Jinsi ya Kusoma Bila Kusahau Ulichosoma
Kwa
muda mrefu nimekuwa nikiitwa na waziri niende kumfundisha binti yake ambaye ni
mwanafunzi jinsi ya kusoma bila kusahau alichosoma. Binti huyu ana tatizo la
kusahau anaposoma na kupelekea matokeo mabaya ambayo mwisho wake ingekuwa
kurudia darasa ama kuhamishwa shule. Baada ya kumpiga chenga waziri kwa muda
mrefu, hatimaye siku moja wakati wanafunzi wapo likizo, nilipata muda, haraka
nikaelekea nyumbani kwa waziri.
“Umebeba
nini?” aliniuliza mlinzi wa waziri baada ya kunikagua kwa kifaa cha ukaguzi.
“Beretta.”
Nilijibu.
“Iache
hapa ukitoka utaichukua.”
“Sawa.”
Nikafanya alivyotaka kisha nikaingia ndani. Waziri alinipokea kwa furaha tele. Tulizungumza
habari za siasa mpaka tukachoka, sasa nikaomba nionane na yule niliyemfuata. Kama
nilivyosema awali, binti waziri amekuwa akisoma kwa bidii lakini anasahau
anachosoma.
Nilikuwa
uso kwa uso na msichana mdogo anayesahau kila akisoma. Nilihisi kama
ananiogopa, hivyo nikaamua kumuuliza swali la kumfanya anizoee.
“Mimi
ni mtu au ng’ombe?” niliuliza, binti akacheka, nikahesabu meno yake, ishirini
na nane, hapo nikagundua nilikaa na msichana mdogo wa miaka 16.
Baada
ya mazungumzo ya hapa na pale, hatimaye nikampa somo lililobadili maisha yake:
JINSI YA KUSOMA BILA KUSAHAU ULICHOSOMA
1.
Penda
unachosoma
Ukisoma
kitu unachopenda kuna uwezekano mkubwa wa wewe kukumbuka. Ni nyimbo ngapi
unaweza kuziimba, wala hukufanya bidii yoyote kuzikariri nyimbo hizo lakini
zipo kichwani. Ni kwa sababu ulizipenda nyimbo hizo. Hivyo unaposoma, penda
kile unachosoma. Soma ukitabasamu, usikunje sura, elimu siyo vita!
2.
Kuwa
na malengo wakati wa kusoma
Unapoanza
kusoma, jiulize, ‘kwa nini ninasoma kitu hiki?’ kwa mfano, kama unasoma mada ya
uandishi, basi lengo lako ni kuelewa uandishi wa vitu mbalimbali kama vile
barua, insha, risala, hotuba na vitu mbalimbali, hivyo inategemewa mwisho wa
kusoma kwako, utakuwa umefahamu vitu hivyo.
3.
Jipime
mwenyewe unaposoma
Unaposoma,
kuwa na kalamu na daftari. Baada ya kila kipengele, jipime ili kuona kama
unakumbuka. Kwa mfano kama unasoma mada ya ‘establishment of colonialism’ na
umefika kipengele cha ‘methods used to establish colonialism’ fanya hivi. Kwanza
andika kipengele hicho juu ya daftari, ‘methods used to establish colonialism.’
Baada ya hapo zisome njia hizo. Ukimaliza kuzisoma, ziorodheshe njia hizo bila
kuangalia katika daftari. Unaweza kujikuta umekumbuka moja, mbili na pengine unaweza
kukumbuka zote. Baada ya kuorodhesha, tazama zile ambazo ulizisahau kisha endelea
na kipengele kinachofuata.
4.
Jenga
picha katika kichwa chako
Tunakumbuka
zaidi picha kuliko maneno. Kwa mfano, unaposoma somo la Historia (leo sijui kwa
nini mifano yangu ipo katika somo la historia.) unaposoma somo la historia,
mada ya ‘colonial social services’, jenga picha kichwani mwako, kuwa kama
unaona huduma za kijamii zilizotolewa na wakoloni, jenga picha ya shule za
zamani, barabara na reli. Jenga picha ya mabomba na nyumba za wakoloni bila kusahau
hospitali zao. Ukifanya hivi, huwezi kusahau.
5.
Rudia
tena na tena
Ukirudia
mara nyingi, utakumbuka mara nyingi. Usisome mara moja ukaona umemaliza, rudia
tena na tena. Pale unapofundishwa darasani isome mada hiyo. Unapokuwa na muda
soma tena. Unapotangaziwa mtihani soma tena. Mada moja ukiirudia kuisoma mara
saba kwa vipindi tofautitofauti, huwezi kuisahau!
6.
Fanyia
mazoezi ulichokisoma
Njia
hii ni bora na inasaidia kukumbuka kwa haraka zaidi. kuna njia mbili za
kufanyia mazoezi kile ulichokisoma:
Njia
ya kwanza ni kumfundisha mtu kile ulichosoma. Soma, kisha muite rafiki, anza
kumfundisha ulichosoma.
Njia
ya pili soma mada fulani, kisha ita marafiki katika majadiliano ili kujadiliana
kuhusu mada hiyo. Wakati wa majadiliano, toa hoja zako kuhusu mada hiyo. Utakuwa
umefanyia mazoezi ulichosoma.
Nilimalizana
na binti waziri. Nikaondoka zangu. Baada ya miezi kadhaa, nilianza kupokea
meseji za pongezi kutoka kwa waziri. ‘Mwalimu Makoba, binti hasahau masomo siku
hizi. Anafaulu vizuri na hawezi kurudia darasa.’
Akirejea
tena, nitamfundisha mbinu saba za kufaulu mtihani wowote shuleni.
Hata wewe unaweza kusoma bila kusahau masomo yako endapo utazingatia mambo niliyofundisha hapo juu.