Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Mwanamke Amebeba Chungu

Swali

Kwa mifano dhahiri kutoka katika riwaya ya Harusi ya Dogoli ya Athumani Mauya na Vuta N’kuvute ya Shafi Adam Shafi, jadili dai kuwa, fasihi ni zao la jamii.

Jibu

Zipo maana nyingi za fasihi zilizotolewa na wataalamu mbalimbali. Ya kwanza ni ile inayosema, Fasihi ni kioo cha maisha. Kwa maana kwamba, mtu anaweza akajitazama, akaona taswira yake na akajirekebisha, (Nkwera, 1970).

Kwa ujumla, fasihi ni sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe wake kwa jamii.

Fasihi ni zao la jamii, hii ina maana kuwa, kazi zote za fasihi huandikwa kutoka katika jamii. Yaani fasihi huchota mambo fulani yaliyopo katika jamii ndipo ikaandikwa. Mifano dhahiri ya kauli hii, inajadiliwa kupitia riwaya mbili: Vuta N’kuvute yake Shafi Adam Shafi na Harusi ya Dogoli yake Athumani Mauya.

Fasihi ni zao la jamii kwani inapata dhamira zake katika jamii. Katika Vuta N’kuvute Mwandishi anajadili dhamira ya mapenzi ameiga mapenzi halisi yaliyo katika jamii yetu na kuyaweka katika kitabu. Tunamuona kijana Denge akimpenda msichana wa Kihindi Yasmini, hata hivyo mapenzi yao motomoto yanakwamishwa, kwanza, na kazi nyingi za Denge na pili, ukosefu wa pesa. Yasmini anampata mpenzi mwingine na mwingine tena aliyeitwa Shihab. Katika Harusi ya Dogoli, tunayaona mapenzi ya Dogoli na Kijakazi, mapenzi ambayo yalipelekea wawili hawa wafunge ndoa kabla mambo hayajaharibika. Katika jamii yetu suala la mapenzi limetawala. Mahusiano ya mke na mume yanayo mifano mingi pamoja na changamoto zake.

Fasihi ni zao la jamii kwani iandikwapo huwa na lengo la kuielimisha jamii. Katika Vuta N’kuvute, elimu inatolewa kuwa, watu waungane pamoja ili kuupata ukombozi wa kisiasa. Tunamuona Denge na wenzake wakiwa msitali wa mbele kupambana na wakoloni ili kuweza kuleta uhuru. Katika Harusi ya Dogoli, mafunzo yapo, mojawapo ya mafunzo ni yale ya kumfundisha mtoto wa kike juu ya kujiheshimu na kujitunza mpaka atakapompata mume. Tunamuona Dogoli akifundishwa namna ya kuwa safi na jinsi ya kufanya kazi.

Fasihi ni zao la jamii kwani huchota migogoro iliyopo katika jamii. Katika Vuta N’kuvute, tunaona migogoro ya wahusika. Yasmini ana mgogoro mkubwa na Bwana Raza, mwanamume mzee mwenye umri sawa na baba yake ambaye amelazimishwa kuolewa naye. Yasmini anapambana na anafanikiwa kutoroka na kuanza kuishi maisha mapya. Katika Harusi ya Dogoli, tunaona migogoro ya wahusika. Mama yake Dogoli ana mgogoro na watu wasiojulikana, wachawi waliomroga mwanae hata jogoo likawa halipandi mtungi, pia, kifo tata cha Dogoli. Mwisho anatuma watu nchi za mbali wakawatafute wachawi hao. Migogoro ya wahusika ni kawaida kutokea katika jamii halisi. Watu hugombana kila siku, mahakamani kesi zimejaa chanzo kikiwa migogoro mbalimbali.

Fasihi ni zao la jamii kwani hutumia wahusika wenye sifa zifananazo na wahusika wa kwenye jamii halisi. Katika Vuta N’kuvute tunawaona wahusika wenye kila aina za tabia. Yupo kijana Denge, huyu ni machachari katika kupambana na wakoloni. Yupo Yasmini, bingwa wa kukataa ndoa za lazima. Tunaye Mwajuma, mtoto wa mjini, mswahili haswaa na anayeujua mji. Katika Harusi ya Dogoli, tunaye Dogoli mwenyewe. Kijana mwenye bahati mbaya ya kukosa nguvu za kiume, jogoo halipandi mtungi! Yupo Kijakazi, binti aliyevunja ungo na kuposwa haraka, pia kuna Kungwi, mwanamke maalumu aliyepewa kazi ya kumuelimisha Kijakazi kwani alielekea kuwa mtu mzima sasa. Hivyo basi, wahusika wanaoonekana katika kazi hizo zote, wametoka katika jamii halisi. vijana machachari wapigania uhuru akina Denge, katika jamii ni akina Nyerere. Akina Dogoli nao wamo katika jamii yetu kwani jamii imejaa mengi.

Fasihi ni zao la jamii kwani hutumia mandhari halisi ya jamii. Katika Vuta N’kuvute, masimulizi yametumia madhari ya miji ya Zanzibar, Mombasa, Tanga na Dar es Salaam. Hii ni miji halisi wanayokaa watu. Katika Harusi ya Dogoli tunayaona mandhari ya pwani, hususani mkoa wa Bagamoyo. Pia, yapo mandhari ya nyumbani, shuleni, barabarani na mazikoni. Madhari yote yanayoonekana katika riwaya hizo mbili, yametoka katika jamii halisi jambo linalothibitisha kuwa, fasihi ni zao la jamii.

Fasihi ni zao la jamii kwani hutumia lugha itumiwayo na wanajamii. Katika Vuta N’kuvute, imetumika lugha ya Kiswahili. Lugha hii ya Kiswahili, imo katika jamii halisi. katika matumizi ya lugha, mwandishi ametumia tamathali za semi, semi na picha na taswira. Pia imetumika methali isemayo, ‘heri nusu shari kuliko shari kamili.’ Katika Harusi ya Dogoli, mwandishi ametumia lugha ya Kiswahili. Tena ametumia lugha kama inavyotumika na watu wa pwani. Sifa zake kuu zikiwa kurudiarudia maneno, kuacha nafasi, maneno mengi na utani wa kutosha. Hivyo basi, bila kuwepo kwa jamii, fasihi isingeweza kupata lugha ya kutumia na pengine fasihi isingekuwepo.

Fasihi ni zao la jamii kwani hutumia mtindo kama ule utumiwao katika jamii. Katika riwaya ya Vuta N’kuvute, tunaona mtindo wa nyimbo ukitumika. Bendi ya Cheusi dawa ilikuwa ikiimba nyimbo za taarabu na kuiburudisha hadhira. Katika riwaya ya Harusi ya Dogoli, mtindo wa mazungumzo umetumia nafsi zote tatu. Nafsi ya kwanza, ya pili na ile ya tatu. Pia, mtindo wa nyimbo umetumika. Zinaimbwa nyimbo za unyago na zile nyimbo za harusi. Hivyo basi, mitindo yote tunayoiona katika fasihi, chanzo chake ni jamii.

Kwa kuhitimisha, ni kweli kuwa fasihi ni zao la jamii. Ilianza jamii, kisha jamii ikatengeneza fasihi. Vipengele vya fani na maudhui huweza kutumika kama uthibitisho wa hoja kuwa, fasihi hutokana na jamii. Kwa kuwa jamii ndiyo iliyoitengeneza fasihi, basi jamii inatakiwa kuendelea kusoma kazi za fasihi. Bila kufanya hivyo, fasihi itapotea.

Marejeo

Mauya, A. (2016). Harusi ya Dogoli. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers.

Mwalimu Makoba 2020, imesomwa 14/12/2021, https://www.mwalimumakoba.co.tz/2020/01/maana-za-fasihi.html

Nkwera, F.M.V. (1978). Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: TPH.

Shafi, A. (1999). Vuta N’kuvute. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers.

Unahitaji Kufanyiwa Swali Lako? Gusa Hapa Kuwasiliana Nami.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne