Safari ya Kuusaka Mwezi | Sehemu ya Kwanza

Picha ya Mwezi

Naitwa Nkenye, nina umri wa miaka Tisa, leo nataka niwasimulie tukio lililotokea katika Nchi yetu ya Rahaja miezi miwili tu iliyopita. Tega sikio…

Ilikuwa usiku wa manane niliposikia kelele za watu nje ya nyumba yetu ya nyasi. Niliamka haraka kisha nami nikaelekea nje ili nikapate kujua kilichokuwa kikiendelea. Huko nje nilikuta watu wote wamesimama wakipiga kelele huku wakiwa wameangalia juu.

“Mwizi! Mwizi! Mwizi!”

Nami nilitazama juu ili nione kilichowaliza, Loooh! Nilikiona kijitu kichafu kimevaa koti jeusi toka sayari ya mbali kikiwa kimeubeba mwezi wetu kikikimbia nao kuelekea mbali huko juu angani. Kabla sijashusha uso wangu chini giza kuu liliingia hata hatukuweza kuonana.

Vijana wa usalama wa nchi, waliwasha mienge ya moto hapo tuliweza kuonana tena, wote tulikuwa na masikitiko makubwa. Nilimuona mama na kaka yangu Mowasha wakilia kwa huzuni.

Watu wote walitamani kusikia chochote kutoka kwa mkuu wa usalama wa nchi ambaye alikuwepo katika eneo hilo, baada ya matarajio mengi mkuu wa usalama wa nchi alikohoa kisha akazungumza,

“Ndugu zangu mwezi umeibwa na kijitu toka sayari ya mbali, ni lazima mwezi wetu upatikane kwani bila mwezi kutakuwa na giza kali sana ambalo litarahisisha wezi kufanya kazi zao. Vilevile, Dunia bila mwezi, siku huisha kwa masaa sita tu, hivyo siku zetu za kuishi zitapungua… lazima mwezi upatikane tuishi miaka mingi!”

“Ndioooo!” Sote tuliitika kwa nidhamu ya hali ya juu.

“Nawaombeni kesho tujitokeze mbele ya kibaraza cha mfalme saa mbili kamili asubuhi, ili tuweze kuwajulisheni njia tutakayotumia kuurejesha tena mwezi wetu.” Mkuu wa usalama wa nchi alimaliza kuongea kisha wote tukasambaa kuelekea majumbani kumalizia usingizi.

Mimi niliongozana na mama, kaka yangu Mowasha na baba yangu shujaa aliyeitwa Mako. Hatukuzungumza lolote njiani, tulihuzunishwa sana na tukio lile la kuibwa mwezi. Nilihuzunika zaidi nilipofikiria kuwa hata siku zetu za kuishi zingepungua!

XX                              XX                              XX                              XX                                
Saa mbili asubuhi Wananchi wote tulikusanyika kwenye kibaraza cha mfalme kama ilivyoamriwa. Mfalme akiwa amevalia joho jeupe alisimama akasema,

            “Leo viongozi hatujalala, matatizo yaliyotokea jana yalitufanya tukeshe tukijadili mwafaka wa Dunia bila mwezi. Kijitu kilichouiba mwezi kinatoka Dunia nyingine iitwayo Vumu iliyo katika mfumo wa jua lingine. Inasemekana katika sayari yao hiyo, mwezi wao ulizimika ghafla wakati watoto waliotumwa kwenda kuusafisha walipozidisha kiasi cha mafuta. Vijitu hivi vinamaarifa mengi sana lakini havijui kitu katika elimu ya kuukarabati mwezi, hivyo suluhisho lao lilikuwa kuiba mwezi mwingine. Sasa basi anatakiwa atumwe mtu kwenda katika sayari ya Vumu kuurejesha mwezi wetu.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie