Matumizi ya Kiambishi ‘kwa’ | Matumizi ya Mofimu

Picha ya kuvutia.
Kiambishi ‘kwa’ kina matumizi mengi, yafuatayo ni baadhi tu ya matumizi hayo:

     1.   Kuonesha umiliki wa mahali

Tazama mifano:
Shangazi amekwenda kwa mjomba.
Musa amelala kwa baba.
Simba amepeleka maji kwa sungura.
Ongeza mifano Zaidi.

     2.   Kueleza sababu

Mifano:
Umepigwa kwa kuiba kuku.
Umehukumiwa jela miaka mitano kwa kutukana watu.
Amekufa kwa kujinyonga.
Jaribu kuweka mifano yako mingine.

     3.   Kuonesha sehemu ya kitu kizima

Mifano:
Amepata tano kwa mia moja.
Musa ana akili sana, katika mtihani amepata sabini na tano kwa mia.
Yahaya ana jitahidi, amepata saba kwa tisa.
Endapo umeelewa dhima hii, weka mifano zaidi.

     4.   Kuonesha muda uliochukuliwa na tendo fulani

Mifano:
Tulimsubiri kwa saa tisa.
Walishauriana kwa saa saba.
Walikesha kwa siku mbili wakila nyama na kucheza mziki.
Ongeza mifano mitatu zaidi.

     5.   Kulinganisha

Mifano:
Timu ya taifa ilishinda mbili kwa moja.
Simba ilifungwa tano kwa nne.
Timu ile haina kitu, imefungwa tatu kwa sifuri.
Fanya mazoezi ya kuongeza mifano zaidi ili utambue kama umeielewa dhima hii.

     6.   Kuelezea kifaa kinachotumika

Shabani ni tajiri kwelikweli, analima kwa jembe la dhahabu.
Anavuna karanga kwa koleo.
Jimotoli anachota maji kwa ndoo.
Fanya mazoezi ya kuongeza matumizi mengine, kisha mshirikishe mtu mwenye ujuzi akusahihishe.

     7.   Kueleza jinsi, namna au mbinu

Anna alipata pesa kwa kuuza vitenge.
Ntobi alikimbia kwa nguvu.
Manege anacheza kwa madaha.
Katika dhima hiyo, fikiria mifano mingine zaidi ili kupima uelewa wako.
Hayo ndiyo matumizi ya kiambishi ‘kwa’. Katika lugha ya Kiswahili, vipo viambishi vingi na kila kiambishi kimekuwa na matumizi yake.
Wanafunzi wengi hukumbwa na changamoto ya kushindwa kutambua matumizi ya viambishi na kujikuta wakitoa majibu ya kubuni, inashauriwa kuwa, ili utambue matumizi ya kiambishi fulani, basi kifanyie mazoezi kiambishi hicho kwa kukiweka katika sentensi tofauti, ni uhakika wangu kuwa, utaweza kuyaona matumizi ya kiambishi chochote. Hakuna sababu ya kushindwa.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1