Ufahamu na Ufupisho | Kiswahili Kidato cha Tano na Sita

Kitabu kimefunuka kurasa

Ufahamu ni kujua au kulielewa jambo hatimaye kuweza kulifafanua. Mtu anaweza akaona, akasoma, ama akasikia jambo na akaelewa au asielewe. Akielewa atakuwa na uwezo wa kufafanua au kutoa taarifa zinazohusiana na habari hiyo.

Ufahamu wa kusikiliza na ufupisho

Ufahamu wa kusikiliza ni ule ambao mhusika anapata taarifa hiyo kwa kusikiliza habari hiyo. inawezekana kupata habari hiyo kwa kusimuliwa au kusomewa.

Ili kupata habari inayosikilizwa au inayosomwa, msikilizaji azingatie mambo haya:

-      Kuwa makini kwa kila kinachosimuliwa au kinachosomwa.

-      Kuhusisha mambo muhimu na habari isimuliwavyo.

-      Kujua matamshi ya mzungumzaji.

-      Kubainisha mawazo makuu.

Kujibu maswali kutokana na habari uliyoisikiliza

Mbinu za kujibu maswali kutokana na habari ya ufahamu wa kusikiliza ni:

-      Kusikiliza kila swali kwa makini.

-      Kutafakari kila swali, yaani kutafuta maana ya swali kwa kulihusisha na matini aliyosimuliwa.

-      Kujibu kila swali kwa ufupi na kwa usahihi, azingatie kiini cha swali na yaliyo katika matini.

Kufupisha habari uliyoisikia

Ufahamu wa habari uliyosikia una maana ya kueleza habari uliyoisikia kwa ufupi kwa kutumia maneno yako mwenyewe.

Hatua za ufupishaji wa habari uliyoisikia

1.   Kusikiliza habari kwa makini.

2.   Kubaini na kutambua mawazo makuu katika kila aya.

3.   Kuunganisha mawazo makuu na kueleza habari hiyo kwa maneno yako mwenyewe.

Habari hufupishwa mpaka kufikia theluthi ya habari ya awali.

Kichwa cha habari hupatikana mara baada ya kubaini mawazo makuu. Pia, kichwa cha habari hakitakiwi kuzidi maneno matano isipokuwa kama itaelekezwa vinginevyo.

Ufahamu wa kusoma na ufupisho

Ufahamu wa kusoma ni kuzingatia maana ya neno, sentensi na habari yote. Msomaji anatakiwa aweze kutambua mpangilio wa herufi, maneno na kuzitofautisha. Hivyo basi, msomaji hutakiwa kueleza jinsi alivyoelewa habari aliyosoma.

Ufahamu wa kusoma ni ule uelewa ambao hupatikana kwa: kusoma kwa sauti, kusoma kwa haraka na kimya na kusoma kwa makini.

Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kubainisha:

-      Mawazo makuu.

-      Maana ya maneno na misemo.

Kujibu maswali yanayotokana na makala uliyosoma

Ili kujibu maswali, msomaji anatakiwa kufuata hatua zifuatazo:

-      Soma makala inayohusika.

-      Soma maswali yaliyoulizwa ili kujua kinatakiwa nini?

-      Rudia kusoma makala yote. Safari hii soma kwa makini zaidi.

-      Tumia kalamu ya risasi kuweka alama katika sehemu ambazo unahisi ni majibu.

-      Baada ya kusoma tena habari na umeweka alama ya sehemu ambazo unahisi ni majibu, sasa jibu maswali.

Maswali yanaweza kutungwa katika namna ya maswali mafupi na maswali marefu.

Maswali mafupi huhusisha: maswali ya kuchagua, maswali ya kukamilisha jibu na maswali ya kuoanisha.

Maswali marefu ni yale yanayotaka kujibiwa kwa kuweka maelezo marefu.

Ufupisho (muhtasari) wa habari uliyosoma

Ufupisho wa habari uliyosoma ni kitendo cha kuelezea habari hiyo kwa ufupi. Ufupisho hukamilika pale msomaje anapounganisha mawazo yake mwenyewe ilimradi tu, habari hiyo iwe na mawazo sawa na ile habari anayoifupisha.

Ufupisho husaidia katika shughuli mbalimbali kama:

-      Wakati wa kutayarisha ripoti na kumbukumbu za mkutano.

-      Uhariri wa habari.

Kanuni za ufupisho

-      Kuwa na stadi zitakiwazo katika kusoma yaani ufahamu, ugunduzi na upangaji wa mambo maalumu yatakiwayo.

-      Habari iwe fupi.

-      Taarifa na maneno muhimu tu ndiyo yanayohitajika.

-      Habari ieleweke, isipoteze kiini chake.

-      Hoja na mawazo yaungane, yafuatane na yachukuane.

-      Sentensi ziwe kamili.

Hatua za ufupisho

-      Soma habari yote mpaka uielewe.

-      Chagua taarifa au maneno maalumu.

-      Kulinganisha taarifa muhimu na habari ya asili.

-      Kuandika muhtasari kama ilivyotakiwa.

-      Kukamilisha usawa wa ufupisho na habari ya asili.

Maswali

1.      Soma kwa makini kifungu hiki cha habari kisha jibu maswali yanayofuata.

UTUPU ni hali ya kutokuwa na kitu. Huenda ukawa utupu wa pochi, chumba, mali, akili na hata utupu wa mwili. Wahenga wa zamani (sio hawa wa mitandaoni), waliupuuza utupu kwa kusema, Mkono mtupu haurambwi.

Hali ya utupu hivi sasa inazidi kubadilika kwa kasi. Utupu umegeuka kitu. Utupu unategemewa kumvusha mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Tazama nyimbo za wanamuziki zilivyo. Wasichana wanaotumika humo  wanacheza utupu kabisa. Hawaogopi lolote na hata aibu hawaoni.

Zamani wazee walipotaka kumwaga laana, walitishia kuwaonesha watoto wakorofi utupu. Enzi hizo kuonekana kwa utupu ilikuwa ni laana kubwa. Wapo ambao walichanganyikiwa na kuwa wehu kwa sababu ya kadhia hii.

Vibinti vya zama hizi vinapiga picha za utupu bila kuogopa chochote. Ukiviuliza kwa nini vinafanya hivyo, utasikia vinajibu kuwa vinapenda kuwa hivyo… vinapenda kukaa utupu. Ujinga mtupu.

Hali ya mabinti kukaa utupu kwa kiasi kikubwa imepunguza hamu ya vijana kuoa. Ndio, vijana wanaona kila kitu. Sasa aoe ili aone nini kingine.

Maadili yamebadilika sana sasa. Ni kweli kuwa hapo zamani mwanadamu alitembea utupu. Lakini tamaduni hubadilika kulingana na wakati. Mwanadamu tangu kupata ustaarabu wake, utupu si jambo la kuonyesha hadharani.

Bado ninaendelea kutafakari nguvu hii ya utupu kukamata hisia za watu imetoka wapi? Ni kweli wanaowachezesha mabinti wakiwa watupu namna ile watafurahi wakiwaona watoto wa kuwazaa wao wakifanya vile? Lazima sasa turejee katika maadili. Heshima iwepo.

Jamaa mmoja aliwahi kunieleza kuwa, utupu kuzidi kuonekana mara kwa mara kumemwaga laaana kali katika jamii. Ndiyo maana kila kukicha limeibuka lile, mara limetokea hili.

Sina uhakika kama kuna sheria inayoeleza lolote kuhusu mavazi. Ni wakati wa kulitafakari hili kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Ni utupu wa fikra kuamini kuwa utupu unaweza kukupatia mafanikio. Sana utaambulia, kupata umaarufu wa mpito.

Maswali

a.      Toa maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika habari uliyoisoma.

i.        Wahenga.

ii.       Laana.

iii.      Sheria.

iv.      Zama.

v.       Tamaduni.

b.      Mwandishi ana maana gani anaposema “waliupuuza utupu kwa kusema, Mkono mtupu haurambwi.”

c.       Unaelewa nini kuhusu mabinti wa zama hizi? Toa maelezo kwa mistari isiyozidi mitatu.

d.      Kwa kutumia aya ya tatu, mwandishi ana mtazamo gani kuhusu wanamuziki.

2.      Fupisha habari uliyoisoma kwa maneno 100.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne