Ufahamu | Kiswahili Kidato cha Pili

Vitabu vimerundikwa.

Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi. Ufahamu wa mtu waweza kupimwa katika kusikiliza jambo au katika kusoma.

Ufahamu wa kusikiliza

Ufahamu wa kusikiliza, ni uwezo wa mtu kuelewa maneno anayoyasikiliza. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe.

Kujibu Maswali ya Ufahamu kutokana na Habari uliyoisikiliza

Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha:
-      Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa
-      Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza.
-      Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa.
-      Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo:
-      Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema.
-      Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha hoja.
-      Msomaji anatakiwa kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumasidia kukumbuka hapo baadae.
-      Kuwa makini na ishara mbambali za mwili kama vile kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho. Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika mazungumzo.

Kufupisha kwa Mdomo Habari uliyoisikiliza

Ili kuweza kufupisha kwa mdomo habari uliyoisikiliza yapo mambo ya kuzingatia. Mambo hayo ni:
-      Kubaini mawazo makuu yanayopaswa yajitokeze katika habari iliyofupishwa,
-      Kupanga maelezo kwa usahihi katika usemaji,
-      Kuzingatia kichwa cha habari ambacho kinapaswa kihusiane na ufupisho na wazo kuu na mwisho ni
-      Kusema ufupisho kwa ufasaha na kwa lugha ambayo ni nzuri.

Ufahamu wa kusoma

Ufahamu wa kusoma ni ule mtu anaoupata kwa njia ya kusoma. Inaweza kuwa ni kusoma kitabu, gazeti, makala na maandishi mengine.

Kusoma kwa Sauti kwa kuzingatia Lafudhi ya Kiswahili

Kuna vipengele viwili vinavyounda mchakato wa ufahamu wa kusoma:
-      Uelewa wa msamiati na
-      Uelewa wa matini.

Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:

-      Kubaini mawazo makuu; msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatakiwa ajiulize, Je, kinachoongelewa hapa ni nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi kwake kuielewa habari hiyo.
-      Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi kama mkato, nukta, nukta-mkato, n.k., kwa kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
-      Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
-      Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.

Kujibu Maswali kutokana na Habari uliyoisoma

Ili kujibu maswali yanayotokana na habari uliyoisoma inatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
-      kubaini mawazo makuu,
-      kuzingatia alama za uandishi,
-      kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali na kutilia maanani vidokezo vya maana. Aidha mawazo yanapaswa kuelekezwa katika jambo linalosomwa, kujiuliza maswali kadri unavyosoma na kuandika ufupisho.

Kufupisha Habari uliyoisoma

Ili kuandika ufupisho mzuri wa habari uliyosoma yapaswa kuzingatia yafuatayo:
-      kuisoma habari uliyopewa zaidi ya mara moja,
-      kubainisha mawazo makuu,
-      kuandika ufupisho kwa lugha fasaha na yenye mtiririko mzuri wa hoja,
-      kuhesabu idadi ya maneno na kuhakikisha haizidi idadi inayotakiwa na kupitia habari ya mwanzo na kisha ufupisho ili kuona kama taarifa muhimu haijaachwa au kusahaulika.
Kusoma hakutakiwi kuwe kwa lengo la kujikumbusha masomo ya shule pekee, bali, watu wasome kwa burudani. Hii itawasaidia kupata maarifa zaidi ya yale yaliyomo darasani.

Matumizi ya kamusi

Kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa katika utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa.

Jinsi ya Kutumia Kamusi

Maneno yanayoingizwa katika kamusi hupangwa kwa utaratibu wa alfabeti. Maneno yanayoanza na herufi a, yote huwekwa chini ya herufi A. Maneno yanayoanza na herufi fulani nayo hupangwa katika utaratibu wa alfabeti kwa kuzingatia herufi ya pili, ya tatu, nne au tano ya neno kama mfano hapa chini unavyoonyesha.
Mfano:ja, jabali, jabiri, jadhibika, jadi.
Maneno yote yanaanza na herufi [j]. herufi ya pili kwa maneno yote ni [a]. herufi ya tatu ni [b] na [d]. Kwa kuwa [b] hutangulia [d] katika mpangilio wa alfabeti maneno yenye [b] kabla ya yale yenye [d]. Kwa kuwa maneno yenye herufi [b] ni mawili itabidi tutazame herufi ya nne ya hya maneno ili tuchague litakaloorodheshwa mwanzo. Neno ‘jabali’ litaorodhewshwa kabla ya ‘jabiri’ kwa kuwa [a] (herufi ya nne) ya ‘jabali’ hutangulia [i] ya ‘jabiri’ ambayo pia ni herufi ya nne. Kisha tunatazama maneno yenye [d] kama herufi ya tatu. Hapa tunaangalia pia herufi ya nne ili kubaini neno litakaloandikwa mwanzo kati ya ‘jadhibika’ na ‘jadi’. Kwa kuwa [h] hutangulia [i] basi ‘jadhibika’ huorodheshwa mwanzo ndipo lifuatiwe na ‘jadi’.
Kwa hiyo hivi ndivyo unavyopaswa kutafuta neno kwenye kamusi. Nenda kwenye herufi ya neno ulalotafuta alafu litafute kwa kufuata mlolongo huo huo wa herufi ya kwanza kuorodheshwa.
Neno linaloorodheshwa kwenye kamusi ili lifafanuliwe linaitwa kidahizo. Kidahizo huandikiwa maelezo ya kukifafanua. Maelezo haya ni matamshi ya kidahizo, maana ya kidahizo, kategoria ya kisarufi, sentensi ya mfano wa matumizi ya kidahizo n.k. Kidahizo pamoja na maelezo yake ndio huitwa kitomeo cha kamusi.

Maswali

1.   Soma habari ifuatayo kisha jibu maswali:
ANA wajukuu wanne, umri wake ni miaka 70, na kila mmoja hushangazwa na muonekano wake! Ni bibi asiye mzee.  Ajabu kubwa!
Siri pekee inayomfanya awe na muonekano huo ni aina ya vyakula anavyokula na kuzingatia mazoezi ya kutosha. Anazingatia anachoweka mdomoni na miguu yake haiishi kutembea.
Bibi huyu, anayetokea Perth, Australia, wakati alipokuwa na umri wa miaka 40 alitahadharishwa na madaktari kuwa endapo angeshindwa kubadili mtindo wa maisha, punde angeugua maradhi ya kisukari. Ili  kuokoa maisha yake, akaamua kuvipa kisogo vinono vyote, na huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya. Ni mwanzo huu unafanya tumzungumzie! Siri ya Bi Carolyn Hartz kuonekana kama binti mdogo.
Ukiachilia mbali vyakula sahihi anavyokula, hulala kwa muda wa saa saba, kujishughulisha na kazi zake binafsi siku nzima, na kama ilivyo asili ya wanawake wengine, hutumia muda kiasi kujipamba. Kipo cha kujifunza kutoka kwa bibi huyu.
i.             Kipi kinafaa kuwa kichwa cha habari hii?
ii.            Taja siri pekee inayomfanya Bi Caroly Hartz kuwa na mwonekano alionao sasa?
iii.           Toa maana ya neno kuvipa kisogo vinono vyote.
iv.          Kwa mujibu wa kifungu hiki cha habari, unafikiri ni ipi njia sahihi ya kufukuza maradhi?
v.           “Kipo cha kujifunza kutoka kwa bibi huyu.” Taja mafunzo manne uliyoyapata.
2.   Fupisha habari hiyo kwa maneno yasiyozidi 60
3.   Eleza maana ya maneno yafuatayo:
i.             Kamusi ii. Kidahizo iii. Kitomeo
4.   Ukitumia kamusi ya Kiswahili sanifu, orodhesha vitomeo vifuatavyo na vidahizo vyake:
i.             Utunzi ii. Mfumbati iii. Tumbawe iv. Vanga
5.   Nini maana ya msamiati?
6.   Fafanua dhima kuu za kamusi.
7.   Eleza maana ya:
a.   Alfabeti b. kategoria
8.   Eleza faida moja ya maneno kwenye kamusi kupangwa kwa alfabeti.
9.   Panga maneno yafuatayo kama jinsi yanavyotakiwa kutokea katika kamusi:
Papa, pepo, popo, pipi, paipu, pua, pau, papo, pepeta, papatika, punda, pepopunda, pepesuka.
10.               Taja tofauti iliyopo kati ya ufahamu wa kusikiliza na ufahamu wa kusoma.
11.               Nini maana ya:
a.   Vitomeo b. tauria
12.               Unaelewa nini kuhusu usomaji wa ziada.

Marejeo

Kaduguda na Wenzake, (2018). Kiswahili Kidato cha Pili. Oxford University Press: Dar es Salaam.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie