Mawazo Makuu ya Kahigi Katika Makala ya Structural and Cohesion Dimensions of Style
Soma makala ya Kahigi (1997) ya Structural and Cohesion Dimension of Style: Consideration of Some Text in Maw (1974) na uelezee mawazo makuu ya mwandishi katika kurasa zisizozidi tatu.
Profesa
Kulikoyela Kahigi ni mwanaisimu, mwanasiasa na mshairi maarufu. Mtaalamu huyu,
amefanya tafiti nyingi katika isimu ya kibantu, mitindo katika isimu na leksikografia.
Makala ya Kahigi, ni matokeo ya kitabu cha Maw (1974). Makala ya Structural and Cohesion Dimension of Style:
Consideration of Some Text in Maw, imegawanyika katika maeneo makuu matano
ambayo ni, utangulizi, mtazamo wa ushikamani, ushikamani katika matini
mbalimbali za kiswahili, vipengele vya kimuundo na vipengele vya kiushikamani
na mwisho kamaliza kwa kutoa hitimisho. Kama inavyoelezwa katika kamusi ya TUKI
(2004), wazo ni jambo ambalo mtu analifikiri. Hivyo basi mawazo makuu ya
mwandishi katika makala hii yanajadiliwa katika aya zifuatazo.
Wazo kuu la kwanza la mwandishi ni, mtazamo
wa ushikamani na uhusiano wa kiushikamani. Mwandishi anaeleza kuwa, ushikamani
huhusiana na kufanya matini iunganishwe pamoja kwa kutumia nyenzo kama,
urejeleo, ubadala, udondoshaji na uunganishaji. Taaluma hii ilianzishwa mnamo
karne ya 16 na 17 na wanaisimu wa kipindi hicho hususani H&H. Katika mtazamo
huu, mwandishi anajadili dhana ya uhusiano wa kiushikamani kuwa “ni uhusiano wa
kimaana kati ya vipashio au vijenzi katika matini na baadhi ya vijenzi
vinginevyo vya msingi katika kufasili matini” (H & H uk.8). Uhusiano huu
unafafanuliwa zaidi kwa mfano ufuatao.
“Kwanza, mvulana humchagua msichana
amwonaye afaa kwa ndoa. Kisha huwaambia
wazee wake.”
Katika
mfano huo, neno kisha linarejelea kwanza, na kamwe haliwezi kueleweka mahali
hapo kama kusingekuwa na neno kwanza. Hivyo maneno hayo yanahusiana. Pia,
mwandishi anaeleza aina tano za uhusiano wa kiushikamani ambazo ni, urejeleo, ubadala,
udondoshaji, uunganishaji na ushikamani wa kileksika. Pasipokutumia vigezo
hivyo, ni vigumu kuupata ushikamani.
Wazo jingine la mwandishi ni, ushikamani
katika matini mbalimbali za kiswahili. Wazo hili linajaribu kuangalia kama kuna
ushikamani wowote katika matini za kiswahili. Ili kusaidia uelewa, mambo ya
kuzingatia katika uchambuzi wa matini yanatajwa kuwa ni: idadi ya vijenzi vya
ushikamani, vipashio katika sentensi inavyofanya kazi kiushikamani, aina ya
ushikamani inayohusika katika kila ufungamanifu na umbali wa ushikamani. Katika
hoja hii, Kahigi anatumia kauli za kitafiti ambazo zinajumuisha uchunguzi juu
ya sifa bainifu za ushikamani wa kisarufi na kileksika na sentensi
zinazochukuliwa kama nduni za kielimu mitindo za kila matini. Kama
zinavyoelezwa hapa chini.
Utafiti wa kwanza umefanyika katika hoja
zilizoandikwa na matokeo yake ni haya: hoja hizi hujumuisha takriri, maneno ya
usawe na maneno vipashio ambayo hayawezi kuainishwa kwa urahisi. Mtoa hoja
huepuka kurudiarudia maneno bali huyachagua katika seti mbalimbali za kileksika.
Utafiti wa pili unazungumzia kifungu habari cha drama, hiki kinatoa sifa
zifuatazo: kuna ushikamani wa kiubadala kwa kiasi kikubwa, kuna udondoshaji kwa
kiasi kikubwa, maswali ya hapo kwa hapo, pia matini inaonekana kuwa na uwiano
wa juu zaidi wa vijenzi vya umbali na urefu wa kudumu. Utafiti mwingine
ulifanyika katika kifungu habari cha kisiasa, ushawishi wa mazungumzo na
masimulizi.
Mwandishi hakuishia kuwa na mawazo hayo
tu, bali wazo jingine tofauti na hayo yaliyopita linapatikana ambalo ni, uhusiano
uliopo kati ya matini andishi na sifa za ushikamani. Uhusiano ulipatikana kwa
kuangalia matini mbalimbali za kiswahili ambazo ni, Uhuru, Julai 26, 1969 (Usumbufu katika mchezo wa kandanda),
mkusanyiko wa matangazo kutoka Taifa
Tanzania, Aprili 13, 1968, Wasifu wa
Siti Binti Saad, S. Robert, Kifungu cha habari kilichosimuliwa na Yakubu wa
Tanga na makala nyingine nyingi zimechambuliwa na kuonesha uhusiano wa matini
andishi na sifa za ushikamani.
Kwa kuhitimisha, malengo ya makala hii ya
Profesa Kahigi ni mawili, lengo la kwanza ni kuongeza ushikamani katika
uchambuzi wa mtindo wa kiswahili kama ilivyooneshwa na Maw (1974), na lengo la
pili ni kuangalia kama kuna uhusiano wowote kati ya muundo na ushikamani.
Mawazo makuu yanayoonekana katika makala hii, yana mchango mkubwa sana katika
taaluma ya ushikamani.