Bwana Mako na Ndege Yake 1 | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 3

Bwana Mako akiwa na upanga wa kung'aa

Mkasa wa Tatu

Bwana Mako na Ndege Yake

Sehemu ya Kwanza

Kwa muda mrefu Bwana Mako alitamani kuitembelea Dunia aione yote akiwa juu. Ndipo alipopata wazo la kutengeneza ndege ambayo ingemsaidia kutimiza malengo yake. Umbo la ndege lilitengenezwa kwa mbao za mninga, ndani aliweka furushi kubwa la nyasi ambalo lingetumika kama kiti cha rubani, nyuma ya kiti cha rubani aliweka godoro nene, hili lingetumika kulala pale anapokuwa amechoka na muda huo ndege ingekuwa katika ‘autopilot.’ injini za ndege hii na namna ilivyofanya kazi, ilikuwa siri yake Bwana Mako.
Aliamka asubuhi kabla mkewe na mtoto wake mdogo hawajaamka. Aliandika ujumbe katika kikaratasi, “Nakwenda ziara, nitarudi baada ya siku tatu.” kisha akaelekea mpaka mahali alipoegesha ndege, akaingia humo, alipokaa vyema, akavuta kigingi cha kwanza, ndege ikaunguruma kwa sauti kubwa na kuanza kuserereka taratibu kama maharusi. Baadaye iliongeza kasi, ikaserereka kwa sekunde chache, kisha akavuta kigingi cha pili, ndege ikaanza kunyanyuka juu, hapo akatazama chini kukiona kijiji chake, loooh! Kumbe wanakijiji waliamshwa na yale makelele ya ile ndege, wote walikuwa nje ya nyumba zao, kuona hivyo, akafungua mlango haraka, akawapungia mkono na kuwafanyia ishara ya kwamba angerejea baada ya siku tatu, akimaliza kufanya hivyo, akaufunga mlango.
Ndege ilikuwa imepaa juu kiasi alichokitaka, akagusa kigingi cha tatu, ikawa sawia huku ikisonga mbele, aliweza kuiona Dunia kwa namna alivyotamani. Aliliona bara la Afrika kama alionavyo katika ramani, akaongeza mwendo zaidi, ndege ikawa inatembea mwendo wa kunguru kumi na tisa kwa saa! Alipoiona Afrika ya Kusini, alitamani atue, awacharaze bakora vijana wahuni wa pale, lakini akapanga kurejea siku nyingine.
Mpaka giza linaingia, alikuwa ameliona bara la Afrika, Amerika ya kusini na sehemu kubwa ya bara la Amerika ya kaskazini. Kwa sababu giza lilimzuia kuona, aliamua kutua Marekani ili kukikucha, apae tena na aweze kuendelea na safari yake ya udadisi. Basi akapapasa mkono wake ili akishike kigingi cha nne, masikini! Kigingi hakikuwepo, alisahau kukiweka kwa sababu ya ile haraka yake ya kutaka kuizunguka Dunia.
Ndege iliendelea kupaa, naye akawa anawaza namna ya kutua, akiendelea kuwaza, ghafla aliona kitu kama kilele cha mlima, akashika haraka kigingi cha pili, ndege ikapaa juu zaidi. Lakini kwa sababu ya kule kupaa juu kwa ghafla na kasi iliyokuwepo, Bwana Mako akateleza na kudondokea upande wa nyuma kulikokuwa na kitanda. Alijaribu kurejea katika kiti chake cha rubani lakini hakuweza, basi akabaki kuangalia jinsi ndege ilivyokuwa ikielekea juu asiyejua hatma yake.
Ndege ilikwenda juu kwa kasi kubwa kwa muda wa saa kumi na nne. Muda wote kulikuwa giza. Lakini baadae mwanga ulionekana ghafla na kumshitua Bwana Mako aliyekuwa amekata tamaa. Akiendelea kutazama vizuri ili atambue eneo hilo, ndege ilianguka chini, ikapasuka vipande viwili, bahati njema kumbe alijua angeanguka muda wowote, hivyo alikuwa tayari kajifunga katikati ya godoro na hivyo akanusurika, pengine na yeye angepasuka vipande kama ile ndege yake.
Alisimama haraka na kuanza kuchunguza mahali pale ili abaini alikuwa wapi, japo alitazama kwa jicho la udadisi hakuweza kutambua wala kufananisha. Ilikuwa sehemu ya tofauti, tambalale yenye nyasi fupi ngumu ajabu!
Akiendelea kushangaa, alishtushwa na sauti ya vishindo, alipotazama mbele, aliona Jitu kubwa refu lipatalo futi hamsini na unene wake ni kama mibuyu miwili. Bwana Mako mwenye futi tano nukta nane, alionekana kiumbe mdogo ilhali Duniani alikotoka yeye ni miongoni mwa watu warefu. Basi kwa kuhofia, alikimbia akajificha nyuma ya mbao mojawapo ya ndege.
“Usijifiche,” jitu lilisema kwa upole, “nimekuona tangu unadondoka na chombo chako. Siwezi kukudhuru kiumbe mdogo.”
Bwana Mako alisogea karibu na Jitu akizungumza, lakini kwa sababu ya ule urefu wake, Jitu halikuweza kumsikia, hivyo lilimbeba likamweka juu ya bega lake mahali palipo karibu na sikio mazungumzo yakaendelea.
“Asante kwa msaada, hapa nipo wapi?” aliuliza Bwana Mako.
“Hapa ni Mailanda, nchi ya mfalme Solupa, katika bara la pili kati ya matatu yaliyopo katika sayari yetu isiyo na jina.” Jitu lilijibu. Bwana Mako akagundua kuwa, ndege yake ilimshusha katika sayari nyingine ya watu hao wakubwa.
Waliendelea kuzungumza, Bwana Mako alisimulia alivyotengeneza ndege yake na jinsi alivyosafiri, alisimulia yote bila kuacha kitu. Mwisho jitu liliahidi kumsaidia kurudi nyumbani, lakini lilimtaka limpeleke nyumbani kwa jamaa zake ili apumzike. Wakati wanaondoka, lilimuweka Bwana Mako katika mfuko wa shati, kisha likayabeba mabaki yote ya ndege kwa mkono mmoja na kuanza kutembea kuelekea uliko mji.

Jiunge katika Group la whatsapp uwe wa kwanza kupokea mkasa Unaofuata Bofya Hapa Kujiunga

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie