Taaluma ya Semiotiki Katika Mazingira Halisi
Semiotiki imefasiliwa na
wataalamu mbalimbali, na hizi ni maana zilizotolewa na baadhi ya wataalamu hao.
Kwa kuanza na mtaalamu Massamba (2004), yeye anasema kuwa, semiotiki ni taaluma
ya kisayansi inayojishughulisha na uchunguzi na uchanganuzi wa mifumo ya ishara
mbalimbali ikiwa inazingatia zaidi uhusiano baina ya kiwakilishi na kitajwa.
Pia mtaalamu Ferdinand
de Saussure kama alivyonukuliwa na Morris (1971) amefasili semiotiki ni
uhusiano kati ya alama na kitu, jambo au hali ya kitu inavyowakilishwa,
akaendelea alama ni kiashiria na kitu ni kiashiriwa. Hakuna uhusiano wa moja
kwa moja kati ya kiashiria na kiashiriwa.
Charles (1934), alishughulikia dhana ya semiotiki kwa kuunda tanzu tatu
ambazo ni sintaksia, Pragmatiki na semantiki.Sintaksia ni taaluma ya uhusiano
kati ya ishara na vitu/ vielezo jinsi vinavyotumika, pragmatiki ni taaluma ya
uhusiano kati ya mfumo wa ishara na mtumiaji wake na semantiki ni taaluma ya
uhusiano kati ya maana na ishara. Hivyo basi semiotiki ni taaluma
inayoshughulikia maana za ishara/ taswira.
Semiotiki hushughulikia neno kama kiwakilishi (utajo) cha kile kitajwa pia
hushughulikia maana ya msingi. Hivyo semiotiki inaona maana inapatikana kupitia
taswira. Yaani kila taswira lazima inakuwa na maana inayowakilisha. Kwa mfano
rangi nyekundu duniani inaashiria upendo hivyo maana ya upendo iliyojitokeza
imetokana na taswira ya rangi hiyo. Hivyo katika taaluma hii maana zote za maneno
zimefumbatwa katika alama. Ni dhahiri kwamba ingawa semiotiki na
semantiki hushughukia maana, semiotiki kwa kiasi kikubwa hujihusisha na alama
za kitaswira na vielezo kwa kiasi kidogo wakati semantiki huchunguza
maana katika mfumo wa ishara wa lugha inayozungumzwa na binadamu.
Mtaalamu Nazarova (1996), anafasili, semiotiki ni nadharia inayohusu mfumo
wa alama katika mawasiliano ya lugha.
Kwa ujumla, semiotiki ni taaluma inayojishughulisha na uchunguzi wa ishara
na alama pamoja na uhusiano kati ya alama na kitu husika.
Hivyo basi Semantiki inatofautiana na semiotiki kwani semantiki
inashughulikia alama za lugha yaani kila lugha huwa na alama zinazoashiria kitu
fulani wakati alama za semiotiki hazihusu lugha yaani huwa ni maana za
mawasiliano, mfano ishara za mawingu, wanyama kama bundi ishara ya uchawi.
Taaluma ya semiotiki inaweza kuelezwa zaidi kwa kuangalia aina tatu za
ishara;
Ishara za usababisho/ asili/ alama halisi. Hizi hueleza kufungamana kwa
kiusababisho kati ya alama au ishara na kile kinachoashiriwa. Maana yake ni
kwamba, jambo moja husababisha jambo la pili. Mfano, moshi – alama ya moto na
mawingu ni alama ya mvua. Vilevile sura yenye makunyanzi huweza kuwa ishara ya
mtu mwenye hasira. Kwani si kawaida kwa mtu mwenye furaha au anayecheka kuwa na
makunyanzi usoni. Pia jogoo anapomkimbiza tetea ni ishara kwamba anataka
kumpanda.
Mfano mwingine wa ishara za usababisho ni mbwa anapobweka sana mawindoni ni
ishara kwamba kuna mnyama karibu. Pia nyayo (alama za miguu) ni ishara kwamba
kuna mtu kapita, kama nyayo hizo zimefifia huashiria kwamba mtu huyo kapita
muda mrefu na kama hazijafifia ni ishara kwamba mtu kapita muda mfupi. Vilevile
mionekano ya sura ya mwanadamu ni ishara za usababisho wa hisia, mfano, mtu
anapotoa machozi huashiria kuwa ana majonzi, japo kwa wakati mwingine huwa ni
kiashiria cha furaha. Tumbo kubwa kupita kiasi kwa mwanamke ni ishara kwamba
mwanamke huyo ni mjamzito. Sauti nene kwa mvulana ni ishara kuwa mvulana huyo
amebalehe na sasa anaingia katika kundi la watu wazima. Vivyo hivyo, msichana
anapokuwa na sauti nyembamba na nyororo huashiria kwamba, msichana huyo si
mtoto tena na huenda amekwisha vunja ungo. Hivyo ishara za usababisho ni alama
ambazo maana yake huwa ni ileile kwa yeyote anayetazama alama hiyo.
Ishara za ufananisho. Katika ishara hizi, huangaliwa kufanana kwa kipicha
kati ya ishara na kinachoashiriwa. Kwa mfano picha ya mtu ke/me katika milango
ya vyoo. Au mchoro wa kitu na kitu chenyewe. Mfano ramani ya nyumba ni
ufananisho wa nyumba yenyewe, pia picha ya mtu ni ufananisho wa mtu fulani.
Mfano mwingine wa ishara za ufananisho ni ule unaoonesha picha ya sigara
ikiwa imekatwa katikati, hii ni ishara ya ufananisho inayotoa amri juu ya zuio
la uvutaji wa sigara katika eneo hilo.
Mfano mwingine wa ufananisho ni ule wa michoro ya barabarani, michoro hiyo
au alama hizo za barabarani huweza kuwakilisha barabara finyu, kona kali, kituo
cha mabasi na amri ya kusimama. Pia bendera huwakilisha chama, nchi, au alama
ya kikundi fulani. Pia katika mahusiano rangi nyekundu huweza kuwakilisha
ishara ya upendo. Mfano mwingine wa ufananisho ni picha ya injini ya kompyuta,
pia alama V katika mkono wa mwanajeshi huonesha anacheo cha sajenti. Pamoja na
mifano hiyo, kuna mifano mipya ambayo imeweza kuibuka katika zama hizi kama
matokeo ya sayansi na teknolojia. Mfano katika mitandao ya kijamii, kama
Instagram, Facebook, WatsApp, Telegram na mingine mingi, kumekuwa na matumizi
ya picha ndogo (emoj) ambazo huambatana na maneno au kusimama peke yake. Picha
hizi ndogo hubeba hisia fulani kwani zimebeba michoro ya vichwa vya watu, zipo
zinazocheka na hutumiwa na mtu anayetaka kuonesha kwamba kafurahishwa na jambo
fulani. Lakini pia zipo zinazolia, hizi huashiria kwamba mwandishi wa ujumbe
ule hakuwa na furaha au mwenye huzuni. Mbali na hayo picha hizo, huweza
kuonesha ramani za nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania. Hivyo hapana shaka mtumiaji
wa mitandao hiyo ya kijamii anaweza akatumia picha hizo ndogo na akaeleweka
hata bila kutumia maneno kabisa.
Ishara za unasibu. Katika ishara hizi hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati
ya ishara na kitu kinachoashiriwa, lakini uelewekaji wake hutokana na mazoea
tu. Hii ni kusema. Uhusiano huo ni wa kiada tu na wala haufuati kanuni yoyote.
Alama hizo ni maneno ya lugha ambayo kimsingi yaweza kuandikwa au kutamkwa tu.
Mfano jina la mtu, ieleweke kwamba ishara hizi zipo katika lugha kwa kiasi
kikubwa ingawa katika ufananisho na usababisho zipo pia. Mfano mwingine wa
ishara za unasibu ni neno kiti, neno hili halina uhusiano wa moja kwa moja na
kiti halisi katika ulimwengu halisi. Mahusiano haya kati ya alama ya kiisimu,
dhana, kitu halisi yaliwahi kuelezwa na wana isimu wa semantiki ambao ni
Richard na Ogden (1968) kwa mchoro uliofahamika kama pembetatu ya maana kama
hivi;
D = dhana, A = alama ya kiisimu na K = kitu halisi
Mchoro huu unaonesha kuwa, kwa msitari usioungana na mistari mingine, kuna
uhusiano nasibu zaidi kati ya alama ya kiisimu na kitu halisi. Aidha kuna
uhusiano dhahiri zaidi kati ya alama ya kiisimu na dhana iliyoakilini
halikadhalika na kitu katika ulimwengu halisi.
Hivyo basi semiotiki kwa jina lingine inajulikana kama semiolojia, ambayo
inajihusisha na ishara pamoja na alama. Iliyotolewa maana na mmoja kati ya
waasisi wa semiotiki, Ferdinand de Sassure. Japo neno semiotiki lilianza
kutumika mnamo karne ya kumi na saba na mwana falsafa wa kiingereza John Locke.
Lakini wazo la semiotiki kama somo lilitokea katika karne ya mwisho ya kumi na
tisa na mwanzoni mwa karne ya ishirini kwa kazi huru ya Ferdnand de Sassure na
mwanafalsafa wa kimarekani Charles Sanders. Kwa hakika, aina hizi tatu za
ishara zinafanana na kuingiliana kwa kiasi fulani, hivyo umakini mkubwa
unahitajika katika kuzielewa.
Marejeo;
Massamba P. B. D (2004) Kamusi ya
Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Morris, Charles W. (1971), Writings
on the general theory of signs, The Hague: Mouton.
Peirce, Charles S (1934), Collected
papers: Volume V. Pragmatism and pragmaticism. Cambridge, MA, USA: Harvard
University Press.
Leech, G. (1981) semantics. The
meaning of meaning. (2nd Edn) Harmondsworth: Penguin Books.
Johansen, Jorgen Dines (1988). “The
Distiction between Icon, Index, and Symbol in the study of Literature,”
Semiotic Theory and Practice, Berlin: Walter de Gruyter.