SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya nane)
Looh! Sikuamini, niliiona Mapandagila 214 ikiwa imeegeshwa mbali kidogo, niliruka kwa furaha nikamkumbatia Chokusi, akanikwaruza ubavuni kwa vile vyuma vyake, sikuhisi maumivu. Lakini tena nikakumbuka jambo, nikauliza.

            “Lakini nilipodondoka iliharibika kabisa… nitawezaje kupaa tena?”

            “Niliitengeneza… kwa sasa iko vizuri na itakufikisha salama huko uendako.”

Nilimkumbatia tena kwa furaha, lakini kabla sijamwachia, akanipiga mweleka, wote tukalala chini.

            “Askari wanakuja na makombora, wamekwishagundua kuwa umetoroka, tambaa mpaka katika ndege yako, usinyanyue kichwa wala kugeuka nyuma, kwa heri.

Chokusi alirudi katika shimo haraka, mimi nilitambaa kama nyoka kuelekea ilipokuwa Mapandagila 214, nikayasikia makombora mazito yakirushwa, nikakaza mwendo.

Kombora moja lilinikosa mguuni, nikajivuta kushoto, nikatazama juu, ndege nyingi ziliranda… nilikwishaonekana, sikuwa na ujanja, nikajivuta mpaka katika jiwe kubwa nikaegama huku nikipiga hesabu za kuifikia Mapandagila 214 bila kuguswa na makombora yale.

Nikiwa nimeegama katika jiwe hatua chache kuifikia Mapandagila, kombora kubwa lilirushwa, Mapandagila 214 ikasambaratishwa vipandevipande. Nililia kwa  uchungu wa kukipoteza chombo hiki kilichokuwa fahari ya nchi yangu, chombo kilichotumia pesa nyingi na maarifa kukitengeneza kilisambaratishwa maramoja bila huruma. Sikujua ni vipi ningetoka salama katika mikono ya adui.

Ndege za adui zilitua, wanajeshi wengi wakashuka na kuanza kuja mahali nilipokuwa, ujanja wangu wote ulibaki mfukoni.

Lakini ghafla, makombora mazito yalirushwa na kuzisambaratisha ndege za adui, kisha chuma kizito kikashushwa, kikawavuta wale watu wa chuma na kuwanasa kama gundi. Niligundua baadae kuwa chuma kile ilikuwa sumaku yenye nguvu sana.

Nilipepesa macho, nikakiona chombo cha masafa ya anga kikitua, ubavuni kiliandikwa MAPANDAGILA 428. Nilitabasamu kwa furaha kwani niligundua chombo kile kilitoka Duniani na bila shaka kilikuja kuniokoa.


Baada ya chombo kile kutua, mlango ulifunguliwa akatoka msichana mdogo mrembo aliyevalia mavazi meupe, nikapepesa macho vizuri ili niweze kumuona, sikuamini macho yangu baada ya kuibaini sura yake, alikuwa Minza binti mfalme kutoka nchi yangu ya Vumu, sikuweza kujizuia niliachia kicheko cha furaha.

itaendelea Jumapili...

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne