa sababu ya uchovu hawana nguvu ya kupiga kelele.

Lakini baada ya siku kadhaa akahisi hatari, akaamua kuteremka kilimani ilipokuwa nyumba yake na kwenda kwa wanakijiji wengine.

Alitembea katika hali ile ya ukimya mpaka alipozifikia nyumba za wanakijiji wengine.

“Wanakijiji kulikoni, mbona kimya na mmejifungia ndani ya nyumba zenu?” aliuliza. “Tatizo nini ndugu zangu?”

Hakuna aliyejibu, wanakijiji walikaa kimya kwa hofu, pengine walidhani simba yule angetokea na kummeza Bwana Mako mara moja. Naye Bwana Mako kuona watu wako kimya, aliamua kusogea katika dirisha la fundi cherehani wa kijiji.

“Fundi, fundi,” alinong’ona. “Nieleze, tatizo nini?”

“Simba ndugu yangu,” alijibu, “anatafuna watu kama atafunavyo swala.”

Bwana Mako alipopata taarifa hizo, alisogea katikati ya nyumba zote.

Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tatu

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne