Sifa Bainifu za Irabu ya Kiswahili Sanifu

Chaki mbili, vitabu viwili na ubao wenye maandishi ABC

Fafanua kwa kina huku ukitumia mchoro sifa bainifu za irabu ya Kiswahili sanifu.

Irabu ni aina ya vitamkwa ambavyo hutolewa pasi, bila kuwepo kizuizi chochote katika mkondohewa au hewa itokayo mapafuni ikipitia katika chemba ya kinywa au ya pua iwapo irabu hiyo itasilimishwa. Irabu ziko za aina nyingi lakini tutatumia zaidi irabu za lugha ya Kiswahili. Katika kuainisha sifa za irabu ni lazima kuzingatia lugha ambamo irabu hizo zinatumika, kwa sababu kila lugha huchagua idadi ya irabu kadhaa kutoka katika bohari la sauti kwa kuzingatia irabu msingi ambacho ndicho msingi wa irabu za lugha mbalimbali.

Kuhusu lugha za Kibantu kuna irabu kuu tano ambazo hutumika karibu katika lugha nyingi za Kibantu na lugha ya Kiswahili ikiwemo kama asemavyo Massamba na wenzake (2004). Irabu hizo huwakilishwa kiimaandishi kama ifuatavyo.

Maandishi ya kawaida Maandishi ya kifonetiki

a) i                        [i] mfano katika neno lia, pi ka

b) e                      [ε] mfano katika neno cheka

c) a                      [a] mfano katika neno kale

d) o                      [ɔ] mfano katika neno pokea,bomani

e) u                      [u] mfano katika neno tume

Zifuatazo ni sifa bainifu za irabu ya Kiswahili sanifu:

Kigezo cha kwanza ni sehemu ya ulimi inayohusika na utamkaji wakati wa kutamka irabu hizo. Ulimi umegawanyika katika sehemu kuu tatu; mbele ambayo inajumuisha ncha ya ulimi, sehemu ya pili ni kati au bapa la ulimi, na sehemu ya tatu ni nyuma au shina la ulimi. Katika sehemu hizi tunapata sauti irabu mbalimbali kama ifuatavyo:

a) Sehemu ya mbele ya ulimi hutumika katika utamkaji wa irabu za kibantu za [i] na [ɛ], na irabu za lugha ya Kiingereza ambazo ni [i:], [e], [ɪ] na [æ]. Irabu hizi hutamkiwa sehemu ya mbele ya ulimi. Irabu hizi zinajulikana kama irabu mbele.

b) Sehemu ya kati ya ulimi hutumika au huhusika katika utamkaji wa irabu ya kibantu  [a] ijulikanayo irabu kati, na irabu za lugha ya lugha za Kiingereza ambazo ni  [ʌ], [ə] na [ɜ:] ambazo hujulikana kama irabu kati.

c) Sehemu ya nyuma ya ulimi huhusika katika utamkaji wa irabu [ɔ] na [u] za lugha  za Kibantu, vile vile huhusika katika utamkaji wa irabu za Kiingereza ambazo ni  [ɑ:], [ɒ], [ɔ:], [ʊ] na [u:] zijulikanazo kama irabu nyuma.

Kigezo cha pili ni mwinuko wa ulimi ndani ya chemba ya kinywa. Kifonetiki ulimi umegawanyika katika sehemu nne za miinuko ya ulimi. Miinuko hii ni mwinuko juu, mwinuko nusu juu (juu kati), mwinuko nusu chini (chini kati) na mwinuko chini. Katika miinuko hii sauti irabu huweza kuangukia ama kati ya mwinuko chini na nusu chini (chini kati) au chini au juu au kati ya juu na na juu kati au katikati ya juu kati na chini kati.

a) Mwinuko juu – huu unahusisha utamkaji wa sauti irabu [i] na [u] za lugha za  Kibantu na za lugha ya Kiingereza ambazo ni [i:] na [u:] zinazojulikana kama irabu juu.

b) Mwinuko juu kati – katika utamkaji wa mwinuko huu sauti irabu huangukia eneo lililoko kati ya juu na juu kati ambapo ulimi huinuka zaidi ya mwinuko juu kati kidogo ambapo tunapata sauti [ɪ] na [ʊ] irabu hizi ziajulikana kama irabu juu kidogo ya juu kati.Wakati sauti irabu za kibantu [ε] na [ɔ] hutamkiwa katika mwinuko wa juu kati. Irabu hizi zinajulikana kama zenye sifa ya kati ya juu kati na chini kati.

c) Mwinuko chini kati – katika mwinuko huu sauti irabu za lugha za Kibantu ambazo  hutamkwa katika mwinuko huo ni [e] na [o] na katika lugha ya Kiingereza  irabu hizi huangukia katikati ya mwinuko juu kati na chini kati. Irabu hizo ni [e], [ɔ:], [ɜ:] na [ə] sauti hizi mwinuko wa ulimi si juu kati wala si chini kati halisi bali uko kati ya juu kati na chini kati.

d) Mwinuko chini – katika mwinuko huu irabu [a] ya lugha ya Kibantu hutamkiwa na sauti [ɑ:] ya lugha ya Kiingereza hutamkiwa katika mwinuko huo. Lakini kuna sauti irabu [æ] na [ɒ] za lugha ya Kiingereza hutamkiwa juu kidogo ya mwinuko chini wakati irabu [ʌ] hutamkiwa kati ya mwinuko chini na chini kati (nusu kati) , nayo ni irabu ya lugha ya Kiingereza.

Kigezo cha tatu ni hali ya midomo wakati wa utamkaji wa irabu. Hapa hali ya midomo au umbo la midomo huwa katika hali tatu, uviringo, msambao na utandazo au hali ambayo si bainifu.

a) Uviringo wa midomo, hali au umbo hili la midomo huhusu utamkaji wa sauti irabu [ɔ] na [u] za lugha za Kibantu wakati huo huo huhusu utamkaji wa irabu [ɔ:], [ɒ], [ʊ] na [u:] za lugha ya Kiingereza.

b) Msambao wa midomo, hali au umbo hili la midomo huhusu utamkaji wa irabu [i] ya lugha za Kibantu na irabu [i:], [ɪ] na [æ] za lugha ya Kiingereza. Midomo inapokuwa imesambaa kama kwamba unataka kutabasamu basi sauti au irabu hizi hutamkwa.

c) Utandazo wa midomo, hali ya midomo inapokuwa si mviringo wala si msambao huitwa hali ya midomo si bainifu au ya utandazo. Umbo hili la midomo huhusu utamkaji au hupelekea kutamkwa kwa sauti irabu [a], [ɛ] na [e] za lugha za Kibantu wakati huo huo irabu [e], [ɑ:], [ʌ], [ɜ:] na [ə] za lugha ya Kiingereza.

Mchoro huu unaonesha sifa za irabu ya Kiswahili kwa kuzingatia sehemu ya ulimi wakati wa utamkaji na mwinuko wa ulimi



Mchoro huu unaonesha sifa za irabu kwa kuzingatia mkao wa midomo



Hivyo ndivyo vigezo vyote vya msingi katika kubainisha sifa pambanuzi za irabu zinazozitofautisha irabu moja na irabu nyingine. Kwa mwanafunzi wa somo la fonolojia na mwanaisimu wa lugha lazima azingatie vigezo hivi, vipo katika upambanuzi wa sifa bainifu za irabu.


Marejeo

Makoba, D. (2017). Faida za Matumizi ya Alama za Kifonetiki. Imepatikana https://www.mwalimumakoba.co.tz/2017/09/faida-za-matumizi-ya-alama-za-kifonetiki.html

Clements, G.N (1983) CV Phonology: Generative Theory of the Syllable. MIT Press, Combridge Mar

Jones, D (1918) An Outline of English Phonetics. New Delhi, Kalyani Publishers.

Katamba ,  F (1986) An Introduction to Phonology. New York, Longman Publishers

Kennedy, M. S (1967) Perception of the Speech Code. University of Toronto Press.

Kihore, Y.M, Massamba , D.P.B na Msanjila, Y.P (2003) Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. Sekondari na Vyuo. Dar es salaam. TUKI

Massamba, D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2004) Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Sekondari naVyuo. Dar es salaam. TUKI

Mgullu, R. S (1999) Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na Fonolojia ya Lugha ya Kiswahili. Nairobi. Longhorn Publishers

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne