Mtihani wa Kiswahili Kidato cha Nne| Pre Necta 19

Mtihani wa Kiswahili Kidato cha Nne| Pre Necta 19
Endapo unataka kufanya mtihani huu ili usahihishwe na Mwalimu Makoba, zingatia mambo haya:
1. Mtu yeyote na kokote aliko anaruhusiwa kufanya mtihani huu.
2. Fanya mtihani huu kwa kutumia aina yoyote ya karatasi.
3. Ukimaliza, piga picha karatasi hizo kisha zitume WhatsApp kwenye namba ya Mwalimu Makoba, 0754 89 53 21.
4. Subiri mtihani wako usahihishwe, Urudishiwe na ufanyiwe masahihisho.
5. Gharama ya mtihani huu ni shilingi 2,000/= (elfu mbili) tu.
Namba za malipo ni: M – Pesa 0754 89 53 21 (Daud Mhuli) na Tigo pesa 0653 25 05 66 (Daud Makoba)
“Kwa kuwa lengo la mtihani huu ni kutaka kujua uwezo na mapungufu ya mwanafunzi ili aweze kupewa mbinu mbadala za kumsaidia kufaulu mtihani wake wa mwisho, kuangalizia majibu hakuna faida yoyote kwani lengo la mtihani si kubaini nani atakuwa wa kwanza na yupi atakuwa wa mwisho!”
Mwalimu Makoba, Mwalimu wa Walimu na Wanafunzi, Mwalimu wa Ushindi!
Sasa fanya mtihani wako…
Sehemu A (Alama 10)
Ufahamu
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
1. Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata.
Tamaduni za waafrika ni tofauti sana na zile za wazungu. Utofauti huu umesababishwa na umbali wa kijiografia baina ya makundi haya mawili ya wanadamu. Hapo zamani palitokea uvumi kuwa, waafrika hawakuwa na utamaduni wao wenyewe. Mawazo haya yalilenga kuwanyong’onyeza watu weusi ili wapate kutawaliwa.
Mitindo ya mavazi ya waafrika imebadilika kwa karne nyingi, hivi sasa, mavazi mafupi yasiyositiri mwili vizuri yanaonekana kuwa si sehemu ya utamaduni wa mtu mweusi. Wapo wanaohoji kuwa, jamii za kiafrika hapo kale zilikuwa zikivaa mavazi mafupi zaidi ya haya tuyaonayo. Jibu lake ni kwamba, hakuna tamaduni zisizobadilika, huko tumetoka na tuko sehemu nyingine.
Mwafrika anapoongea na mkubwa hamtazami usoni, endapo atamtazama, maana yake ni kwamba, kijana huyu hana nidhamu na ni nunda. Kwa mzungu, kuzungumza na mkubwa bila kumtazama usoni ni ishara kwamba unayosema si kweli na huenda ukawa mwizi au laghai.
Tamaduni ni jambo gumu kwa sababu katika kila jamii kuna tamaduni zao. Hata hivyo, yapo mambo ambayo yanaunganisha tamaduni za dunia nzima. Mambo hayo ni kama: mchezo wa soka, kikapu na riadha. Kuwako kwa mfanano na mwingiliano huu, ni matokeo ya utandawazi.
Maswali
A. Eleza sababu ya tofauti ya tamaduni za wazungu na zile za waafrika.
B. Fafanua kwa nini mwafrika anapoongea na mkubwa hamtazami usoni.
C. Ni ipi sababu ya mwingiliano wa tamaduni?
D. Kipi kinafaa kuwa kichwa cha habari hii?
2. Fupisha habari uliyosoma kwa maneno yasiyopungua 80 na yasiyozidi 100.
Sehemu B (Alama 25)
Sarufi na utumizi wa lugha
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
3. Katika kila sentensi uliyopewa, orodhesha vishazi huru katika Safu A na vishazi tegemezi katika safu B.
(a) Ngoma hailii vizuri kwa kuwa imepasuka.
(b) Watoto walioandikishwa watakuja kesho.
(c) Kiongozi atakayefunga mkutano amepelekewa taarifa.
(d) Mtawatambua walio wasikivu.
(e) Kitabu ulichopewa kina kurasa nyingi.
4. Toa maana tano tofauti za neno “kibao” kisha tunga sentensi moja kwa kila maana uliyotoa.
Sehemu C (Alama 10)
Uandishi
Jibu swali moja (1) kutoka sehemu hii.
5. Andika barua kwa rafiki yako ukimweleza maandalizi yako ya mtihani wa kidato cha nne. Jina la rifiki yako liwe Doto Joto wa S.L.P 400 Shinyanga na jina lako liwe Kijoto Bohari wa Shule ya Sekondari Samata, S.L.P 700 Dar-es-Salaam.
Sehemu D (Alama 10)
Maendeleo ya Kiswahili
6. Elezea vyanzo vitano vya lahaja katika lugha ya Kiswahili.
Sehemu E (Alama 45)
Fasihi kwa Ujumla
Jibu maswali matatu, swali la 11 ni la lazima
7. Fafanu hasara za kuhifadhi fasihi simulizi katika maandishi.
8. “Kwa kuwa msanii ni mzawa wa jamii, basi haandiki kitu isipokuwa kinaihusu jamii hiyo.” Jadili kauli hii kwa kutumia hoja tatu kutoka katika kila diwani katika diwani mbili ulizosoma.
9. “Elimu ni chanzo cha mafanikio.” Fafanua kauli hii kwa kutoa hoja tatu kwa kila kitabu kati ya vitabu viwili vya riwaya vilivyoorodheshwa.
10. “Katika kazi ya fasihi, wapo wahusika mfano wa kuigwa na jamii kwa matendo yao mazuri.” Thibitisha kauli hii kwa kutumia hoja tatu kwa kila mhusika kutoka katika tamthiliya mbili ulizosoma.
11. Tunga shairi la kimapokeo lenye beti nne kuhusu “mbwa wako aliyekufa kwa kugongwa na gari.”

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie