Uhakiki wa Riwaya ya Joka la Mdimu

ganda la kitabu cha riwaya ya joka la mdimu

Mwandishi: Abdallah Saffari

Mhakiki: Mwalimu Makoba

Simulizi kwa ufupi

Joka la mdimu ni aina ya nyoka ambaye hukaa katika majani ya kijani. Kwa kuwa nyoka huyu hufanana na majani, ni ngumu sana kumtambua. Joka hili la mdimu linafananishwa na viongozi. Viongozi hawa wanafanana na sisi kwa kila kitu hivyo ni vigumu mno kutambua hatari yao ya uongozi mbaya, rushwa, mauaji na ulaghai.

Cheche anaumia akishiriki maonyesho ya sherehe za uhuru. Kwa sababu ya kukosekana kwa fedha za kigeni, inashindikana kumpeleka Uingereza kutibiwa, na japo serikali inawajibika kumtibia, haionekani kufanya hivyo wala kujali. Baba yake anavamia benki, anapata fedha na kufanikiwa kumpelekea Uingereza kutibiwa.

Maudhui

Dhamira

Hali ngumu ya maisha

Katika riwaya hii tunauona ugumu wa maisha. Mhusika Jinja Maloni anafanya kazi yoyote ilimradi mkono uende kinywani. Anafanya kazi ya kuchimba makaburi na kupakua vyoo.

Hali hii ngumu ya maisha inasababishwa na uongozi mbaya, viongozi wameshindwa kuzuia rushwa, mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira rasmi.

Rushwa

Bila rushwa hakuna huduma, mambo mbalimbali sasa hayafanyiki mpaka utoe chochote kitu.

Tino anatoa rushwa ili mkewe aweze kusafiri.

Cheche anahitaji kwenda kutibiwa uingereza, Dokta Mikwala anapewa rushwa ili aweze kuidhinisha kibali hicho.

Naye Brown Kwacha anatoa rushwa ili kuweza kujipatia kila anachohitaji.

Urasimu

Cheche anaumia katika sherehe za uhuru, lakini ananyimwa haki yake ya kwenda kutibiwa nje. Wahusika wanapiga chenga kila wanapofuatwa.

Mwisho Amani anaamua kutoa rushwa ili aweze kupata haki ya mwanae.

Kutowajibika

Brown Kwacha hawajibiki kwa umma kama kazi yake inavyotaka. Matokeo yake anaitumia ofisi hiyo kwa manufaa yake binafsi.

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Mwanamke amechorwa katika mambo mbalimbali, mazuri na mabaya kama inavyoezwa:

Mzazi na mlezi wa familia. Mwema mkewe Tino aliwalea viizuri sana watoto wake Cheche, Tabu na Subira pia alimpenda na kumtunza vyema mumewe.

Pia mke wa Brown Kwacha aliwalea vyema mabinti zake watatu kwa kiasi kikubwa peke yake bila msaada wa karibu wa mumewe.

Mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe. Katika riwaya tunaona namna mabaharia wanavyowatumia wanawake kwa lengo la kujifurahisha tu.

Pia, tunamuona Brown Kwacha akiwatumia wanawake kwa kujifurahisha.

Kiumbe duni. Mwanamke anaonekana duni asiyekuwa na mchango wowote. Brown Kwacha anamdharau mkewe na hamshirikishi kwa lolote.

Jasiri, upande mwingine mwanamke anaonekana mwenye ujasiri wa hali ya juu. Pamela anamkataa Brown Kwacha bila kujali fedha wala cheo chake.

Ujumbe

Viongozi wanasababisha hali ngumu ya maisha

Rushwa ni adui wa haki

Viongozi waache urasimu, watende haki kwa wote

Umasikini ni chanzo cha watu kujihusisha na matendo yasiyofaa kama vile uhalifu.

Migogoro

Jinja Maloni na  Vibaka

Jinja anaingia katika mgogoro na vijana wanaojaribu kumbaka mwanamke, anawapiga na kumuokoa mwanamke yule.

Mgogoro baina ya Tino na Kondakta na Utingo wa basi

Kondakta na Utingo wake waliona Tino anawachelewesha, walishuka ili waweze kumpiga, lakini walipoona amesimama imara, walirudi ndani ya basi lao.

Mgogoro kati ya vjana waliokuwa wakipigania matenga yaliyokuwa yakishushwa, vijana hawa walipigana bila kuamuliwa na mtu yeyote mwishowe walichoka na kutazamana kama majogoo yaliyokuwa yakitangaza vita.

Mgogoro kati ya katibu mkuu wa wizara ya mila na utamaduni na kijana waliopigana katika uzinduzi wa nyumba ya Brown Kwacha,walikuwa wakimpigania mwanamke aitwaye Esther,walipigana mpaka wakatumbukia katika bwawa la kuogelea.

Migogoro ya nafsi

Tino ana mgogoro wa nafsi, anawaza na kuwazua juu ya namna ya kupata fedha za kuwezesha kumpeleka mtoto wake, Cheche nje kutibiwa.

Mtazamo/msimamo

Mwandishi ana mtazamo wa kimapinduzi.

Mwandishi anaeleza bila kuficha kwamba, viongozi ndiyo chanzo cha matatizo mengi yanayotokea katika jamii.

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa matatizo makubwa yanayojitokeza katika jamii yanatokana na uongozi mbaya.

Fani

Mtindo

Mtindo wa monolojia au masimulizi.

Mtindo wa dayolojia au majibizano

Matumizi ya nafsi ya tatu kwa kiasi kikubwa.

Matumizi ya nyimbo

Muundo

Riwaya ya Joka la Mdimu ina jumla ya sura kumi ambazo amezipa majina ya wahusika, mahali na matukio yanayobeba kisa kizima cha hadithi katika sura husika.

Mwandishi ametumia muundo wa rukia kwani amekuwa akisimulia visa kwa kusimulia matukio mengine na kuyaacha kuelezea matukio mengine katika sura tofauti tofauti.

Wahusika

Amani

Ni dereva taksi

Ni kijana mchapakazi

Ana huruma, hekima na busara

Rafiki yake Tino

Alimsaidia Tino katika tukio la kuiba benki.

Brown Kwacha

Ni mkurugenzi wa idara ya fedha za kigeni

Ni malaya

Anahudumia watu ofisini kwa upendeleo hasa wanawake

Ni mpenda rushwa.

Anajihusisha na magendo na ujangili

Tino

Ni mvuta kwama

Ni baba wa watoto watatu, Cheche,Tabu na Subira.

Ni jasiri sana

Ni mchapa kazi na mwanamichezo.

Jinja Maloni

Ni mtu mkakamavu na asiye mwoga.

Hufanya kazi kama za kupakua vyoo na kuchimba makaburi

Ana upendo na moyo wa kujitoa hasa inapokuja suala la kuokoa mtu

Anapenda muziki.

Dakta Mikwala

Ni daktari bingwa wa mifupa

Ni mlevi

Ni mpenda rushwa/hongo

Shiraz Bhanj

Ni mfanyabiashara mkubwa.

Ni mwajiri wa Amani

Rafiki yake Brown Kwacha

Ni mtoa rushwa

Cheche

Ni mtoto wa kiume wa Tino

Alivunjika kiuno katika michezo ya  sherehe za uhuru

Ana tabia njema

Ni mcheshi, mdadisi na mwanamichezo

Alipendwa sana na watu.

Wahusika wengine ni: Zitto, Leila, Josephine, Pamela, na Mwema

Mandhari

Riwaya hii imetumia mandhari ya mjini. Matukio mengi yanafanyika mjini. Huko ndiko kuna rushwa, biashara ya ukahaba, maisha ya kubahatisha na visa vya kila namna. 

Matumizi ya lugha

Misemo

Asiye na bahati habahatishi

Tandu kwenda mbele na nyuma ndiyo hulka yake

Asiyezika hazikwi

Mmetupa jongoo na mtiwe

Methali

Asilolijua mtu ni usiku wa giza

Ukiona mwenzio ananyolewa tia maji

Mtaka waridi sharti avumilie miiba

Biashara haigombi

Matumizi ya lugha nyingine

Kiingereza

Mission to Seamen please

Hey man you will pay extra dollars

Kiarabu

Inna lillahi wa inna ilahi rajiunna!

Tamathali za semi

Tashbiha

Zepher 6 ile iliunguruma kama samba aliyeghadhibishwa (uk. 9)

Wote walikimbilia kule wakiminyana kufa au kupona kama kaa wanavyogombea mavi ya mvuvi(uk. 21)

Maduka makubwa yalichipua  mithili ya uyoga

Miguu yake ilikazana mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa

Tashihisi

Utumbo ulimlaumu

Mvua ikarindima kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu

Lakini hata fikra nazo zilikuwa kama zimempiga chenga

Sitiari

Sote kobe

Sarahange wetu mbogo kweli siku hizi

Mbinu nyingine za kisanaa

Onomatopea/tanakali sauti

Saa mezani iliendelea kugonga ” ta ta ta”

Akazungusha ufunguo wa gari lake na kutaka kuliwasha lakini ikatokea sauti kali fupi “ta nye nye”

Takriri

Funga ,shinda! Funga,shinda! Sauti za mashabiki zikarindima tena

Shinda! Shinda! Shinda! Kibanda kilitetemeka tena

Shetani! Oyee! Shetani! Oyee! Shetani chinja!

Popular posts from this blog

Colonial Administrative System | History Form Three

Ubora na Udhaifu wa Uainishaji wa Ngeli za Nomino Kimofolojia

SMS 20 za Vichekesho Zinazochekesha Sana