Mtihani wa Kiswahili Kidato cha Nne| Pre Necta| 28 Apr 18

Mtihani wa Kiswahili Kidato cha Nne| Pre Necta| 28 Apr 18

Sehemu A

Ufahamu (alama 10)

1. Soma habari ifuatayo kisha jibu maswali yanayofuata:
BAADA ya kusikia simulizi mbalimbali kuhusiana na ‘chuma ulete’  kwa muda mrefu, nikaamua nijaribu ili niweze kurahisisha maisha. Nilitamani sana zile hadithi za ‘chuma ulete’ ziwe kweli juu yangu. Ninunue bidhaa kisha fedha zinirudie, zikiwa nyingi zaidi. Nile bila jasho.
Baada ya mawazo hayo, siku chache zilizopita nikaamua kwenda kwa mganga mmoja wilayani Bagamoyo ambaye alisifika sana kwa kutengeneza utaalamu huo.
Nilifika kwa mganga, nikavua viatu kisha nikaingia ndani. Kama kawaida mganga alinikaribisha kwa mapambio ya ‘kilozi’. Zilipigwa chafya nyingi zilizosindikiza maneno yasioeleweka.
Kabla sijamweleza shida iliyonipeleka pale, mganga akaanza kubashiri: “Kijana una matatizo makubwa, mambo yako hayaendi kuna watu wanakuchezea… umekuja kumtambua anayekufanya ushindwe kupiga hatua… “
Mganga mtaalamu mlozi aliendelea kuongea mambo mengi ambayo sikuhusiana nayo, nilipoona anazidi kupotea, nikamweleza shida iliyonipeleka: “Mzee nimekuja kwa shida moja tu, nataka unipe uchawi wa chuma ulete, nipate pesa bila jasho.”
Mtaalamu alicheka sana, kabla hajatoa tiba akaniomba niweke shilingi laki mbili ndani ya bakuli kubwa lililokuwa umbali mdogo kutoka usawa wa mapaja yake. Nilitembea na fedha ya kutosha, nikaweka kiwango alichotaka.
Alifurahi alipokiona kitita cha fedha, akatamka maneno ambayo sikuyaelewa, kisha akachukua kitu mfano wa kunde, akakimeza.  Akajitikisa kidogo akakitapika, akachukua kipande cha mti, akanuia maneno fulani, baadaye akatoa kitambaa chekundu kilichokuwa na unga mweupe. Alipomaliza hayo, akachanganya vitu vyote katika kitambaa chekundu, akakifunga vizuri na kukishona kwa sindano ya mkono.
“Chukua dawa yako!” alinikabidhi kwa sauti ya kukoroma, “dawa hii nakupa, ukienda dukani, ukitoa noti ya shilingi elfu kumi, mwenye duka atakurudishia elfu ishirini, ukitoa elfu tano, utarudishiwa elfu kumi, pia baada ya muda, fedha zake zitaanza kuhamia kwako. Nenda kijana.”
Niliagana na mganga nikiwa na furaha ya kutoka kimaisha. Nilifika nyumbani usiku, nikalala nikiwa na shauku ya kuanza mkakati wa utajiri asubuhi.
Asubuhi ilifika, nikaenda dukani nikiwa na noti ya shilingi elfu kumi. Nikanunua vocha ya elfu mbili. Nilitegemea mwenye duka angenirudishia elfu ishirini kama nilivyoelezwa na mganga. Haikuwa hivyo, nilipewa fedha kamili, elfu nane!
Nilijaribu duka jingine bila mafanikio. Hakuna fedha iliyozidi. Nikachoka, nikarudi nyumbani kulala.
Mpaka sasa nimejaribu kununua vitu katika maduka mengi bila kile nilichoahidiwa na mganga kutokea. Na sasa nimeamini kuwa nilitapeliwa na siamini tena kama kuna kitu kinaitwa ‘chuma ulete.’ Huu ni uongo tu! Mjinga mimi, mganga kala laki mbili yangu bure!

Maswali

(a) Kichwa cha habari hii kinachofaa ni kipi?
(b) Ungemshauri nini msimuliaji wa mkasa huu?
(c) Kwa mujibu wa habari hii, eleza maana ya ‘chuma ulete’.
(d) Taja sababu mbili zinazowafanya watu wapende kupata mafanikio kwa njia za haraka.
2. Andika ufupisho wa aya mbili za mwisho za habari uliyoisoma kwa maneno hamsini (50) .

SEHEMU B (alama 25)

SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA

3. Viambishi awali na viambishi tamati vina uwezo wa kubadili umbo na maana ya neno. Katika maneno yafuatayo eleza dhima ya kila kiambishi.
(a) Watakapotupambanisha.
(b) Sielekezi.
4. Eleza njia zilizotumika kuunda misamiati ifuatayo katika lugha ya Kiswahili.
(a) Sigara.
(b) Mwanajeshi.
(c) Kipima pembe.
(d) Pembe tatu.
(e) Mtutu.

SEHEMU C (alama 10)

UANDISHI

5. Manyanda akiwa mfanyakazi wa kiwanda cha korosho Tanita alipewa taarifa kuhusu ugonjwa wa baba yake. Wewe kama Manyanda andika barua ya kuomba ruhusa. Anuani ya kiwanda ni S.L.P.1030, Kibaha.

SEHEMU D (alama 10)

MAENDELEO YA KISWAHILI

6. Eleza jinsi shughuli za Waarabu zilivyosaidia kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili nchini Tanzania kabla ya uhuru.

SEHEMU E (alama 45)

Jibu maswali matatu katika sehemu hii. Swali la 10 ni la lazima.
FASIHI KWA UJUMLA
7. “Mshairi ni mhakiki wa jamii”. Kwa kutumia vitabu teule viwili (2) vya ushairi ulivyosoma, jadili kauli hii.
8. “Jina la kitabu ni kivutio cha wasomaji wa riwaya”. Kwa kutumia riwaya teule mbili (2) ulizosoma linganisha majina ya vitabu jinsi yanavyosadifu yaliyomo.
9. “Waandishi wengi huandika kazi zao kwa lengo la kutoa ujumbe katika jamii”. Kwa kutumia tamthiliya mbili (2) zilizoorodheshwa, thibitisha ukweli wa kauli hii.
10. “Tenzi zina kanuni maalumu”. Tunga utenzi wenye beti tatu (3) unaohusu ugonjwa wa UKIMWI.
Mwisho
Endapo unataka kufanya mtihani huu ili usahihishwe na Mwalimu Makoba, zingatia mambo haya:
 Mtu yeyote na kokote aliko anaruhusiwa kufanya mtihani huu.

Fanya mtihani huu kwa kutumia aina yoyote ya karatasi.

Ukimaliza, piga picha karatasi hizo kisha zitume WhatsApp kwenye namba ya Mwalimu Makoba, 0754 89 53 21.

Subiri mtihani wako usahihishwe, Urudishiwe na ufanyiwe masahihisho.

Gharama ya mtihani huu ni shilingi 2,000 (elfu mbili) tu.

Namba za malipo ni: M – Pesa 0754 89 53 21 na Tigo pesa 0653 25 05 66

“Kwa kuwa lengo la mtihani huu ni kutaka kujua uwezo na mapungufu ya mwanafunzi ili aweze kupewa mbinu mbadala za kumsaidia kufaulu mtihani wake wa mwisho, kuangalizia majibu hakuna faida yoyote kwani lengo la mtihani si kubaini nani atakuwa wa kwanza na yupi atakuwa wa mwisho!”

Mwalimu Makoba| Mwalimu wa Waalimu na Wanafunzi| Mwalimu wa Ushindi!

Unataka kufanya mtihani huu na hujaelewa taratibu zake? Wasiliana na Mwalimu Makoba kwa 0754 89 53 21.

Mwalimu Makoba

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie