Watekaji | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 2

bwana Mako kasimama na panga lake la kung'aa
Mkasa wa Pili
Watekaji
“Zaidi ya watoto elfu moja wametekwa na majambazi ambao wamedai hawawezi kuwaachia mpaka wapewe kiasi cha Shilingi Trilioni saba…” ilisikika taarifa ya habari katika redio ndogo aliyokuwa akisikiliza Bwana Mako mchana saa sita. Mako huishi mjini na kijijini, nchi kavu na majini, na mara chache angani. Leo alikuwa mjini alipopokea taarifa hiyo.
“Juhudi za kuwaokoa zimegonga mwamba,” iliendelea taarifa, “watekaji wametishia kuwaua watoto wote endapo hawatalipwa fedha wanazotaka ndani ya dakika 30. Pia wametaja mfumo wa malipo hayo ufanyike kwa njia ya mtandao na malipo yawe katika Bitcoin.”
Bwana Mako alitambua kuwa siku hiyo kulikuwa na sherehe iliyohusisha watoto wa viongozi na wafanyabiashara wakubwa nchini kwake. Watoto hao wa wakubwa, walikutana pamoja katika sherehe iliyohusisha michezo mingi ikiwemo kuogelea. Bwana Mako hakupenda sherehe za aina hizi kwa sababu kwake yeye hazikuwa na maana yoyote zaidi ya ubaguzi tu, kwani watoto wa hohehahe hawakupata nafasi ya kuwa hapo. Hata hivyo, japo hakukubaliana na sherehe hizo, kitendo cha watoto wasio na hatia kutekwa hakikumfurahisha hata kidogo, alitambua kuwa watoto wale hawakuwa na kosa.
Kwa haraka aliingia katika chumba maalumu, humo alitoka na bunduki aina ya Colt M4 Commando akaipachika ndani ya mfuko wa koti kubwa alilovaa siku hiyo kisha akaelekea eneo la tukio. Bwana Mako hutumia bunduki ya aina hii akiwa na hasira sana.
Bwana Mako aliendesha pikipiki mpaka katika jengo moja refu, akapanda mpaka juu ya jengo hilo kisha akachukua darubini yake ili aweze kuwaona watekaji.
Alifanikiwa kuona wanaume watatu wa kizungu wakiwa wameshika vyema bunduki zao aina ya AK 47. watekaji hao walikuwa wametawanyika na kutengeneza umbo la pembe tatu, watoto waliwekwa katikati na hakuna aliyeruhusiwa kujitikisa. Alishuka haraka katika jengo na kuanza kuelekea walipo watekaji wale. Njiani aliendelea kutunga njia za kuwamaliza.
Pikipiki aliiacha mbali kidogo kwani sauti yake ingewashtua watekaji na pengine kuhisi wanafuatiliwa hivyo kuwaua mateka wao. Alipofika hatua chache kuelekea eneo la tukio aliona kamba za njano zimezungushwa nazo zimeandikwa, ‘usivuke hapa.’ Kumbe watekaji wale walizungusha uzio ili watu wasiohusika wasivuke msitari huo na labda ndiyo sababu hapakuwa na askari yeyote karibu. Inaonekana watekaji walitumia mbinu hii ili iwe rahisi kwao kutoroka pindi watakapopewa fedha walizotaka.
Bwana Mako aliangaza kila kona ili kujiridhisha kuwa hakuna mtu aliyemuona, haikuchukua muda, aligundua uwepo wa askari wengi waliojificha pembezoni pengine nao walipanga mipango ya kuokoa watoto wale. Pia alitambua uwepo wa kamera ndani ya jengo walilotekwa watoto ambapo watekaji walikuwa wakiona yote yanayotendeka nje na endapo wangeona juhudi zozote za kutaka kuokoa watoto bila fedha, watoto wangekuwa hatarini. Wakati haya yanatendeka, zilibaki dakika 10 zile dakika 30 zilizotolewa na watekaji ziishe!
Bwana Mako hakuwajali askari waliokuwa pembeni, akatambaa kama nyoka mpaka alipoufikia ukuta wa jengo. Akiwa hapo akaukwea ukuta mithili ya mjusi mpaka akawa juu ya jengo. Jengo hili upande wa juu lipo wazi hivyo Bwana Mako akawaona watekaji wote, wakati anawaona watekaji, askari waliokuwa nje nao walimuona wasijue mtu yule katoka wapi.
Kitu kipya alichogundua ni kwamba, watekaji hawakuwa watatu, bali walikuwa wanne, mmoja alikuwa katika kona akiwa na kompyuta ndogo, bila shaka alikuwa akikagua kama fedha walizodai zililipwa au la.
Bwana Mako alitunga upya sheria zake kwani alizotunga awali zililenga kupambana na watu watatu, kumbe sasa wapo wanne. Alipomaliza mpango wake akaanza kazi.
Alilenga shabaha kwa wale watu watatu, waliosimama na silaha, akampiga mmoja, wakati wawili wakitafuta adui alipo, alimdungua mwingine kisha akammalizia yule wa tatu. Bwana Mako alikuwa na uwezo wa kummaliza yule jamaa wa nne aliyekuwa na kompyuta ndogo, lakini aliamua kuwapa burudani watoto.
Aliruka kutoka juu, akatua ndani ya jengo. Yule mtekaji aliyekuwa kashughulika na kompyuta akawa anakimbia kwenda kuchukua moja ya bunduki zilizokuwa zimeshikiliwa na wale watekaji wenzake. Alichelewa, Bwana Mako alimkanyaga teke akadondoka.
Mtekaji yule aliinuka, akakunja ngumi ili apambane, Bwana Mako akawageukia watoto akawaambia, “Watoto, nimekuja kuwaokoa, watekaji wote nimewamaliza isipokuwa huyu mmoja. Sasa nawaomba mnishangilie kwa nguvu ili niweze kumshinda huyu adui, akinipiga ngumi zomeeni, nikimpiga shangilieni mkilitaja jina langu, Maaako… Maaako… Maaako… halafu ili kutunza kumbukumbu, washeni simu zenu muweze kuchukua video za tukio hili!”
Bwana Mako alikuwa na uwezo wa kummaliza adui yule kwa sekunde moja tu, lakini alitaka kuwaburudisha watoto, Bwana Mako wakati mwingine hupenda sifa. Basi Mtekaji akarusha ngumi, Ikampata Bwana Mako watoto wakazomea. Bwana Mako akarusha ngumi, ikampata mtekaji watoto wakashangilia, ikawa ni kurusha ngumi na kujibu mpaka Bwana Mako alipoamua kuhitimisha burudani, aliruka juu kama mwewe akiwa amenyoosha vidole vyake kama panga, alipotua akampiga dhoruba moja mtekaji ambaye aliitikia kwa kudondoka chini akiwa amepoteza fahamu, kisha Bwana Mako kwa kutaka sifa zaidi akalia kwa sauti kubwa akipiga kifua chake, “Hiyaaaaaaaaaa!” watoto walijua kumfurahisha Bwana Mako, wakashangilia, “Maaako…. Maaakooo…. Maaakooo.”
“Watoto,” aliita Bwana Mako akivaa vyema koti lake jeusi, “nimekuja kuwaokoa na tayari adui zenu wamekwisha lala chini. Mimi narudi nyumbani, siwezi kubaki hapa kwa sababu askari wakija wataninyang’anya bunduki yangu nami naipenda sana. Wakikuulizeni nani kawaokoa, waambieni ni Bwana Mako, waonesheni video zangu mlizorekodi.”
Alipomaliza kusema hayo, watoto wakamzunguka kila mmoja akitaka kumshika mkono wa kwa heri, wakati zoezi hilo likiendelea, geti la kuingilia likavunjwa, askari wengi wakaingia wakiwa na silaha, watoto wakamtazama Bwana Mako kwa hofu, wakihofia kuwa sasa atanyang’anywa siraha yake anayoipenda, lakini hawakumuona… Bwana Mako alikwisha ondoka eneo hilo na bila shaka alikuwa nyumbani kwake!

Jiunge katika Group la whatsapp uwe wa kwanza kupokea mkasa wa tatu Jiunge Hapa

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024