Mtihani wa Kiswahili 2 kwa Wanafunzi wa Kidato cha Sita 2

Mtihani wa Kiswahili 2 kwa Wanafunzi wa Kidato cha Sita 2

Endapo unataka kufanya mtihani huu ili usahihishwe na Mwalimu, zingatia mambo haya:
1. Mtu yeyote na popote alipo anaruhusiwa kufanya mtihani huu.
2. Fanya mtihani huu kwa kutumia aina yoyote ya karatasi.
3. Ukimaliza, piga picha karatasi hizo kisha zitume WhatsApp kwenye namba ya Mwalimu Makoba, 0754 89 53 21. Bofya hapa kusoma maelekezo yote.
Muda: Saa 3
Sehemu A (Alama 20)
Fasihi kwa Ujumla
1. Kwa kutumia mifano katika jamii ya Tanzania, jadili mambo manne muhimu yanayoweza kumfanya mwandishi apoteze uhuru wake.
2. Ni kwa namna gani fasihi inatofautina na sanaa zingine kama ususi, uchongaji na uchoraji. Toa hoja tano.
Sehemu B (Alama 20)
Ushairi
3. “Washairi wengi huimarisha jamii zao kwa kuyataja maovu.” Tetea usemi huu kwa kutoa hoja nne kwa kila kitabu katika diwani mbili ulizosoma.
4. “Viongozi hawana huruma na watu wao.” Jadili ukweli wa kauli hii kwa kutoa hoja nne kwa kila kitabu katika diwani mbili ulizosoma.
Sehemu C (Alama 20)
Riwaya
5. “Waandishi wa kazi za fasihi hufanya kazi ya kuishauri jamii ya Tanzania.” Fafanua kauli hii kwa hoja nne kwa kila kitabu kutoka katika riwaya mbili ulizosoma.
6. “Kazi ya fasihi huwa na wahusika ambao huibua dhamira mbalimbali.” Thibitisha kauli hii kwa kutoa hoja nne kwa kila kitabu.
Sehemu D (Alama 20)
Tamthiliya
7. “Waandishi wa kazi za fasihi hulenga katika kuumba upya jamii zao.” Fafanua mbinu tano kwa kila kitabu katika tamthiliya mbili ulizosoma zilizopendekezwa na waandishi kama nyenzo za ujenzi wa jamii mpya.
8. Tamthiliya nyingi ni za machungu kutokana na ujumbe mzito unaobebwa kwa jamii. Thibitisha dai hili ukifafanua hoja nne zinazodhihirisha machungu kwa kila kitabu katika tamthiliya mbili ulizosoma.
Sehemu E (Alama 20)
Usanifu wa maandishi
9. Soma habari ifuatayo kisha jadili mbinu za kifani zilizotumika kufikisha ujumbe.
Hakuna kilichobaki, wamekula kila kitu. Sasa njaa imetanda, hakuna aliyesalama, labda wezi wachache wenye vitambi laini vya dhambi.
Njaa inawatandika wasio na ajira na wenye ajira. Yote haya yamesababishwa na watu walioaminiwa, wakawekwa pale juu lakini wakafanya mambo yanayoshusha kila kitu. Upuuzi.
Sauti ilisikika katika chumba alicholala Mzee, aliwakamata mkono wajukuu zake wawili na kuanza kuwausia.
“Wajukuu sikieni, haya maradhi ya umasikini nimepambana nayo ningali na nguvu nyingi kama nyinyi, lakini wapi, umasikini umenitandika vilivyo hata sina hamu.
Sasa nawaomba nyinyi, mpambane na huyu adui. Hata hivyo, sidhani kama mtaweza, lazima mtarudishwa nyuma na wale jamaa wenye vitambi laini.
Hata hivyo, ipo namna ya kupambana na huyu adui. Ipo namna nawaambia, hata hivyo msiniulize kwa nini mimi sikuitumia mpaka sasa nakufa katika chumba hiki kisicho na heshima, nisikilizeni kwa makini, mkitaka kufanikiwa tumieni njia hii ninayowaambia.
Njia pekee ya kuushinda umasikni ni kufanya kazi kwa bidii, na njia sahihi ya kuwashinda wale wenye vitambi laini ambao hata mkifanya kazi kwa bidii lazima watawarudisha nyuma… njia pekee ya kuwashinda wenye vitambi laini ni…”
Mzee hakumaliza neno lake. Alikata roho kabla hajatoa njia. Wajukuu walilia, kwani walijiona nao wakihangaika na mwisho wangekufa kifo cha mzee.
Kifo cha masikini ni kituko sana, kama hakijatokea kitu. Teh! Teh!

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024