Sababu Wanafunzi wa Kike Kutofanya Vizuri kama wa Kiume
Wanafunzi wa kiume na wale wa kike hawana tofauti katika akili zao. Ukweli ni kwamba, wanafunzi wa kike hufanya vizuri zaidi wawapo katika madarasa ya chini, na huendelea kushuka uwezo wao wa kufanya vizuri kadri wanavyozidi kuongeza madarasa. Akili ya mwanamume na mwanamke zote zipo sawa. Lakini kumekuwa na utofauti mkubwa wa ufaulu wa wanafunzi wa kike na wale wa kiume. Lakini wapo wasichana ambao pamoja na yote, bado wanafaulu vizuri kuliko wale wa kiume, hapa tutaeleza, kwa nini wanafunzi wa kiume hufaulu zaidi ukilinganisha na wale wa kike.
1.
Hofu ya kufanikiwa
Wasichana hutengenezewa hofu
ya kufanikiwa tangu wakiwa watoto. Kutokana na tamaduni zetu, wasichana huona
kama ni kosa kupigania mafanikio, hata wanapofanikiwa, hufananishwa na wale wa
kiume.
Mwanafunzi wangu mmoja
aitwaye Helena aliwahi kunisimulia mkasa wake ulionisisimua vilivyo. Anasema
akiwa darasa la kwanza, alikuwa akifanya vizuri darasani na kushika nafasi ya
kwanza. Watu wengi walimsifu kwa kuwashinda wanafunzi wenzake wa kiume. Watu
haohao waliomsifia, waliwacheka na kuwadhihaki wanafunzi wa kiume wa darasa
lake kwa kushindwa na msichana.
Alipofika darasa la tatu,
walimu walikuwa wakiingia darasani na kuwasema vibaya wanafunzi wa kiume.
Walikuwa wakiwahoji kwa nini wanakubali kushindwa na mwanamke. Helena
hakujisikia vizuri, aliona kama hakuwa na haki ya kufanya vizuri kuliko wanafunzi
wa kiume.
Mambo hayakuishia hapo,
walimu walianza kuwaadhibu kwa viboko wanafunzi wa kiume kila walipozidiwa
naye. Hali hii ilimtengenezea hali ya chuki Helena na wanafunzi wa kiume. Wapo
baadhi ya wanafunzi watukutu ambao walithubutu kumfuata na kumuonya kuwa endapo
ataongoza tena, wakichapwa viboko nao watamshikisha adabu. Kuona hivyo, Helena
aliamua kuanza kujiferisha makusudi katika mitihani. Wakati alipofanya vizuri
maneno mengi yalisemwa kumuelekea, alipofanya vibaya na darasa kuongozwa na mwanafunzi
wa kiume, walimu walipongeza kwa kusema, wanaume wa darasa wameamka!
2.
Matabaka ya ushindani
Yapo matabaka ya ushindani
yanayotofautisha jinsia. Huu ni utaratibu ambao hutenganisha wanafunzi wa kiume
na wale wa kike. Utasikia wataalamu wa elimu wakisema, aliyeongoza upande wa
wasichana ni fulani bin fulani. Jambo hili ni baya na linamfanya msichana ahisi
kama yeye hapaswi kushindana na mwanamume.
Yapo mengi, mengi tena
mengi, mengine unayoyafahamu, ongeza.