Uhakiki wa Riwaya ya Usiku Utakapokwisha

usiku utakapokwisha

RIWAYA: USIKU UTAKAPOKWISHA
MWANDISHI: MBUNDA MSOKILE
MWAKA: 1990
WACHAPISHAJI: DUP
MHAKIKI: DAUD MAKOBA (MWALIMU MAKOBA)

Utangulizi

Usiku Utakapokwisha ni riwaya inayojadili matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii ya Mtanzania.
Ukosefu wa ajira unafanya vijana watatu, Chioko, Gonza na Nelli wasifikie ndoto zao za mafanikio.
Kitabu hiki japo kinajadili mambo kadha wa kadha, lakini kimejikita sana katika matatizo ya kiuchumi.

Maudhui

Dhamira
Rushwa
Viongozi wako msitari wa mbele katika kutoa na kupokea rushwa. Chioko anashindwa kupata ajira kwa sababu hakuwa na rushwa.
Umasikini
Familia nyingi zinaishi katika lindi zito la umasikini. Mwandishi anaonyesha jinsi ambavyo umasikini umelitawala tabaka la chini. kwa mfano, familia moja inakufa Buguruni kwa kukosa chakula.
Mapenzi
Mwandishi amejadili mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo. Mapenzi ya kweli yameonekana kwa Chioko. Kijana huyu anampenda kwa dhati mpenzi wake Nelli. Hata anaposhauliwa na rafiki yake Gonza kuwa amshawishi Nelli ahonge penzi ili apate pesa, Chioko anakataa katakata.
Mapenzi ya uongo hayakuachwa. Mwandishi ameonyesha wanawake wakipenda wanaume kwa sababu ya pesa.
Mapenzi ya pesa yanatokana na sababu ya hali ngumu ya maisha inayowakabili watu wa hali ya chini.
Wizi na ujambazi
Kutokana na ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha, Gonza anajiingiza katika ujambazi. Hapo mwandishi anaonyesha namna ambavyo tatizo la ukosefu wa ajira linavyoweza kuleta matatizo lisipotafutiwa ufumbuzi.
Nafasi ya mwanamke katika jamii
Mwanamke amechorwa kama:
-      Chombo cha starehe. Viongozi na mameneja wanawatumia wanawake pindi wanapokwenda kutafuta kazi.
-      Kiumbe duni na asiye na maamuzi. Katika jamii ya Chioko watu wanaamini kuwa kazi ya mwanamke ni kuzaa, kupika na kumtumikia mume.
-      Mshauri mzuri. Nelli anawashauri Gonza na Chioko kurudi kijijini, japo Gonza na Chioko wanakataa, lakini huu ni ushauri mzuri sana ambao ungewanufaisha endapo wangeuzingatia.
-      Mwenye mapenzi ya kweli. Nelli anampenda kwa dhati Chioko.

Ujumbe

i.             Ili tuweze kujenga jamii mpya ni lazima tupige vita rushwa.
ii.            Jamii ishirikiane kwa pamoja kuondoa umasikini.
iii.           Wizi si suluhisho la umasikini. Gonza anaiba ili aondokane na umasikini, hapati anachotaraji, badala yake anauawa kwa kupigwa risasi.
iv.          Tatizo la usafiri litatatuliwa endapo serikali itajenga miundombinu mingi.

Migogoro

Migogoro ya wahusika
-      Gonza na Chioko. Gonza anamtaka Chioko waende Zambia ambako kuna maisha mazuri. Chioko anakataa na kusababisha wawili hawa wasielewane japo hili halikuua urafiki wao. Suluhisho la mgogoro huu halijaonyeshwa. Hata hivyo Gonza anaamua kutafuta pesa ili aende huko peke yake.
-      Nyundo na wazazi wake. Nyundo hakuwaheshimu wazee wake, aliwatukana na kuwadharau, mwisho anajiingiza katika ujambazi.
Migogoro ya nafsi
-      Chioko anapatwa na mgogoro wa nafsi juu ya suala la kwenda Zambia. Kwa asilimia kubwa haafiki mpango huo.
-      Nelli naye anapatwa na mgogoro wa nafsi. Kila anapoomba kazi anaombwa rushwa ya ngono. Hataki kumsaliti Chioko, lakini pia, hataki kukosa kazi. Suluhisho la mgogoro huu ni Nelli kukataa kutoa rushwa ya ngono.
Migogoro ya kiuchumi
Jamii inayozungumziwa na mwandishi ina matabaka mawili, tabaka la wenye nacho na tabaka la wasionacho.
Tabaka la chini linafanya kila purukushani ili waweze kujikomboa. Kwa mfano Gonza anaamua kuliibia tabaa la juu. Anapigwa risasi na kupoteza maisha.
Migogoro ya kisiasa
Serikali imo katika mgogoro na wananchi wake. Serikali ikitumia mgambo wa jiji, inawatimua walalahoi wote na kuwapeleka katika vijiji vya ujamaa. Hata hivyo walalahoi hawakubali kuishi kijijini, wanarudi mjini na mgogoro unaendelea.

Msimamo

Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani anaamini wanachi wataondokana na lindi la umasikini endapo tu watafanya kazi kwa bidii huku serikali ikiwasaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazowarudisha nyuma.

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa, umasikini utaisha endapo watu watafanya kazi kwa bidii na serikali ikiwasaidia kufikia malengo yao.

Fani

Muundo

Mwandishi ametumia muundo wa urejeshi. Kwanza anatuonyesha maisha ya dhiki wanayoishi Chioko na Gonza walipokuwa Dar es Salaam, kisha baadaye anatukumbusha historia ya watu hawa, walikozaliwa na shule walizosoma. Anafanya hivyo pia, pale anapomuelezea Nyundo.
Pia, riwaya hii ina sura zipatazo tisa.

Mtindo

Msaniii ametumia:
-      Dayolojia
-      Monolojia
-      Nyimbo. Mfano katika ukurasa wa 23 mwandishi katumia wimbo wa KILINDWACHO.
-      Barua. Chuchu kutoka Zambia anamwandikia barua Gonza inayomtaka aende Zambia kwani huko kuna maisha mazuri.
Mandhari
Mwandishi ametumia jiji la Dar es Salaam na viunga vyake kama:
-      Manzese
-      Kariakoo
-      Posta
-      Tandika
-      Buguruni
Vilevile ametumia mandhari ya nyumbani, ofisini, barabarani, kijijini, baa na vichochoroni.

Wahusika

Chioko
-      Amemaliza darasa la saba na anatafuta kazi ya ofisini
-      Ni rafiki yake na Gonza
-      Ni mpenzi wake Nelli
-      Anawakilisha tabaka la vijana wasio na ajira
Gonza
-      Anaishi Manzese
-      Anaendesha maisha yake kwa kuuza karanga
-      Anaamua kuwa mwizi kutokana na ugumu wa maisha
Nelli
-      Ni mpenzi wake Chioko
-      Anakamatwa na kupelekwa katika kijiji cha Mapinduzi lakini anatoroka
-      Anawakilisha kundi la wasichana wasiokuwa na ajira
Wahusika wengine ni:
Nyundo, Mlinzi, Msukuma mkokotoni, Chuchu, Walevi, Meneja wa kiwanda cha mabomba.

Matumizi ya lugha

Tamathali za semi
-      Tashibiha. “Hata majengo yaliyokuwa yamesimama kama askari jela wa kikoloni.”
-      Tashihisi. “Alichukuliwa na usingizi harakaharaka…”
-      Sitiari. “Nelli ndiye waridi la moyo wangu…”
-      Tanakali sauti. “Myaaau! Myaaau! Myaaau!”
-      Takriri. “Kila kitu kilikuwa kimya! Kimya kushoto, kimya kulia…”
Misemo, nahau na methali
“Mtu aliyelala mbavu za mbwa.”
“Ukishindwa kupata kware mawindoni rudi na bundi.”
“Usipochomwa mwiba hujui kiatu.”
Taswira na picha
Mwandishi ametumia taswira za wadudu kama nzi, kunguni na  viroboto kuashiria makazi duni ya watu huko Manzese.

Kufaulu kwa mwandishi

-      Mwandishi amefaulu kuonyesha chanzo na matatizo yanayowakumba watu wa tabaka la chini.
-      Pia, amefaulu kutumia lugha inayoeleweka vizuri na iliyojazwa tamathali nyingi za semi.

Kutofaulu kwa mwandishi

Jina la kitabu Usiku utakapokwisha linavyosadifu yaliyomo ndani

-      Mwandishi hajaonyesha suluhisho la maisha ya makabwela, mpaka mwisho wa kitabu watu hawa wameendelea kuishi maisha duni.
Jina la kitabu Usiku utakapokwisha linavyosadifu yaliyomo ndani

Usiku ni ishara ya jambo lolote baya, hivyo, mambo mabaya kama umasikini, ukosefu wa ajira,  rushwa, tatizo la usafiri n.k, ndiyo usiku wenyewe. Mwandishi anasema usiku utakapokwisha, akimaanisha matatizo yatakapokwisha.


Gonza na Chioko wanaishi katika matatizo makubwa,hivyo, usiku kwao bado haujakwisha.

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Hotuba