Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Kwanza

 

Mfalme na Malkia

Mako alijibanza katika kichaka cha kijani. Mbele alitazama kundi kubwa la swala. Akapiga hesabu haraka yupi amkamate. Aliona swala watatu waliokuwa na watoto, hao hakutaka kuwakamata, asingependa kuwatenga swala wale wadogo na mama zao. Basi alitazama kwa makini akagundua uwepo wa swala mzee kuliko wengine, huyo akamuwekea lengo la kumkamata.

Alichomoka katika chaka alilojificha kwa kasi kama Simba. Swala walikimbia, naye akamkimbiza mmoja aliyekuwa mzee, alitamani kwenda kumgeuza kitoweo, wadogo aliwaacha wafurahie dunia. Swala mzee alikimbia kama gari jipya, nayo mbuga ikatulia ikimtazama Mako na swala.

Kona ya kwanza ilikatwa, Mako naye akakata, kona ya pili, chenga, kona ya tatu, hola, kona ya nne, imo! Swala akakamatwa. Mako aliwinda bila silaha, yeye alikimbiza wanyama kama wafanyavyo wanyama wengine wala nyama.

Wakati yote hayo yakitokea, Malkia wa nchi ya Kanakantale alikuwa akishuhudia. Siku hiyo, yeye na wasaidizi wake, alikwenda porini kujionea wanyama. Alishangazwa mno kushuhudia mtu akiwinda bila kutumia silaha yoyote.

Malkia alisogea mpaka alipo Mako, Mako alisimama na kumpa ishara ya heshima kwa kupiga mguu wa kulia mara tatu ardhini.

“Jina lako nani?” aliuliza Malkia.

“Naitwa Mako.”

Japo haikutarajiwa, lakini Malkia alivutiwa mno na Mako. Mako alikuwa mwanamume mwenye urefu wa futi tano na nchi saba, rangi yake maji ya kunde, nywele kipilipili, tumbo limejengeka vyema, mikono imejaa misuli nayo miguu ipo imara.

Malkia alilishika tumbo la Mako, kisha akauliza swali, “Unawezaje kumkamata mnyama bila silaha?”

“Mimi hutumia mbinu anazotumia Simba au chui. Wanyama hawa huwinda bila silaha,” alijibu Mako akimchinja mnyama wake. “Malkia wangu,” aliongeza Mako, “chukua mguu, kampikie supu mfalme na wewe usisahau kula kidogo.

Mako aliondoka na kumuacha malkia akiwa na wasaidizi wake. Bila shaka nao waliondoka hapo baadae.

Mako alitembea mpaka alipofika katika mji wa Kanakantale, mji huu ulikuwa makao makuu ya nchi ya Kanakantale. Alipita katika familia duni, akagawa nyama vipande vipande. Vipande vilivyobaki alikwenda kula yeye na familia yake. Kitendo cha kugawia masikini sehemu ya mawindo, kilimfanya apendwe sana na watu wa mji wa Kanakantale. Mako hakuwa mchoyo, hakuwa na makuu.

Kwa upande wa pili, malkia hakutulia siku hiyo. Muda wote alimuwaza Mako. Kila akitoka chumba hiki akiingia kile mawazo yake yalikuwa kwa mtu mmoja.

Hata ule mguu aliopewa ampikie mfalme supu, hakufanya hivyo, aliuchukua, akawaagiza watumishi wake wauchome, nao wakakaa pamoja wakila nyama choma. Wakati wa kula, Malkia alipeleleza habari za Mako, nao wakasimulia mikasa yake.

“Malkia wangu, ninao mkasa mmoja wa Mako, naomba nikusimulie.” alisema dada wa kazi akilitafuna pande la nyama choma.

“Nisimulie.” alijibu Malkia akipaka chumvi katika pande la nyama lililometameta kwa yale mafuta yake.

Dada akakaa vizuri, wanawake wanne wakamtazama huku wakimsikiliza masikio yamewasimama kama sungura. Basi akasimulia mkasa mmoja wa Mako.

Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Pili


Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Hotuba