Mtihani wa Kiswahili 1 Kidato cha Sita| Pre necta| Dec 2017

Mtihani wa Kiswahili 1 Kidato cha Sita| Pre necta| Dec 2017


Muda: saa 3

Maelekezo

1.   Mtihani huu una maswali saba katika sehemu A, B, C, D na E.
2.   Jibu maswali yote.

JINSI YA KUUFANYA MTIHANI HUU

Mtu yeyote na kokote aliko anaruhusiwa kufanya mtihani huu.
Fanya mtihani huu kwa kutumia aina yoyote ya karatasi.

Ukimaliza, piga picha karatasi hizo kisha zitume WhatsApp kwenye namba ya Mwalimu Makoba - 0754 89 53 21.

Subiri mtihani wako usahihishwe. Urudishiwe na ufanyiwe masahihisho.

Gharama ya mtihani huu ni shilingi 2,000 tu.

Namba za malipo ni: M – Pesa 0754 89 53 21 na Tigo pesa 0653 25 05 66

“Kwa kuwa lengo la mtihani huu ni kutaka kujua uwezo na mapungufu ya mwanafunzi ili aweze kupewa mbinu mbadala za kumsaidia kufaulu mtihani wake wa mwisho, kuangalizia majibu hakuna faida yoyote kwani lengo la mtihani si kubaini nani atakuwa wa kwanza na yupi atakuwa wa mwisho!”
Daud Makoba – Mwalimu Makoba – Mwalimu wa Waalimu.

Unataka kufanya mtihani huu na hujaelewa taratibu zake? Wasiliana na Mwalimu Makoba kwa 0754 89 53 21.

Sasa fanya mtihani wako.

SEHEMU A (Alama 20)

UFAHAMU

1.   Soma kwa makini kifungu hiki cha habari kisha jibu maswali yanayofuata.
UTUPU ni hali ya kutokuwa na kitu. Huenda ukawa utupu wa pochi, chumba, mali, akili na hata utupu wa mwili. Wahenga wa zamani (sio hawa wa mitandaoni), waliupuuza utupu kwa kusema, Mkono mtupu haurambwi.
Hali ya utupu hivi sasa inazidi kubadilika kwa kasi. Utupu umegeuka kitu. Utupu unategemewa kumvusha mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Tazama nyimbo za wanamuziki zilivyo. Wasichana wanaotumika humo  wanacheza utupu kabisa. Hawaogopi lolote na hata aibu hawaoni.
Zamani wazee walipotaka kumwaga laana, walitishia kuwaonesha watoto wakorofi utupu. Enzi hizo kuonekana kwa utupu ilikuwa ni laana kubwa. Wapo ambao walichanganyikiwa na kuwa wehu kwa sababu ya kadhia hii.
Vibinti vya zama hizi vinapiga picha za utupu bila kuogopa chochote. Ukiviuliza kwa nini vinafanya hivyo, utasikia vinajibu kuwa vinapenda kuwa hivyo… vinapenda kukaa utupu. Ujinga mtupu.
Hali ya mabinti kukaa utupu kwa kiasi kikubwa imepunguza hamu ya vijana kuoa. Ndio, vijana wanaona kila kitu. Sasa aoe ili aone nini kingine.
Maadili yamebadilika sana sasa. Ni kweli kuwa hapo zamani mwanadamu alitembea utupu. Lakini tamaduni hubadilika kulingana na wakati. Mwanadamu tangu kupata ustaarabu wake, utupu si jambo la kuonyesha hadharani.
Bado ninaendelea kutafakari nguvu hii ya utupu kukamata hisia za watu imetoka wapi? Ni kweli wanaowachezesha mabinti wakiwa watupu namna ile watafurahi wakiwaona watoto wa kuwazaa wao wakifanya vile? Lazima sasa turejee katika maadili. Heshima iwepo.
Jamaa mmoja aliwahi kunieleza kuwa, utupu kuzidi kuonekana mara kwa mara kumemwaga laaana kali katika jamii. Ndiyo maana kila kukicha limeibuka lile, mara limetokea hili.
Sina uhakika kama kuna sheria inayoeleza lolote kuhusu mavazi. Ni wakati wa kulitafakari hili kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Ni utupu wa fikra kuamini kuwa utupu unaweza kukupatia mafanikio. Sana utaambulia, kupata umaarufu wa mpito.

Maswali

a.   Toa maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika habari uliyoisoma.
i.             Wahenga.
ii.            Laana.
iii.           Sheria.
iv.          Zama.
v.           Tamaduni.
b.   Mwandishi ana maana gani anaposema “waliupuuza utupu kwa kusema, Mkono mtupu haurambwi.”
c.   Unaelewa nini kuhusu mabinti wa zama hizi? Toa maelezo kwa mistari isiyozidi mitatu.
d.   Kwa kutumia aya ya tatu, mwandishi ana mtazamo gani kuhusu wanamuziki.
2.   Fupisha habari uliyoisoma kwa maneno 100.

SEHEMU B (alama 20)

SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA

3.   Katika tungo zifuatazo taja kielezi na fafanua aina ya kielezi hicho.
i.             Hospitali imefungwa kwa mara ya saba.
ii.            Amekaa juu ya ndoo.
iii.           Anapigana kishujaa.
iv.          Nitaondoka asubuhi na mapema.
v.           Mwanenu ameelekea upande wa kushoto.
4.   Ni kwa vipi lugha ya Kiswahili inafaidishwa na rejesta? Toa hoja tano.

SEHEMU C (alama 20)UTUNGAJI

5.   Jifanye wewe ni meneja wa kiwanda cha kufyatua matofali S.L.P 700 Kigoma, andika barua ya kumpa ruhusa ya siku tatu mfanyakazi wako aitwaye Kitalula Abubakari S.L.P 1223 Kigoma. Jina lako liwe Chimatu Baraka.

SEHEMU D (alama 20)MAENDELEO YA KISWAHILI

6.   Lahaja ya Kiunguja ilikidhi vigezo fulani hata ikasanifishwa kuwa Kiswahili tukionacho leo. Ni masharti yapi yalifikiwa na lahaja hii hata ikaweza kupitishwa? Toa hoja tano.

SEHEMU E (alama 20)TAFSIRI NA UKALIMANI


7.   Tafsiri na ukalimani ni dhana ambazo zimekuwa zikichanganywa mno na watu. Tumia maarifa uliyoyapata katika kozi hii, kuondoa utata huo. Toa hoja nne.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu