Uandishi | Kidato cha Kwanza Mpaka cha Nne

mzee akiandika

Uandishi wa Insha

Insha ni mfululizo wa sentensi zinazohusiana na mada inayozungumziwa au kuandikwa. Urefu au ufupi wa insha hutegemea mada husika inayojadiliwa.

Muundo wa Insha

Insha bora inatakiwa iwe na muundo huu:
Kichwa cha insha
Mwanzo au utangulizi wa insha
Kiini cha insha
Mwisho wa insha

Insha za wasifu

insha za wasifu ni isha zinazoelezea uzuri wa kitu, mtu, mahali au hali fulani.

Mfano wa insha ya wasifu

BAHARI YA HINDI
Bahari ya Hindi ni bahari kubwa inayobeba eneo la mashariki mwa Afrika mpaka kwenda India. Nchini Tanzania, bahari ya Hindi ipo katika mikoa ya: Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Bahari hii ni miongoni mwa maliasili zenye thamani nchini Tanzania.
Bahari ya Hindi huonekani ya bluu ukiitazama kwa mbali. Hii ni kwa sababu maji yake huakisi mawingu na kuifanya ionekane kama ya bluu. Hata hivyo, ukiyafikia maji yake ni meupe tena safi.
Bahari ya Hindi pembezoni kabla ya kuyafikia maji ina mchanga mwingi. Mchanga huu huwafanya watu wanaotembelea bahari hii wakae huku wakifurahia hali ya hewa ya baharini ambayo huambatana na upepo mzuri.
Bahari ya Hindi ina mimea mingi kando yake. Mimea hii yote ni ya kijani. Pia, miti ya minazi ni mingi kandokando mwa bahari. Mimea hii, hupepea kufuata upepo, pale upepo unapovuma.
Bahari ya Hindi ni kivutio cha watalii. Wapo watu ambao hutembelea Tanzania ili waweze kujionea kwa macho uzuri wa bahari hii. Miongoni mwa watalii hao ni wale wa ndani na wa nje. Watalii watembeleapo bahari yetu, hutoa fedha za kigeni na kusaidia kukuza pato la nchi.
Bahari ya Hindi ni chanzo cha maisha ya viumbe wengine kama samaki na nyangumi. Uwepo wa samaki umewafanya waTanzania wengi wajiingize katika shughuli za uvuvi na kuwafanya wajipatie kipato ambacho kinafanya waweze kuendesha maisha yao.
Bahari ya Hindi maji yake ni ya chumvi. Maji haya huwafanya wale wanaooga wayateme haraka pindi yanapoingia mdomoni kwa bahati mbaya. Hata hivyo, maji haya ya chumvi ni faida kubwa kwani uzarishaji wa chumvi nyingi hutoka katika maji hayo ya baharini.
Bahari ya Hindi ina sifa lukuki ambazo haziishi kuelezeka. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha bahari hii inaendelea kuwa safi na salama kwani inaliletea taifa letu heshima na fedha za kutosha.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne