Uandishi | Kiswahili Kidato cha Pili
Insha za hoja
Insha
za hoja ni insha zinazoelezea jambo fulani katika hali ya kujenga hoja ambazo
zinatetea msimamo fulani alionao mwandishi wa insha hiyo juu ya jambo
analolizungumzia. Hoja ni maelezo bayana yanayotolewa na mwandishi kutetea
msimamo wake.
Katika
uandishi wa insha za aina hii, mwandishi hutakiwa kuonesha ni jambo gani ambalo
analiunga mkono na ni lipi ambalo hakubaliani nalo.
Ili
hoja zote zipate kueleweka ni sharti zipangwe katika mtiririko wa mawazo ulio
sahihi kiasi kwamba mtu aisomapo anapata kuelewa ni mada gani mwandishi
anaijadili na ana msimamo gani kuhusu mada hiyo.
Mambo ya Kuzingatia Katika Uandishi wa Insha za Hoja
Unapoandika insha za hoja, au aina zingine za insha,
zingatia mambo haya:
1. Kubaini mada ya kuandikia insha na kuielewa
vyema.
2. Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki.
3. Kutumia mtindo unaoendana na kusudi la insha. Kwa
mfano, mtindo wa masimulizi, unafaa kwa hadithi au insha zingine za kisanaa.
4. Kutumia lugha fasaha na inayoeleweka.
5. Kufuata kanuni za uandishi. Kwa mfano, matumizi
ya alama za uandishi, aya, herufi kubwa na ndogo, n.k
6. Kupanga insha katika muundo wake, yaani kichwa, utangulizi, kiini na
hitimisho.
Mfano wa Insha ya Hoja
VIJANA NA STAREHE
Vijana wengi, wake kwa waume, wamekuwa wakijiingiza
katika starehe zisizofaa ikiwemo, utumiaji wa madawa ya kulevya kama: pombe,
unga na bangi. Vijana hawafanyi kazi kwa kuelemewa na starehe. Jambo hili siyo
zuri na linaweza kuleta maafa makubwa.
Vijana hawa watakuwa na mwisho mbaya kwani pombe na
vilevi vingine wanavyotumia vinaharibu afya zao na hivyo kufupisha maisha na
kuwapa mzigo wanaowategemea pindi watakapoanza kuwauguza.
Vijana hawa hawatakuwa na maendeleo yoyote na endapo
watafika uzeeni hawatakuwa na kitu kwa sababu nguvu zao za ujana walizitumia
katika mambo yasiyofaa.
Mbali na hayo, vijana hawa wanakabiliwa na hatari ya
kuugua magonjwa ya kuambukiza kwa sababu wawapo katika starehe, wamekuwa
wakijihusisha na tabia hatarishi.
Endapo vijana hawatazinduka na kuacha starehe,
watakabiliwa na mwisho mbaya ambao utazidi kufanya nchi yetu iendelee kuwa
masikini.
Barua Rasmi
Barua
rasmi ni barua zinazohusu mambo rasmi ya kiofisi.
Dhima za barua rasmi
Dhima
za barua rasmi ni:
1.
kutoa
taarifa.
2.
kuomba
kazi au huduma.
3.
kuagiza
vitu na kutoa mwaliko kwa mfano kwa kiongozi fulani wa nchi.
4.
kutoa
malalamiko na kuweka kumbukumbu au marejeo.
Mfano wa barua rasmi
Mtaa wa Kisutu,
S.L.P 25,
Kinondoni Dar es Salaam.
28/01/2019.
Mkuu wa
shule,
Shule ya
Sekondari Kigoma,
S.L.P 175,
Kigoma.
Ndugu,
Yah: KUTUMIWA CHETI
Husika na kichwa cha barua hapo juu. Nilihitimu
kidato cha nne katika shule yako mwaka 2011. Kwa muda wote huo, sikuweza
kuchukua cheti changu cha kuhitimu elimu ya kidato cha nne.
Ninaomba unitumie cheti hicho kwa njia ya posta na
nitashukuru sana endapo utafanya hivyo.
Wako mtiifu,
A. Maiga
Chacha Maiga
Simu ya maandishi
Simu
ya maandishi ni aina ya barua fupi ambazo husafirishwa kwa haraka sana kuliko
barua za kawaida.
Simu
hizo huandikwa kwenye fomu maalumu ambazo hutolewa na shirika la posta. Simu za
maandishi hujulikana kama telegram.
Gharama
za simu za maandishi hutozwa kulingana na idadi ya maneno yaliyotumika. Kwa
hiyo ujumbe unaotumwa huandikwa kwa maneno machache ili kuepuka kutozwa gharama
kubwa.
Dhima
ya simu ya maandishi ni kutuma ujumbe wa dharura. Hivyo simu ya maandishi
huandikwa kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa haraka.
Mfano wa simu ya maandishi:
ABELI
MATHIAS SLP 5299 DSM NJOO HARAKA DADA MGONJWA SINGIDA
Kadi za mialiko
Kadi
za mialiko ni aina ya karatasi ngumu zinazopeleka taarifa fupi za kumwomba mtu
ahudhurie katika sherehe fulani kama vile harusi, ubatizo mahafali n.k
Uandishi wa dayolojia
Dayalojia
ni mazungumzo au majibizano baina ya watu wawili au zaidi wanaozungumza kwa
kupokezana. Kama zilivyo kazi nyingine za utungaji, dayalojia inaweza
kuwasilishwa kwa nijia ya mazungumzo au maandishi.
Mfano wa dayalojia
KIMATI: (Anaonekana
mwenye furaha,anamwita rafiki yake, Tazaa) Wow, Tazaa! Tumekutana tena, nafurahi
kukuona! (wanakumbatiana wote wakitabasamu.)
TAZAA: (Anatabasamu
huku ameshikilia mkono wa kulia wa Kimati, anaonesha shauku kuu.) Kimati!
Bado unanikumbuka? Nina furaha sana kwa kweli, ni muda mrefu sana.
KIMATI: (Anachekelea)
Aaaah, nahisi kama naota Tazaa, siamini kama nimekutana na wee leo hii ni muda
mrefu sana, nimefurahi kwa kweli.
TAZAA: (Anachekelea).
KIMATI: Mbona wachekelea tu…. Sema jambo rafiki.
Maswali
1.
Eleza
namna barua rasmi zinavyotofautiana na barua za kirafiki.
2.
Tunga
dayolojia kuhusu athari za madawa ya kulevya.