Uhifadhi wa Kazi za Fasihi Simulizi | Kidato cha Pili


Uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi ni kitendo cha kutunza kazi za fasihi simulizi ili zidumu kwa muda mrefu na ziweze kutumiwa na vizazi vingi zaidi.

Njia za kuhifadhi kazi za fasihi simulizi

Kichwani

Hii ndio njia ambayo imekuwa ikitumiwa kuhifadhi kazi za fasihi tangu kale na inaendelea kutumika hadi leo. Kwa kutumia njia hii kazi ya msanii hukaa kwenye ubongo wa msanii, naye huweza kuiwasilisha kazi hiyo, wakati wowote bila gharama yoyote.

Ubora wake

1. Uwasilishaji unafanyika wakati wowote

Uwasilishaji wa kazi hiyo unaweza kufanyika wakati wowote bila kuhitaji kufanyika maandalizi yoyote, hususani ya kiufundi.

2. Hakuna gharama

Msanii hahitaji kugharimia kitu chochote ili aweze kuitoa kazi ya fasihi kichwani, ni uamzi wake tu, anaweza kuimba papo kwa papo.

3. Kazi ya fasihi iliyohifadhiwa kichwani ni hai

Hii ni kwa sababu msanii anakuwa ana kwa ana na hadhira yake. Kutokana na matumizi ya mbinu tofauti za kisanaa kama vile kucheza, kubadili sauti, miondoko na mengineyo mengi, kazi yake inapata uhalisia zaidi mbele ya hadhira.

Udhaifu wake

1. Kupotea kwa kazi ya fasihi

Kwa mfano msanii anapokuwa amefariki dunia kazi anayokuwa ameihifadhi kichwani nayo hupotea. Ndio maana katika baadhi ya jamii kazi za kifasihi zimepotea. Hii ni kwa sababu wasanii wanapoondoka duniani hondoka na fani hizo.

2. Ni rahisi kubadilika

Hii inatokea pale ambapo msanii anasahau baadhi ya maneno kutokana na umri wake au sababu nyinginezo.

Njia ya maandishi

Maandishi ni njia moja wapo inayotumika kuhifadhia kazi za fasihi. Njia hii imeanza kutumika baada ya watu kujua kusoma na kuandika. Uhifadhi wa kazi za fasihi kwa njia hii hupitia njia mbili kubwa. Hatua ya kwanza ni kubuni kisa au wazo; na hatua ya pili ni kuliweka wazo hilo katika maandishi. Kazi za fasihi simulizi zinazoweza kuhifadhiwa katika maandishi ni hadithi, nyimbo, mashairi, ngonjera, majigambo n.k

Ubora wake

1. Kazi iliyohifadhiwa inaweza kudumu kwa muda mrefu
2. Kazi iliyohifadhiwa inaweza kufikia hadhira hata ya mbali na aliko msanii.
3. Kazi iliyohifadhiwa katika maandshi haipotezi fani yake na maudhui yake bali huendelea kuwa katika asili yake ya awali hadi msanii atakapoamua kuibadilisha.

Udhaifu wake

1. Hii njia ni kwa ajili ya watu wachache tu wanaojua kusoma na kuandika.
Wasanii wanaoweza kutumia njia hii ni wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
2. Ni ghali sana kuhifadhi kazi za kifasihi kwa njia ya maandishi. Msanii atalazimika kununua vifaa vinavyohitajika katika maandishi ambavyo ni kalamu, karatasi, meza. Kwa hiyo ni aghali.
3. Uwasilishaji wake si hai kwani hakuna kuonana ana kwa ana kati ya hadhira na fanani. Kwa hiyo msomaji hawezi pata vionjo vya msanii hivyo itambidi ajibunie yeye mwenyewe.
4. Wahusika pia hawawezi kuonekana, endapo ni igizo mabalo limehifadhiwa katika maandishi, hivyo ubora wa kazi ya msanii huchujuka.

Njia ya vinasa sauti

Vinasasauti ni miongoni mwa vyombo vinavyotumika kuhifadhi kazi za fasihi simulizi. Hii ni njia iliyoendelea kuliko ile ya maandishi.

Ubora wake

Kazi ya msanii huweza kuwafikia watu hata walio mbali na alipo mtunzi.
Ikihifadhiwa katika vinasasauti kama vile tepurekoda au CD ubora wake huwa haupotei wala kuharibika endapo vifaa hivyo vitatunzwa vizuri.
Sauti ya mtunzi unaisikia moja kwa moja.
Unaweza kusikia vionjo vya msanii.

Udhaifu wake

Njia hii ni ghali kutumia, kununua vinasasauti ni gharama.
Uwasilishaji wake si hai, ingawa unaweza sikia sauti ya msanii au wahusika lakini hawawezi kuonekana.
Kazi yoyote ya kifasihi inapohifadhiwa katika vinasasauti, kwa mfano nyimbo, huwa ni mali ya msanii husika, mtu yeyote haruhusiwi kuitumia kama mali yake binafsi bila kuruhusiwa na msanii.

Njia ya kompyuta

Njia hii imeanza kutumika katika miaka ya hivi karibuni baada ya watu kuanza kujua namna ya kutumia kompyuta.

Ubora wake

Njia hii ni ya uhakika zaidi kwa vile shuguli za kisanaa zinazohusika huhifadhiwa katika kompyuta na hutolewa pale zinapokuwa zinahitajika.

Udhaifu

Msanii au wasanii wanaohusika hawawasiliani na hadhira papo kwa papo. Hivyo hadhira hukosa kuuliza maswali katika vipengele vinavyotatiza.
Ili kuhifadhi kazi ya fasihi kwa kutumia njia hii ni sharti msanii awe anajua kutumia kompyuta.
Pia ni ghali sana, kuzingatia kwamba kununua kompyuta ni gharama kubwa.

Njia ya kanda za video

Msanii huweza kutumia kanda ya video kuhifadhi kazi yake.

Ubora wake

Kwanza wasanii na vifaa wanavyotumia huonekana.
Sauti zao na milio ya ala wanazotumia husikika na pia huonekana kwa hadhira. Hii angalau huipa uhai kazi ya msanii mbele ya hadhira.
Huweza kudumu kwa muda mrefu endapo kanda ya video iliyotumika kuhifadhi kazi ya msanii itatunzwa vizuri.

Udhaifu wake

Uhifadhi wa njia hii ni ghali, msanii atahitajika kununua, kanda ya video, kumlipa mpiga picha na mzalishaji pia.
Watu wanaoweza kunufaika na njia hii ni wachache mno na wengi wao ni wale wenye uwezo wa kumiliki televisheni ambao kimsingi hupatikana maeneo ya mijini.
Ingawaje hadhira wanaweza kumwona msanii lakini hawawezi kuwasiliana nae ana kwa ana, hivyo kukosa kuuliza swali pindi wanapohitaji kufanya hivyo.

Umuhimu wa kuhifadhi kazi za fasihi simulizi

Ni muhimu kuhifadhi kazi za fasihi simulizi. Umuhimu huo,unaelezwa:

1. Ili kazi za fasihi simulizi zisipotee

Zisipopotea, zitaendelea kutumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine, hii itasaidia kurithisha maarifa yaliyomo katika kazi za fasihi.

2. Ili zitumike kama kivutio cha utalii

Kazi za fasihi simulizi zilizohifadhiwa, zinaweza kutumika kama kivutio cha watalii, kwani, watu wengi huja kutoka ng’ambo kwa lengo la kujifunza fasihi za jamii zingine.

3. Ajira

Kazi za fasihi simulizi ni ajira. Hivyo, ni muhimu kuzihifadhi ili ziendelee kutoa ajira kwa watu. Mfano, ngoma, maigizo na kazi zingine, zimewapatia kipato watu wengi.

Maswali

1. Eleza umuhimu wa kazi za fasihi simulizi.
2. Eleza namna njia hizi za uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi zinavyotofautiana:
A. Njia ya kanda za video B. Njia ya kompyuta.
3. Ni njia ipi ya uhifadhi za fasihi simulizi umeipenda, kwa nini?
4. Eleza ubora na udhaifu wa kuhifadhi kazi za fasihi simulizi kwa maandishi.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024