Mchezo wa Maneno Katika shairi la Mcheza Hawi Kiwete

Wanawake wanacheza mziki.


Swali
Siku zote mshairi hucheza na maneno katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii anayoiandikia. Thibitisha kauli hii kwa kutumia mifano kutoka katika shairi la ‘Mcheza hawi kiwete’ la diwani ya Wasakatonge.
Jibu
Mchezo wa maneno huhusisha mpangilio wa maneno ambayo huonekana kuwa na tahajia na hata matamshi ya namna moja lakini namna yanavyotumika yanaonesha kuwa na maana tofauti. Katika jamii ya Waswahili hutumiwa sana hususani na washairi wa Kiswahili. Kwani kuna bahari mahususi ya ushairi wa Kiswahili inayojulikana kwa jina la zivindo. Bahari hii ni mahususi katika kufundisha lugha na imejikita sana katika matumizi ya mchezo wa maneno. Mchezo wa maneno ni mbinu ambayo hutumiwa na washairi ili kutanua maana ya kile kisemwacho na kuongeza utamu wa usemaji. Mara nyingi maneno yenye umbile moja lakini maana tofauti hutumiwa kwa ajili hii. Kwa mfano katika shairi la M. Mulokozi la ‘Wale wale’ maana tatu za neno wale zinachezwa ili kuleta ujumbe fulani. Mshairi anaona kuwa hakuna mabadiliko ya msingi yaliyotokea, kundi lile lile la walaji limerejea katika madaraka. Kadhalika maneno kama ‘kura’ na ‘kula’ yanawekwa sambamba ili kuonyesha uhusiano uliopo kati ya uchaguzi na kupiga kura yaani ulaji. (M.M. Mulokozi, 1990). Katika diwani ya Wasakatonge, shairi la ‘Mcheza hawi kiwete,’ mshairi ametumia mchezo wa maneno ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii anayoiandikia kama inavyothibitishwa.
Shairi la ‘Mcheza hawi kiwete ni nasaha kwa watu kuwa, wanapotaka kufanya jambo fulani, basi wafanye jambo hilo kwa bidii kubwa bila ulegevu. Matao ni mbwembwe na machachari aliyonayo mtu katika kucheza. Kilema hawezi kucheza ndiyo maana shairi likaitwa ‘Mcheza hawi kiwete’.
Mchezo wa maneno unaonekana katika ubeti wa kwanza wa shairi. Neno ‘shika’ limeleta maana mbili tofauti. Shika iliyotumika katika mshororo wa kwanza ina maanisha mtu kupatwa na ulemavu. Shika iliyotumika katika mshororo wa tatu, ina maanisha mtu kupata ushindi.
“Mcheza hawi kiwete, kilema kilomshika,
Lau mchezo wa kete, angezila pasi shaka,
Au kama kibafute, ushindi angeushika,
Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao.”
Ujumbe unaopatikana hapa ni kwamba, ili ufanikiwe katika jambo fulani, sharti ufanye kazi kwa bidii.
Katika ubeti wa tatu, mchezo wa maneno unaleta ujumbe kuwa, ubunifu unahitajika katika kazi ili kuweza kupata mafanikio. Bila ubunifu, wapinzani wako watakuzidi na utabaki bila faida.
“Ngoma hutaka madaha, ya bashasha na kucheka,
Nyuso kubeba furaha, haiba kuongezeka,
Na nyimbo za ufasaha, si kupayukapayuka…”
Maneno: madaha, bashasha, furaha, kucheka na haiba, ndiyo ubunifu ambao mtu akiwa nao anaweza kupata mafanikio katika shughuli zake.
Katika ubeti wa tano, mchezo wa maneno unaleta ujumbe kuwa, uzembe na kukosa uaminifu ni chanzo cha kushindwa. Mwandishi anasisitiza watu wasiwe wazembe wala kupoteza uaminifu lasivyo ngoma haitachezeka ikiwa na maana ya mafanikio hayatapatikana.
“Mcheza huwa na ringo, viungo kutikisika,
Kuidengua na shingo, na viuno kubenuka,
Kucheza kwa songombingo, ngoma haitachezeka…”
Ringo, kudengua na viuno kubenuka ni bidii katika kazi, lakini songombingo ndiko kukosa bidii na matokeo yake huwa ni kushindwa.
Katika ubeti wa sita, mchezo wa maneno unaleta ujumbe kuwa, watu wafuate sheria za nchi wafanyapo shughuli zao. Kushindwa kufuata sheria za nchi kuna hasara katika nchi husika, lakini pia kuna hasara kwa mhusika menyewe.
“Mcheza hufuata dundo, vile linavyosikika,
Halichezi kwa vishindo, na mishipa kumtoka,
Ngoma huleta uhondo, raha ilokamilika…”
Mcheza hufuata dundo, vile linavyosikika, ikiwa na maana ya watu kufuata sheria, na endapo sheria zitafuatwa, basi ngoma huleta uhondo, raha ilokamilika ikiwa na maana ya kupata mafanikio kwa njia halali na kufurahia utamu wa mafanikio hayo.
Katika ubeti wa kumi, mchezo wa maneno unaleta ujumbe kuwa, watu wavivu, wasio tayari kufanya kazi kwa bidii, hawawezi kupata mafanikio.
“Wenye vilema vya mwili, ngoma mnazozitaka,
Msiitake shughuli, bure mtahangaika,
Mtapata mushkeli, mtakuja adhirika,
Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao.”
Vilema vya mwili imetumika kumaanisha uvivu, mshairi anawaasa wasiitake shughuli kwani hawatapata mafanikio. Ni ushauri mzuri kwa jamii ya Tanzania ambayo inapambana iwe nchi ya uchumi wa kati, ni lazima kila mmoja wetu afanye kazi, la svyo, bure atahangaika. Wavivu watapata mushkeli na kuja kuadhirika. Suluhisho la yote haya ni kufanya kazi kwa bidii.
Ujumbe mwingine ni umuhimu wa tamaduni zetu. Mshairi anatumia mchezo wa maneno kufikisha ujumbe huu, anasema:
“Si unyago si sindimba, na msewe kadhalika,
Hata kukiwa na rumba, machezo hayatatoka,
Mkilema hatatamba, ngoma yake kunogeka.”
Unyago, sindimba na msewe ni ngoma za asili. Bila shaka lengo la mshairi ni kutaka kuwakumbusha watu tamaduni zao ikiwemo ngoma za asili alizotaja. Taifa lisiloheshimu tamaduni zake, hilo ni taifa lililokufa. Ni muhimu kuheshimu tamaduni zetu kwani kupitia kufanya hivyo tunaweza kupata faida nyingi ikiwemo kutunza maadili na wakati mwingine kuvutia watalii na kujipatia fedha za kigeni.
Hivyo ndiyo mshairi wa diwani ya Fungate ya uhuru katika shairi la ‘mcheza hawi kiwete’ alivyotumia mchezo wa maneno kufikisha ujumbe. Mchezo wa maneno ni mbinu ambayo hutumiwa na washairi kufikisha ujumbe. Hata hivyo, zipo faida nyingi zaidi za kutumia mchezo wa maneno ikiwemo kukuza lugha.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne