Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne

Jinsi ya Kuandika Risala| Kiswahili Kidato Cha Tatu na NneRisala ni hotuba fupi iliyokatika maandishi na ambayo husomwa mbele ya mgeni rasmi ikielezea kuhusu mafanikio, changamoto na maombi ya kundi fulani.

Muundo wa Risala

-      Utangulizi. Katika kipengele hiki, cheo cha kiongozi (mgeni rasmi) hutajwa. Pia kundi linalowakilishwa.
-      Kiini. Mafanikio ya kundi, changamoto za kundi, mapendekezo na ushauri.
-      Hitimisho. Kipengele hiki hukaa shukrani.
Sasa hebu tazama mfano huu wa risala:
Swali; Jifanye wewe ni mwanafunzi wa kidato cha nne na umechaguliwa kuandaa risala itakayosomwa mbele ya mgeni rasmi siku ya mahafali yako ya kumaliza kidato cha nne. Andika risala utakayoisoma siku hiyo.

RISALA YA WANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE KWA MGENI RASMI
Ndugu mgeni rasmi, waalimu, wazazi, wanafunzi wenzetu, wageni waalikwa mabibi na mabwana.
Ndugu mgeni rasmi, tunayofuraha kukualika leo hii katika sherehe yetu ya mahafari haya ya kidato cha nne ili usherehekee pamoja nasi na zaidi uweze kusikia mafanikio yetu pamoja na changamoto zinazotukabili.
Ndugu mgeni rasmi, awali ya yote tunapenda kutoa shukrani kwa uongozi mzima wa shule yetu kwani wamekuwa wazazi bora waliotuongoza katika misingi imara ambayo itatusaidia sana hata baada ya kuwa tumemaliza elimu yetu.
Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 60, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo maradhi, utoro na ukosefu wa fedha, tumebaki wanafunzi 40. Wavulana wakiwa 15 na wasichana 25.
Ndugu mgeni rasmi, miongoni mwa mafanikio tuliyonayo katika shule yetu ni umiliki wa mradi wa miti ya matunda. Mradi huu umetusaidia sana sisi wanafunzi kuweza kupata matunda katika kila mlo tuupatao na hivyo kuwa na afya bora.
Ndugu mgeni rasmi, mafanikio mengine ni uwezo wetu mkubwa kitaaluma. Ni kweli kuwa, uwepo wa waalimu bora ndiyo umekuwa sababu ya shule yetu kushika nafasi ya kwanza katika mitihani yote ya kujipima tunayofanya na shule za mkoa wetu. Ukiachilia mbali kuwa wa kwanza, tumepata maarifa stahiki ambayo tulipaswa kuwa nayo na tunatumaini yatatusaidia sana katika kupambana na changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii yetu.
Ndugu mgeni rasmi, mbali na mafanikio hayo, kuna changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikitusumbua. Miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa vitabu vya kutosha. Tatizo hili limetufanya tusome kwa shida kwani kitabu kimoja kinachangiwa na wanafunzi saba.
Ndugu mgeni rasmi, tatizo jingine ni uhaba wa vifaa vya maabara. Uhaba huu unapelekea wanafunzi wengi kushindwa kuisoma sayansi kwa vitendo na badala yake tunaisoma kwa nadharia tu.
Ndugu mgeni rasmi, tunatumaini mafanikio yetu na changamoto zetu umezisikia na utatusaidia kadri ya uwezo wako ili shule yetu iendelee kuwa sehemu salama ya kujipatia elimu. Pia, tunakushukuru kwa kufika mahali hapa, kwani pamoja na kuwa ulitingwa na shughuli zako za muhimu, lakini, umeweza kupata muda wa kujumuika nasi. Asante na karibu sana.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu