Mtihani wa Kiswahili kwa Kidato cha Nne| Pre Necta20

Mtihani wa Kiswahili kwa Kidato cha Nne| Pre Necta20

Endapo unataka kufanya mtihani huu ili usahihishwe na Mwalimu Makoba, zingatia mambo haya:

1. Mtu yeyote na kokote aliko anaruhusiwa kufanya mtihani huu.
2. Fanya mtihani huu kwa kutumia aina yoyote ya karatasi.
3. Ukimaliza, piga picha karatasi hizo kisha zitume WhatsApp kwenye namba ya Mwalimu Makoba, 0754 89 53 21.
4. Subiri mtihani wako usahihishwe, Urudishiwe na ufanyiwe masahihisho.
5. Gharama ya mtihani huu ni shilingi 2,000/= (elfu mbili) tu.
Namba za malipo ni: M – Pesa 0754 89 53 21 (Daud Mhuli) na Tigo pesa 0653 25 05 66 (Daud Makoba)
“Kwa kuwa lengo la mtihani huu ni kutaka kujua uwezo na mapungufu ya mwanafunzi ili aweze kupewa mbinu mbadala za kumsaidia kufaulu mtihani wake wa mwisho, kuangalizia majibu hakuna faida yoyote kwani lengo la mtihani si kubaini nani atakuwa wa kwanza na yupi atakuwa wa mwisho!”
Sasa fanya mtihani wako…

Sehemu A (Alama 10) UFAHAMU

1. Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata.
Nchi yetu Tanzania imebarikiwa kwelikweli. Inavyo vivutio vingi ambavyo vinaifanya izidi kuheshimika kila kukuchapo. Uzuri wake na maajabu yake, utakuacha kinywa wazi ukiushuhudia.
Kuna maziwa yenye maji safi. Katika maziwa haya, kuna samaki wengi ambao ni kitoweo safi chenye virutubisho vya kutosha. Uwepo wa maziwa haya, unasaidia katika kutoa ajira, kwani watu wengi wamejiajiri au kuajiliwa katika uvuvi.
Bahari ina faida sawa na zile za maziwa. Uwepo wake ni chanzo kikubwa cha mapato katika taifa letu. Uwepo wa fukwe umekuwa baraka kubwa.
Viko vingi vya kuzungumza kuhusu Tanzania ambavyo kusema kweli ni ngumu sana kuvimaliza katika karatasi. Ila nimalize kwa kuuzungumzia mlima mrefu kuliko yote Afrika. Kilimanjaro.
Kilimanjaro ni mlima ambao umeitangaza zaidi Tanzania na kuipatia watalii lukuki ambao huja kutazama hiki na kile kinachofanyika nchini. Mlima huu unavyo vilele viwili: Kibo na Mawenzi.
Watalii maridadi hupanda juu ya mlima huu na kufika kileleni wakiwa hoi. Hata hivyo, kufika kileleni huwafanya wasahau machungu yao na kujikuta wakitabasamu kwa sababu wametimiza malengo.
Hata hivyo, Watanzania wengi hawaonekani kupenda utalii wa ndani. Hawaonekani kutembelea vivutio vyao kama wanavyofanya wageni. Hofu yangu ni kwamba, huenda wageni wanajua vitu vyetu zaidi kuliko tunavyovijua sisi! Aibu.

Maswali

(a) Andika kichwa cha habari hii kisichozidi maneno manne.
(b) Taja dhamira kuu inayotokana na habari hii.
(c) Mwandishi anatoa ushahidi gani kuthibitisha kuwa nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii?
(d) “Hata hivyo, Watanzania wengi hawaonekani kupenda utalii wa ndani” Thibitisha kauli hii kwa mujibu wa habari uliyosoma.
(e) Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika kufungu cha habari
(i) maridadi
(ii) kileleni
2. Fupisha habari uliyosoma kwa maneno yasiyozidi arobaini (40).

SEHEMU B (Alama 25) SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA

3. Taja aina za sentensi zifuatazo kisha eleza muundo ujengao kila sentensi.
(a) Maisha ni safari ndefu.
(b) Ukisoma kwa bidii utafaulu kwa kiwango cha juu.
(c) Mtoto aliyelazwa hospitalini ameruhusiwa kwenda nyumbani.
(d) Nitakuja leo ingawa nitachelewa sana.
(e) Alinunua madaftari lakini kitabu cha Kiswahili alipewa na mwalimu.
4. Andika maneno matano ambayo yameundwa kutokana na kufananisha sauti. Kwa kila neno tunga sentensi moja.

SEHEMU C (Alama 10) UANDISHI

5. Andika insha isiyozidi maneno mia tatu (300) na isiyopungua mia mbili na hamsini (250) kuhusu faida za kompyuta kwa jamii.

SEHEMU D (Alama 10) MAENDELEO YA KISWAHILI

6. Taasisi ya Elimu (TET) na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ni miongoni mwa asasi zilizoanza mara tu baada ya uhuru. Fafanua kazi tatu kwa kila moja katika kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Tanzania.

SEHEMU E (Alama 45) FASIHI KWA UJUMLA

Jibu maswali matatu (3) kutoka katika sehemu hii. Swali la 11 ni la lazima.

7. Vitendawili vina dhima kedekede. Fafanua dhima tano za vitendawili kwa jamii.
8. "Mshairi ni mwelimishaji wa watawala." Jadili kauli hii kwa kutoa hoja tatu kutoka katika kila diwani kati ya diwani mbili ulizosoma.
9. "Fasihi ya Kiswahili haikamiliki bila kumjadili mwanamke." Thibitisha usemi huu kwa kutumia hoja tatu kwa kila riwaya kutoka katika riwaya mbili ulizosoma.
10. Kwa kutumia hoja tatu kwa kila tamthiliya kutoka katika tamthiliya mbili ulizosoma, jadili kufaulu kwa waandishi katika kipengele cha utumizi wa tamathali za semi.
11. A. Nini maana ya visasili?
B. Tunga kisasili kuhusu kisa chochote.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu