Maana na Muundo wa Vitendawili Katika Lugha ya Kiswahili

nanasi
Maana ya vitendawili
Vitendawili ni maneno yanayoficha maana ya kitu ili kisijulikane kwa urahisi. Kwa mfano, naweza kusema, “kuku wangu ametagia mwibani.” Hapo nakuwa nimeficha maana ya jambo hilo ambapo ukitafakari kwa makini kisha ukahusianisha na mazingira, jibu lake ni nanasi.
Muundo wa vitendawili
Vitendawili vipo katika muundo huu:
Utangulizi wa Kitendawili
Utangulizi huanza kwa kuuliza, “Kitendawili.” Hadhira huitikia, “Tega.”
Swali
Hapa mtega kitendawili huuliza swali lake, kwa mfano: “Mama hachoki kunibeba.” Swali hili huelekezwa kwa hadhira ili waweze kutoa majibu.
Jibu
Hadhira huweza kutoa jibu sahihi au lisilo sahihi. Katika swali hapo juu, mtoa jibu anaweza kujibu, “Kitanda.” na mtega Kitendawili akakubali kuwa amepata.
Endapo jibu litakalotolewa halitakuwa sahihi, mtega Kitendawili hupewa mji ili aweze kutoa jibu la Kitendawili chake.
Kwa mfano, jibu linapokosekana, fanani ambaye ndiye mtega Kitendawili huwaambia hadhira ambao ndiyo wanaopaswa kutegua kitendawili, “nipeni mji.” hadhira huitikia kwa kumpa mji, “Nenda Tanga.” Fanani asiporidhishwa hujibu,
“Siendi!”
“Nenda Mbeya.”
“Nakwenda,” akiisha kusema anakwenda, hutoa jibu la kitendawili chake kisha huwa zamu ya mtu mwingine kutega kitendawili. Jambo la kufurahisha katika vitendawili ni kwamba, kila mtu anaweza kuwa fanani au hadhira kwa wakati mmoja kwa sababu, mara nyingi vitendawili hutegwa kwa zamu.
Miaka ya hivi karibuni, vitendawili vimezidi kupotea kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Ule muda uliokuwa unatumiwa kutega na kutegua vitendawili, sasa unatumiwa kufuatilia habari mtandaoni.
Mahali pekee ambako panaweza kuokoa kifo cha vitendawili ni shuleni. Walimu wakiwaongoza wanafunzi wao kutega na kutegua vitendawili, hapana shaka kuwa taaluma hii itaendelea kusalia kwa miaka mingi pengine hata milele.
Vitendawili katika lugha ya kiswahili ni sehemu ya utamaduni wetu, hivyo ni lazima tuhakikishe vinaendelea kuwako jana, leo, kesho na kesho kutwa.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi

Chimbuko la Fasihi na Sanaa, Mtazamo wa Kiyakinifu na Kidhanifu