Mambo ya Kuzingatia Kabla na Wakati wa Mtihani

wanafunzi wakiwa na baiskeli
Nifanye nini ili nifaulu? Naulizwa kila siku swali hili.
Sijawahi kumshuhudia mwanafunzi asiye na hofu ya mtihani, hata wenye uwezo mkubwa tena waliosoma mada zote, huhofia mtihani unapokaribia. Hofu hii ni kitu cha kawaida, inakusaidia usijiamini kupita kiasi na uwe makini, hivyo usihofu kuhofia, bali kuwa na hofu pale uikosapo hofu!
Hata hivyo, kuwa na hofu kupita kiasi ni tatizo, tafadhali hebu jiamini… Unaweza, usiogope sana!
Nimekuwa nikifuatwa kwa njia ya teknolojia na miguu na makumi elfu ya wanafunzi wakiniuliza, “mwalimu wa walimu na wanafunzi, tufanye nini tufaulu?” nami huwajibu, “kuwa makini kabla ya mtihani na wakati wa mtihani.”

Mambo ya Kuzingatia Wakati wa Mtihani

zingatia mambo haya:

Usiwe na hofu

Jiamini unaweza kufanya mtihani wako na ukapata matokeo mazuri. Hakuna jipya katika mtihani, hakuna gumu, yote ni kawaida na kazi yako ni kuthibitisha kuwa una maarifa fulani katika kichwa chako.

Kula kidogo

Ubongo wako unahitaji chakula ili uweze kufanya kazi. Usiingie katika mtihani ukiwa na njaa. Hakikisha umekula, lakini usile kupita kiasi, kula kidogo.

Soma maswali kwa makini

Kuwa makini katika kusoma maswali yako na hakikisha unaelewa maswali hayo yanataka majibu gani. Kushindwa kusoma maswali kwa makini ni kushindwa kuyapata maswali hayo, hivyo kuwa makini sana hapa.

Tumia muda vizuri

Hakikisha uingiapo katika mtihani una saa yako ya mkononi. Hii itakusaidia kujua muda unaotumia kujibu maswali, pia inakuepusha na hofu juu ya muda uliosalia kuisha kwa mtihani wako.

Jibu maswali unayoyaweza

Anza kujibu maswali unayoyaweza, katika mtihani unaruhusiwa kuanza kujibu swali lolote. Unaweza ukaanza na swali la tisa kisha likafuata la kwanza. Hivyo anza na maswali mepesi na hapo baadaye, maliza na magumu.

Usijibu kupita kiasi

Kuandika sana hakukufanyi upate alama nyingi. Katika mtihani wako, andika mambo ya msingi pekee. Kwa mfano, katika maswali ya kujieleza, katika aya moja inatarajiwa kuwa na mistari mitano mpaka 10.
Naomba niishie hapo, zingatia sana hayo niliyosema… oooh, kuna kitu nimesahau, wakati naandika nilitakiwa kuanza na mambo ya kuzingatia kabla ya mtihani, sasa nimeanza na mambo ya kuzingatia wakati wa mtihani! Nimeanza kuzeeka? Mbona bado ningali mwalimu kijana… balaa gani hili? Ptuuuuuh!

Mambo ya kuzingatia kabla ya mtihani

1. Soma mada zote.
2. Elewa mada ulizosoma, usikariri.
3. Shirikiana na wenzako.
4. Fanya mitihani ya kujipima. Habari njema ni kwamba hata kama uko mbali na huna mwalimu, mitihani yangu ya Mwalimu Makoba online Examination unaweza kuifanya ukiwa popote. Asante teknolojia!
5. Pitia maswali ya mwisho ya kujiandaa kufanya mtihani wako. Chini hapo nimekuwekea link ya kuwasiliana nami ili uweze kuyapata.
Mwisho, nakutakia maandalizi mema ya mtihani na mtihani mwema rahisi unaojibika.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie