Maana za Fasihi

Vitabu vimerundikwa.


Eleza kwa kina maana mbalimbali zinazozungumzia maana ya fasihi kisha eleza ubora na udhaifu wa kila fasili/maana.
Fasihi ni sanaa ambayo hutumia lugha katika kufikisha ujumbe wake. Wataalamu mbalimbali wamejaribu kutoa maana ya fasihi hivyo, zipo maana nyingi zinazozungumzia maana ya fasihi. Japo maana hizo zinatofautiana, lakini zote zinakubali ukweli kuwa, fasihi ni sanaa ambayo hutumia lugha kufikisha ujumbe wake. fasili hizi zina ubora na mapungufu yake kama inavyoelezwa hapa chini.
Fasihi ni kioo cha maisha. Kwa maana kwamba, mtu anaweza akajitazama, akaona taswira yake na akajirekebisha. Nkwera (1970). Hivyo kazi ya fasihi imefananishwa na kioo kwa sababu jamii hujiona katika kazi za fasihi kwani zinapoandikwa, huakisi yale yatokeayo katika jamii. Fasili hii ina ubora wake, lakini pia ina mapungufu nayo yanaelezwa:
Ubora wa fasili hii ni kuwa, ni kweli fasihi inawasaidia watu kujiona mambo yao wanayofanya kama kifanyavyo kioo. Kwa mfano, kupitia kazi za fasihi, watu huweza kuona yale wanayoyatenda yakisemwa katika kazi hizo. Mambo kama ulevi, ujambazi, imani za kishirikina hufanyika katika jamii na fasihi imetumika kama kioo kuyaonesha. Hivyo jamii hujiona katika kioo kinachoitwa fasihi.
Riwaya ya Takadini ni mfano wa kazi za fasihi ambazo zimesimama kama kioo. Riwaya hii inaonesha imani potofu zilizopo katika jamii ambazo zinapelekea watu wenye ulemavu kuuawa katika jamii yao wenyewe kwa hofu kwamba, endapo wakiachwa, maafa yataikumba jamii. Imani hizi hazina ukweli wowote lakini zimetajwa kuaminiwa na wanajamii hususani miaka ya zamani.
Udhaifu wa fasili hii ni kwamba, kioo hakina uwezo wa kumweleza mtu jambo la kufanya ili hali yake iwe bora zaidi. Kioo huonesha tu sehemu ya mwili lakini hakina uwezo wa kushauri. Kwa kuwa fasihi hushauri mambo ya kufanya, ni makosa kusema fasihi ni kioo kwani fasihi haiishii kuonesha tu, bali hushauri nini cha kufanya.
Pia, kwa kutumia kioo si sehemu zote za mwili ambazo unaweza kujiona. Kioo hakina uwezo wa kuonesha sehemu zote za mwili. Hivyo fasili hii haiko sawa kwa sababu fasihi imekuwa ikionesha mambo yote yanayofanyika katika jamii.
Maana nyingine ya fasihi ni ile isemayo kuwa, fasihi ni hisi. Hii ina maana kuwa, lazima kuwe na mguso fulani wa wahusika ili mtu aweze kuandika na kueleza jambo fulani. Sengo na Kiango (1973) wanasema, hisi ni kama kujisikia njaa, baridi, joto, uchovu na pengine kuumwa.
Ubora wa fasili hii ni kuwa, ni kweli kabisa baadhi ya wanafasihi huandika kazi zao kutokana na hisia zao wakati wanaandika. Wapo ambao hutunga nyimbo za hisia kali pale wanaposalitiwa na wapenzi wao hivyo fasili hii inaelekea kuwa na ukweli kwa kiasi fulani.
Hata hivyo, upo udhaifu mkubwa wa fasili hii kwa sababu inashindwa kujbu maswali kama, fasihi ina maana moja kati ya hiyo? Je uamuzi wa kutenda jambo huja wakati mtu ameguswa? Je hizo hisi ziko wapi? Je mtu ambaye haguswi sana moyoni hawezi kuwa mwanasanaa mashuhuri? Je wanamuziki ambao huusifu uzuri wa mwanamke wanaguswa moyoni? Kwa maswali haya na mengine mengi, hatuwezi kuikubali maana hii, kwa sababu haiwatoshelezi wanafasihi wa kisayansi wanaotaka kuikuza sanaa hili bila kungojea kuguswa moyoni.
Maana nyingine ya fasihi inasema, fasihi ni mwamvuli. Kwa maana kwamba, mwamvuli humkinga mtu katika mvua na jua, na fasihi huhifadhi au hukinga amali za jamii zisiharibike (Sengo na Kiango, 1973).
Ubora wa fasili hii ni kuwa, inasisitiza utunzajii wa kile kizuri kwa maana kuwa jamii inachambua kwa makini na kuona amali za jamii zinazohifadhiwa. Kaza za fasihi kama tamthiliya ya Kinjekitile, zinaendana na fasili hii kwani tamthiliya hiyo imehifadhi historia ya Tanganyika katika kipindi cha utawala wa Wadachi.
Hata hivyo, fasili hii ina mapungufu kwa sababu jamii siku zote haitulii kama maji katika mtungi. Jamii hubadilika mara kwa mara kutokana na nguvu za migongano. Kitu kipya huzaliwa na cha zamani hufa. Basi kwa maana hiyo, hakuna haja ya kuhifadhi amali za jamii katika mwamvuli kwa sababu wimbi la mabadiliko litautoboa mwavuli huu.
Maana nyingine ya fasihi ni ile isemayo, fasihi ni sanaa ya uchambuzi wa lugha yoyote kadri inavyosemwa, inavyoandikwa na kusomwa. Maana hii inakuja kwa sababu msingi mkubwa wa fasihi ni lugha.
Ubora wa fasili hii ni kuwa, ni kweli lazima fasihi itumie lugha kwani lugha ndicho chombo muhimu kitumiwacho na fasihi na si fasihi tu bali taaluma zote hutumia lugha. Hivyo kwa kuwa lugha ndiyo chombo muhimu katika fasihi basi fasihi ni sanaa ya uchambuzi wa lugha yoyote kadri inavyosemwa.
Fasili hii ina mapungufu, imejikita katika uchambuzi wa lugha kana kwamba hakuna vipengele vingine vinavyochambuliwa katika fasihi zaidi ya lugha. Ukweli ni kwamba katika fasihi kuna vipengele vingine ambavyo huchambuliwa, vipengele hivyo ni kama wahusika, mtindo, muundo na mandhari.
Maana nyingine ya fasihi inasema, fasihi ni kielelezo cha hisia za mwandishi juu ya mambo yanayomwathiri yeye, kikundi cha jamii nzima anamoishi na kwamba lengo lake ni kustarehesha au kufunza wasomaji wake.
Ubora wa fasili hii ni kwamba, ni kweli kabisa fasihi hutumika kama kielelezo cha hisia za mwandishi juu ya mambo yanayomwathiri yeye au jamii yake. Hutokea mwandishi akaandika kazi ya fasihi kutokana na matatizo fulani aliyonayo katika maisha yake ikiwemo masuala ya mapenzi, maradhi au umasikini. Pia, kazi nyingi za fasihi ni kielelezo cha maisha katika jamii. Kazi nyingi zinazungumzia yale yanayotokea katika jami yetu halisi.
Mapungufu ya fasili hii ni kwamba, inampa uwezo mkubwa sana mwandishi, inamfanya aonekane kama chanzo pekee cha uumbaji wa sanaa na hasa akili yake. Fasili hii ni matokeo ya falsafa ya kidhanifu kwa kuhusisha uchambuzi wa mambo katika fikra bila kutazama hali halisi ya maisha ya watu.
Maana nyingine ya fasihi inasema, fasihi ni chombo cha utetezi wa maslahi ya tabaka moja au jingine na kwamba mwandishi ni mtumishi wake anayejijua au asiyejijua, atake asitake mwandishi huyu huwa na lengo au dhamira fulani anayotaka kuionyesha. Wasomaji wanaweza kuyakataa au kuyakubali maudhui ya kazi yake na pengine fani kufuatana na msimamo juu ya itikadi ya kisiasa inayotawala katika kipindi kile na jinsi mwandishi anavyoainisha maandishi yake na itikadi hiyo.
Ubora wa maana hii ni kuwa, fasihi ni mojawapo ya silaha nyingi zinazotumiwa na tabaka moja kutetea maslahi yake katika mapambano ya kudumu dhidi ya matabaka mengine. Diwani ya Wasakatonge ni mfano wa kazi za fasihi ambazo zimeandikwa kuwakilisha mapambano ya watu wa tabaka la chini dhidi ya wale wa tabaka la juu katika kulisaka tonge.
Maana hii ina mapungufu, si kila kazi ya fasihi inayoandikwa inalenga kutetea tabaka fulani. Katika dunia ya sasa, wanafasihi wengi wanatetea matumbo yao wenyewe na wapo ambao wanafanya bila kutetea tabaka lolote. Kwa mfano, ni vigumu kubaini mwanafasihi anatetea tabaka gani pale anapotunga wimbo wa kusifia uzuri wa mwanamke wake, kwani hatujui mwanamke huyu anatoka katika tabaka la juu au la chini.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba, fasili za fasihi zilizotolewa na wataalamu mbalimbali ni nyingi. Fasili hizo, zina ubora na mapungufu yake. Hata hivyo, maana inayoelekea kukubalika zaidi ni ile isemayo, fasihi ni sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe wake kwa jamii. Maana hii ni bora kwa sababu kwanza, inakubali ukweli kuwa fasihi ni sanaa inayotumia lugha. Hakuna kazi yoyote ya fasihi ambayo inaweza kufikishwa kwa jamii bila kutumia lugha. Riwaya, tamthiliya na ushairi, vyote hutumia lugha. Pili, fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake kwa jamii, kumbe basi lengo la fasihi ni kuweza kufikisha ujumbe kwa jamii iliyokusudiwa. Kazi za fasihi hutoa ujumbe wa kutosha katika jamii ikiwemo kuiasa jamii kuachana na imani potofu, kufanya kazi kwa jamii, kuachana na uhalifu na mambo mengi yenye manufaa katika jamii hufundishwa katika kazi za fasihi kwa kutumia lugha.

Marejeo

Nkwera, F.M.V. (1978). Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: TPH.
Ndungo, C.M. (1991). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: University of Nairobi.
Masebo, J & Nyambari N. (2000). Nadharia ya Fasihi. Dar es Salaam: Nyambari Nyangwine Publishers.
https://www.mwalimumakoba.co.tz/2017/09/nadharia-mbalimbali-zinazoelezea-maana.html

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie