Jinsi ya Kuzuia Kusinzia Darasani Mwalimu Anapofundisha

Paka akiwa kalala.
Kabla mwalimu hajaingia darasani, unakuwa na nguvu za kutosha na unazungumza na wanafunzi wenzako. Mwalimu anapoingia, hali inabadilika, kadri anavyoongea na wewe ndiyo usingizi unazidi kukolea. Badala ya kuelewa kipindi, unaishia kusinzia. Sasa mwalimu katoka na usingizi nao haupo. Ni kama umerogwa eeeh? Hapana, hujarogwa hilo ni tatizo la kawaida na karibia kila mwanafunzi hukutana nalo. Tatizo la kusinzia darasani.

Kusinzia darasani kunaweza kukufanya uyachukie masomo na mwisho wake upate matokeo mabaya ya darasani kwani kile ulichotakiwa kukielewa hutakielewa kwa sababu ya kukosa usikivu. Tatizo hili linahitaji tiba, na zifuatazo ni njia za kufanya ili kuzuia kusinzia darasani.

     1.   Pangilia vizuri muda wako wa kulala

Lala muda unaofanana na amka muda unaofanana kila siku hata katika siku za mwisho wa wiki. Kwa mfano, kama unalala saa sita usiku na kuamka saa moja asubuhi, fanya hivyo siku zote. Muda wa kulala ni saa nane, hata hivyo kama ratiba yako ni ngumu, bado ni sahihi kulala saa sita au saba. Hakikisha unalala kwa angalau saa sita kwa siku, chini ya hapo ni hatari kwa afya yako na utaendelea kusinzia darasani.

     2.   Lala kidogo mchana

Baada ya kutoka darasani, lala kidogo kwa muda wa dakika 30. Hii itakuepusha kupata usingizi utakapokuwa darasani.

     3.   Fanya mazoezi

Fanya mazoezi ya kawaida ili kuchangamsha mwili wako. Wanafunzi wangu wenye tatizo la kusinzia darasani huwa nawashauri wafanye mazoezi haya: kukimbia, kuruka kamba, na ‘push up’.

     4.   Punguza kazi nyingi

Ni lazima kufanya kazi, lakini kazi nyingi zitakufanya mchovu na mwili utahitaji kupumzika na hapo ndipo usingizi unapovamia. Hivyo punguza mambo mengi. Zile safari za kumfuata msichana au kaka yule ndiyo chanzo cha uchovu unaokufanya usinzie darasani.

     5.   Usile kupita kiasi muda mfupi kabla ya kulala

Mwanafunzi wangu mmoja aliyekuwa na tatizo la kusinzia darasani, nilimshauri mambo manne hapo juu bila mafanikio, ndipo nilipokuja kugundua kuwa, kumbe mwanafunzi huyu, hula ugali mkubwa na maharage ndipo analala usiku. Jambo hili siyo jema, linachosha mwili na kesho utasinzia darasani.

Haikatazwi kula muda mfupi kabla ya kulala, lakini kula kidogo na kaa angalau kwa saa moja kabla hujalala.

Kama una tatizo la kusinzia darasani, jaribu mambo hayo matano, natumaini utapata matokeo mazuri na utafurahia masomo.


Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1