Uhistoria Mpya Katika Diwani ya Chini ya Mwembe

Maembe Mawili


Swali

Historia huumba matini ya kisanaa tunayoyaona, kuyasikia na kuyasoma. Tumia nadharia ya uhistoria mpya kusawiri uhusiano uliopo kati ya historia ya maendeleo ya taifa la Tanzania na maudhui ya diwani ya Chini ya Mwembe (2017) ya Eric F. Ndumbaro na Gloria D. Gonsalves.

Jibu

Nadharia ya uhistoria mpya ni nadharia ambayo inaeleza uhusiano uliopo baina ya historia na fasihi. Inatambulika kwamba wahakiki wa uhistoria mpya wa Kimarekani ndio wanaotambulika kwa kuenea kwa mkabala wa uhistoria katika fasihi katika miaka ya 1980 na ile ya 1990. Wahakiki wa uhistoria mpya wao walisoma matini za kifasihi kama zao la kitu kinachotokana na mazingira ya kipindi mahususi cha kihistoria. Miongoni mwa majina makubwa ya wahakiki wa mkabala wa uhistoria mpya wa Marekani ni Stephen Greenblattt na Louis Montrose.

Wamitila (2008), anajadili kipengele kingine muhimu kinachoshughulikiwa na wanauhistoria mpya. Anadai kwamba kwa wanauhistoria mpya, matukio ya kihistoria siyo lazima yaonekane yote kwa wazi kabisa. Kuna matukio mengine yanaweza kujitokeza kwa njia ambayo si ya wazi sana, lakini bado tukaweza kubaini matukio halisi ya kihistoria yanayojadiliwa.

Hivyo basi kuna uhusiano wa karibu sana kati ya fasihi na historia, hususani riwaya. Kukna mambo mengi yanayochangiwa kwa pamoja kati ya fasihi na historia. Mambo hayo ni pamoja na ubunaji, mahali, wakati, usimulizi, matukio halisi ya kihistoria na suala la ukadinaji katika kueleza utokeaji wa matukio au jambo fulani.

Maudhui ni jumla ya mawazo yote ya mwandishi katika kazi ya fasihi. Maudhui hujumuisha vipengele vifuatavyo: dhamira, ujumbe, migogoro, falsafa na mtazamo.

Diwani ya Chini ya Mwembe ni kusanyiko la mashairi tofauti yanayogusa maisha ya mwanadamu. Mashairi yaliyopo yanatambua hisia mbalimbali kama mapenzi, furaha, Amani na wasiwasi, uchungu na hasira. Maisha bila hisia ni kifo. Diwani hii inahamasisha watu watafute mti wa mwembe utakaosaidia kutafakari hisia za maisha.

Uhusiano uliopo kati ya historia na maendeleo ya taifa la Tanzania na madhui ya diwani ya Chini ya Mwembe yanajadiliwa:

Kwanza tunaona mawazo ya kimvuvumko na mwamko mpya kuhusu historia. Mawazo haya yanaonekana katika shairi la UJUZI WA FUNDI NGUO. Mshairi anakosoa tabia mbaya ya fundi nguo. Anasema,

“Umaarufu unao, ila punguza uongo,

Utakuja adhirika, mbele ya kadamnasi,

Toa miadi ya kweli, epuka msongamano,

Fundi huyu fundi gani? Kila nguo anashona.”

Ubeti huu unabeba malalamiko ya miaka mingi kuhusu mafundi. Mafundi wamekuwa si waaminifu kiasi cha kuharibu kazi. Upo uhusiano kati ya historia hiyo ya mafundi na maendeleo ya taifa. Fundi anaweza kufananishwa na kiongozi yeyote asiye muadilifu ambaye ameshindwa kuleta maendeleo katika jamii yake.

Dhamira inayopatikana katika shairi hili ni umuhimu wa kusema ukweli. Mshairi anamuonya fundi,

“Fundi acha longolongo, mara leo mara kesho,

Na kesho ikishafika, kauli kubadilisha,

Nenda urudi jioni, vimebaki vishikizo,

Sifa zako zatambaa, na kupita vizingiti.”

Ni vyema mafundi wakawa wakweli kwani wanayo nafasi ya kufanya mabadiliko na kubadili historia.

Jambo jingine ni kujirudia kwa historia. Katika shairi la SAFARI YA KANAANI, mshairi anatamani kuona historia ikijirudia. Katika ubeti wa pili mshairi anasema,

“Upo wapi ewe Joshua, Joshua wake Tanzania,

Ewe Rabuka, twasikia twatii anayotwambia.”

Mshairi anatamani historia ya wana wa Israel ijirudie ili kuleta ukombozi katika nchi ya Tanzania. Anatamani kumuona Joshua akirudi tena.

Dhamira inayopatikana katika shairi hili ni hamu ya mabadiliko. Wtu wamechoshwa na hali ya sasa, wanatamani kuona mabadiliko yakipatikana ili kuweza kuleta maendeleo, mshairi anasema,

“Ni nchi yetu ya ahadi, tangia enzi za Farao,

Kanaani hatuna budi, hilo ni letu kimbilio.”

Kauli ya mshairi imebeba matarajio ya Watanzania wengi ambao wanatamani kuona mabadiliko yakitokea. Watanzania wamechoka kuonewa na kufanyiwa mambo yote yasiyofaa. Hivyo basi, shairi hili linabeba malalamiko ya miaka mingi. Tangu enzi za ukoloni Watanzania wanatamani kuona mabadiliko na mpaka sasa hawajayaona.

Pia, mshairi anapinga maneno ya wahenga ili kusaidia kuleta maendeleo ya taifa. Katika shairi la YA WAHENGA YAKAPIMWE. Mshairi anasema,

“Bado nipo fikirani, wema hawana maisha!

Mantiki yake nini? Wabaya wana maisha?

Ni msemo wa zamani, wengi ulitupotosha.”

Mshairi anapinga msemo usemao wema hawana maisha ambao umesemwa na wahenga miaka mingi iliyopita. Mshairi anaona kuwa, kuendelea kukubaliana na msemo huu ni kuruhusu maovu na ubaya. Vitu hivi vikizidi, maendeleo ya jamii hukosekana.

Ujumbe unaopatikana katika shairi hili ni, siyo kila kilichosemwa na wahenga ni sahihi, bali zipo kauli zao zenye utata na zisipotumiwa vizuri zinaweza kuharibu. Mshairi anasema,

“Sio yote walosema, yamejaa ufaafu,

Hili napinga mapema, tena pasipo kashifu,

Fikirani nimekwama, natema kwa utiifu.”

Hivyo basi, katika jamii, watu wasiache kutenda wema kwa madai kuwa wema hawadumu. Wema ni chanzo cha maendeleo na wema ndiyo msingi wa ubinadamu.

Vile vile tunaona nafasi ya historia katika jamii. Katika shairi la AMANI mshairi anasema,

“Amani kuichezea,

Utakuja ijuita,

Hakika nakuambia,

Wengine watamania.”

Mshairi anaonesha umuhimu wa Amani ambayo Tanzania imeendelea kuwa nayo. Katika historia, kwa miaka mingi Tanzania inajulikana kama kisiwa cha Amani. Hivyo, chondechonde tusithubutu kuichezea Amani yetu.

Ujumbe unaopatikana katika shairi hili ni, Amani ni kitu muhimu na kinapopotea, athari kubwa hujitokeza. Mshairi anasema,

“Amani kuipoteza,

Hakika nawaapiza,

Tutaishi kwenye kiza,

Kama fuko mashimoni.”

Mshairi anaonesha umuhimu wa historia yetu ya Amani ili kuleta maendeleo ya taifa la Tanzania. Ni ukweli usiopingika kuwa, bila Amani hatuwezi kuwa na maendeleo.

Pia, tunaona nafasi ya mwanadamu katika kuibadili historia yake. Katika shairi la MWALIMU WA UBUNIFU, mshairi anampongeza mwalimu ambaye amembadilisha kutoka asiyejua mpaka anayejua. Mshairi anasema,

“Mwalimu wa ubunifu, fanaka nakuombea,

Kamwe sitaki kufuru, mazuri kukyachimbia,

Nitasema kwa uhuru, mambo ulonitendea,

Mwalimu wangu hodari, kunifanya mbunifu.”

Ni dhahiri kuwa, mshairi hakuwa mbunifu ila amepata ubunifu huo kutoka kwa mwalimu wa ubunifu.

Mshairi ana mtazamo wa kimapinduzi. Anaamini kuwa, mwanadamu ni chanzo cha mabadiliko kama alivyo mwalimu wa ubunifu. Anasema,

“Bidii kipaji chake, uzembe ugonjwa wake,

Uvivu ni mwiko kwake, kujituma hobi yake,

Uchoyo ni sumu yake, hupenda aeleweke,

Mwalimu hongera sana, vipaji umeibua.”

Mshairi anabainisha kuwa, bidi na kujituma ndiyo vyanzo vya maendeleo. Mshairia anawapongeza walimu ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuelimisha.

Hoja nyingine ni historiografia ya kitaifa au ya kimapinduzi. Katika shairi la WAMENIACHIA UHAI, mshairi analaani vikali ukoloni mamboleo ambao umefunga furs azote na kutuachia uhai pekee. Mshairi anasema,

“Wamenifunga miguu, ningekuja kukuona,

Siwezi kukujongea.

Wameniziba mdomo, ningesema ukweli,

Nashindwa nawe kuongea.

Wamenifunga mikono, ningekushika mkono,

Siwezi kushikilia.

Wamenifunga machoni, kweli ningekutazama,

Siwezi kuangalia.

Lakini nawashukuru, uhai wameniachia,

Kwani bado napumua.

Japo hewa si safi, lakini nawashukuru,

Hawajaniziba pua.”

Ni kweli kwamba mataifa ya Afrika hayana uhuru wa kufanya lolote isipikuwa kutii amri za mabeberu.

Ujumbe unaopatikana katika shairi hili ni mataifa ya Afrika yaungane pamoja kupambana na ukoloni mamboleo. Ukoloni mamboleo unaweza kuondolewa kwa kuwa na viongozi wazuri, teknolojia na uchumi wa kujitegemea.

Kwa kuhitimisha, historia huumba matini ya kisanaa. Nadharia ya uhistoria mpya imesawiri uhusiano uliopo kati ya historia na maendeleo ya taifa la Tanzania ikiwa ni pamoja na kutaja vipengele vya maudhui kama: dhamira, ujumbe na msimamo. Hivyo basi, historia inayo nafasi yake katika kazi za fasihi na hakuna sababu ya kuipuuza.

Marejeo

Mushengyezi, A. (2003). Twentieth Century Literary Theory. Kampala: MukonoPublishing Company Ltd.

Ndumbaro, E na Gonsalves G. (2017) Chini ya Mwembe.

Njogu, K na R. Chimera (1999). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: The Jommo Kenyatta Foundation.

Senkoro, F.E.M.K. (1987). Fasihi na Jamii. Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.

Unahitaji Kufanyiwa Swali Lako? Gusa Hapa Kuwasiliana Nami.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne