Ubora na Udhaifu wa Uainishaji wa Ngeli za Nomino Kimofolojia

UAINISHAJI WA NGELI ZA NOMINO KIMOFOLOJIA, UBORA NA UDHAIFU

Mgullu (1999) anafasili nomino kuwa ni maneno ambayo hutaja vitu. Anaendelea kusema, “kwa hiyo nomino hutaja majina ya watu, vitu, mahali, vyeo, dhana na hata tendo. Ndiyo maana wanaisimu wengine wanaziita nomino majina.” Kwa upande wa dhana ya ngeli, wataalamu mbalimbali wameweza kuifafanua kama ifuatavyo;

Kapinga (1983) anasema neno ngeli limetoka katika lugha ya kihaya likiwa na maana ya kitu au vitu. Naye Mgullu (1999) anasema istilahi ngeli imechukuliwa kutoka lugha ya kihaya (Tanzania). Katika lugha ya kihaya, neno ‘ngeli’ lina maana ya aina ya kitu. Anaendelea kusema kwa kuinukuu kamusi ya Kiswahili sanifu (1981) kuwa ngeli ni utaratibu wa taaluma ya sarufi ya lugha katika kupanga aina za majina (nomino). TUKI (1990) wanasema, ngeli za nomino ni kundi moja la majina yaliyo na upatanisho wa kisarufi unaofanana na viambishi vya umoja na wingi vinavyofana. Naye Massamba na wenzake (2012) wanasema ngeli ni mgawanyiko wa aina mbalimbali za nomino katika mtazamo wa kisarufi katika fikra ya viashirio vya nomino katika aina nyingine za maneno zinazo ambatana nazo. Kwa ujumla ngeli ni aina au namna ya kuweka au kupanga au kuweka majina katika makundi yanayofanana au yanayowiana. Aidha uainishaji wa ngeli za nomino ni utaratibu au mchakato wa kupanga au kupachika aina za majina katika makundi kwa kuzingatia kuwiana au kufanana kisifa.

Kigezo cha kimofolojia ni miongoni mwa vigezo vitumikavyo katika uainishaji wa ngeli za nomino. Kigezo hiki cha kimofolojia ndicho kikongwe kabisa katika uainishaji wa ngeli na kimekitwa katika misingi mikuu miwili. Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali akiwamo Massamba na wenzake (2012) na kapinga (1983) kwa kuwanukuu au kuwarejelea waasisi wa kigezo hiki cha kimofolojia, Wilhem Bleek (1862) na Carl Meinhof wanabainisha msingi wa kwanza ambao ni wa kutumia viambishi vya nomino. Katika msingi huu, jumla ya ngeli 18 kama
zinavyoonekana chini zilibainishwa;

NAMBA
VIAMBISHI NGELI
                                 MIFANO
1
Mu-/Mw-/M
Muuguzi, Mwalimu, Mtoto
2
Wa-
Wauguzi, Waalimu, Watoto
3
Mu-/M-
Mungu, Mti
4
Mi-
Miungu, Miti
5
Ji-/Ø
Jiwe, Panga
6
Ma-
Mawe, mapanga
7
Ki-
Kiti, Kiatu, Kikombe, Kiongozi
8
Vi-
Viti, Viatu, Vikombe, Viongozi
9
N-
Nyumba, Nyama, Nyanya
10
N-
Nyumba, Nyama, Nyanya
11
(l) u-**
Lubao/ ubao
12
M-
Mbao
13
Ka**
Katoto
14
U-
Ugonjwa, Uchungu
15
Ku-
Kucheza, Kuimba, kulima
16
Pa-
Pahali, Pale
17
Ku-
(Kwahala*), huku, kule
18
Mu-
(Mwahala*), humu, mule

Viambishi vilivyowekewa nyota mbili ( **  ) zinatokana na maneno yenye athari za kibantu nab ado hayajakubalika moja kwa moja katika Kiswahili sanifu, ingawa baadhi ya watu wanayatumia. Maneno yaliyowekewa nyota moja ( ) yanatokana na lahaja za Kiswahili lakini pia hayatumiki sana katika Kiswahili sanifu.

Msingi wa pili katika kigezo hiki cha kimofolojia ni wa jozi ya viambishi vya umoja na wingi ambao ulianzishwa na Ashton mwaka 1944. Katika msingi huu, ngeli zifuatazo zimebainishwa ambazo Ashton aliziweka katika namba za kirumi.

NAMBA
VIAMBISHI NGELI
                            MIFANO
I
Mu-/ Mw-/ M- Wa
-Muuguzi, mwalimu, mtoto
-Watoto, wauguzi
II
M- Mi
-Muundo
-Miundo
III
Ji/Ø- Ma-
-Jiwe
-Mawe
IV
Ki- Vi-
-kiongozi, kiti
-viongozi, viti
V
N- N-
-Nyama, nyumba
VI
U- N-
-uzi, ufa
-nyuzi, nyufa
VII
Ka**- Tu**-
-katoto
-tutoto
VIII
U-Ma
-Ugonjwa
-Magonjwa
IX
Ku-Ku
-kucheza, kuimba
X
Pa- Pa
-Pahali
XI
Ku- Ku
-kwahala*, kule
XII
Mu-Mu
-(mwahala*), mule

(**- athari za kibantu, *- kutoka lahaja za kiswahili)

Kigezo hiki cha kimofolojia cha uainishaji wa ngeli za nomino za Kiswahili kina ubora ufuatao;

Huwawezesha wanafunzi wa lugha ya Kiswahili kuzielewa nomino au kuzifahamu nomino pamoja na maumbo yake ya umoja na wingi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, kigezo hiki kimekitwa katika misingi ambayo huzihusu nomino moja kwa moja. Mfano; kwa msingi wa kwanza ambao hutumia viambishi vya nomino moja kwa moja mtu anayejifunza lugha ya Kiswahili hususani wanafunzi wa kigeni huweza kuzifahamu nomino za Kiswahili. Mfano ngeli ya kwanza humuwezesha mwanafunzi kuweza kuzitambua nomino kwa haraka anaporejelea kwenye ngeli hiyo. “Mu-/Mw-/M-“.

Mfano; - mwananchi- Mw
-          Mwana- Mw
-          Mtoto- M
-          Muumini- Mu
-          Muuguzi- Mu

Hivyo, anapoona nomino hizi, haraka huweza kugundua kuwa hizi ni nomino za Kiswahili kwa kuangalia tu kiambishi cha nomino husika. Pia katika msingi wa pili ambao huzingatia vambishi vya umoja na wingi katika nomino, humuwezesha mtu anayejifunza lugha kugundua wingi au umoja wa nomino husika kwa urahisi. Mfano, nomino “mwana” mtu anapoiona hutambua kuwa hii inatoka ngeli ya Mu-/Mw-/M-Wa- na hapo anaweza kubaini pasipo na shaka wingi wa nomino hiyo mwana kuwa wana, anapozingatia na kurejelea kwenye ngeli hiyo (Mu-/Mw-/m-Wa-). Hivyo wanafunzi huweza kujifunza nomino za Kiswahili kwa urahisi.

Hudhihirisha/ huonesha uhusiano uliopo kati ya lugha ya Kiswahili na lugha za kibantu na hivyo kuthibitisha pasipo na mashaka kuwa Kiswahili ni kibantu. Huu ni ukweli usiotiliwa mashaka kabisa kutokana na ukweli kuwa nomino nyingi za kibantu zinaridhia pasipo na mashaka kabisa mtiririko wa ngeli hizo.

Mfano;

MSINGI WA KUTUMIA
NGELI YA
KIAMBISHI NGELI
MFANO

KISWAHILI
KISUKUMA
KIHEHE
1.VIAMBISHI VYA NOMINO
15
KU-
Kulima
Kucheka
Kulima
Kuseka
Kulima
Kuheka
2. JOZI YA VIAMBISHI
VYA UMOJA NA WINGI
1× (a)
KU- KU-
Kulima
Kucheka
Kulima
Kuseka
Kulima
Kuheka

Pia kuna ngeli ambazo moja kwa moja ni za nomino za kibantu. Mfano ngeli ya 11 na 13 katika msingi wa kutumia viambishi vya nomino ambazo ni (l) na Ka, moja kwa moja inatokana na athari za kibantu, hivyo basi kuonesha uhusiano wa moja kwa moja na wa karibu kabisa  na usiotiliwa mashaka yoyote baina ya Kiswahili na lugha za kibantu na hivyo kuthibitisha kuwa Kiswahili ni kibantu.

Ubora mwingine wa kigezo hiki cha kimofolojia katika kuainisha ngeli za nomino ni kuwa, kigezo hiki ni kikongwe na ndicho cha kwanza ambacho kimekuwa ni msingi au chimbuko la vigezo vingine vya uainishaji wa ngeli za nomino za Kiswahili. Pia ndicho kigezo cha kwanza kuzipanga au kuziainisha nomino za Kiswahili katika makundi yake mbalimbali na hivyo kuwawezesha wanafunzi wa lugha ya Kiswahili na watu wote wanaofuatilia kwa ukaribu lugha hii adimu kuweza kubaini makundi ya nomino za Kiswahili.

Sanjari na ubora huo kama ulivyoweza kubainishwa hapo juu, kigezo hiki cha kimofolojia katika uainishajiwa ngeli za nomino za Kiswahili, una udhaifu au mapungufu yafuatayo;

Matumizi ya viambishi vinavyofanana katika baadhi ya ngeli. Katika kigezo hiki cha kimofolojia kuna matumizi ya viambishi vinavyofanana miongoni mwa baadhi ya ngeli hali ambayo huleta utata na ugumu katika kuzitofautisha  ngeli hizo. Mfano katika orodha ya ngeli 18 za msingi wa kutumia viambishi vya nomino, ngeli ya 9, 10, na 12 zote zina kiambishi ngeli ‘N’. Pia ngeli ya 11 na 13 ni ‘U’- ngeli ya 8 na 14 ni ‘Ma’- hali ambayo huleta utata katika kuzitofautisha na kuzishika akilini miongoni mwa wanafunzi.

Kutozingatia muundo wa sentensi, kigezo hiki cha kimofolojia hakizingatii kabisa muundo wa sentensi hali ambayo husababisha nomino zisizokuwa na maumbo maalumu ya umoja na wingi kukosa ngeli ambayo nomino hizo zinaweza kuwekwa. Mfano; uchafu, usafi, utajiri, maji na nomino zingine ni vigumu kuziweka katika ngeli yoyote kwa kuzingatia kigezo hiki cha kimofolojia kwani nomino hizo hazina umbo maalumu la umoja na wingi na hivyo kigezo kupwaya kabisa na kudhihirika pasipo na shaka kuwa ni dhaifu.

Kuingizwa kwa nomino za kibantu zisizo za Kiswahili sanifu; kigezo hiki cha kimofolojia katika misingi yote miwili yaani msingi wa kutumia viambishi vya nomino na ule wa kutumia jozi ya viambishi vya umoja na wingi umeingiza ngeli  ambazo ni za nomino za kibantu ambazo si za Kiswahili sanifu, hali ambayo ni sawa na kuichafua lugha ya Kiswahili kwa kuingiza nomino zisizokubalika. Mfano ngeli ya 11 katika zile 18, ambayo ni (l) u- ambapo kuna nomino kama lubao ambayo haipo kabisa katika Kiswahili sanifu. Pia ngeli ya VII katika msingi unaotumia jozi ya umoja na wingi ambayo ni ‘Ka-Tu-‘ mfano wa nomino ni katoto-tutoto. Nomino hizi zina athari ya kibantu na si za Kiswahili sanifu. (Rubanza,1996).

Kutozingatia hadhi ya nomino, uainishaji wa ngeli za nomino katika kigezo hiki cha kimofolojia, haujazingatia kabisa hadhi ya nomino zenyewe kwani nomino zenye tofautitofauti zinapachikwa katika kundi moja. Mfano katika ngeli ya Ki-Vi, kuna mchango wa nomino zisizo na hadhi sawa mfano;

Ki-
Vi-
-          Kiti
-          Kiongozi
-          Kikombe
-          Kijana
-          Viti
-          Viongozi
-          Vikombe
-          vijana

Nomino kiti, kiongozi, kikombe na kijana hazina hadhi sawa lakini zimechanganywa katika ngeli moja na hivyo kuonesha udhaifu mkubwa mno katika kigezo hiki cha kimofolojia. Hivyo kigezo cha upatanisho wa kisarufi ni bora katika hili (Kapinga, 1983).

Idadi kubwa ya ngeli. Huu nao pia ni udhaifu wa kigezo hiki cha kimofolojia. Katika msingi wa kutumia viambishi vya nomino, kuna ngeli 18 na katika msingi wa kutumia jozi za umoja na wingi kuna ngeli 12 ambazo bado ni nyingi na hivyo kuleta ugumu miongoni mwa wanafunzi katika kuzishika na kuzipambanua. Kutokana na hali hii wanafunzi wengi huona somo hili kuhusiana na ngeli za nomino kuwa ni gumu na hivyo kukata tamaa na ujifunzaji hata wa taaluma zingine za lugha hususani isimu ya lugha ya Kiswahili.

Hivyo kutokana na udhaifu mkubwa wa kigezo cha kimofolojia katika uainishaji wa ngeli za nomino, ndipo wataalamu wengine wakaibuka na kuleta vigezo vingine au misingi ya uainishaji wa ngeli za nomino za Kiswahili. Misingi hiyo ni pamoja na msingi wa kutumia viambishi vya upatanisho wa kisarufi ambao ni wa kigezo cha kisintaksia ulioasisiwa na Kapinga (1983) ambapo uainishaji ulizingatia muundo wa sentensi na kupatikana  ngeli 11 ambapo wataalamu wengine huziweka katika ngeli 9. Pia msingi mwingine ni ule unaotumia viambishi vya nomino na upatanisho wa kisarufi yaani unachanganya kigezo cha kisintaksia na kigezo cha kimofolojia ambapo uliasisiwa  na Kihore na wenzake (2007) ambapo walibainisha ngeli 18. Hata hivyo, kuna haja ya kuendelea kufanya utafiti zaidi juu ya  uainishaji wa ngeli na nomino za Kiswahili ili kupata uainishaji bora kabisa usiokuwa na mapungufu mengi.

MAREJEO
           
Ashton, E. O (1994). Swahili Grammar. London; Longmans
           
Kapinga, C. (1983). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam; TUKI

Kihore, Y.M. et al (2007). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA). Dar es Salaam; TUKI

Massamba, D.P.B. et al (2012). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA) Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam; TUKI.

Mgullu, R.S. (1999). Mtaala Wa Isimu, Fonetiki, Fonolojia Na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi; longhorn publishers.

Rubanza, Y. L (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es Salaam. Chuo kikuu huria cha Tanzania (OUT).

TUKI (1990). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam; TUKI

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne