Usipofanya Mambo Haya Utajifungua kwa Upasuaji
Idadi ya wanawake wanaojifungua
kwa njia ya upasuaji imekuwa ikongezeka siku hadi siku. Njia hii huchukuliwa
kama maamuzi ya mwisho ya kuhakikisha mama anajifungua salama. Ipo hatari kubwa
kujifungua kwa njia ya upasuaji, wote, mama na mtoto hukumbwa na hatari hii.
Tafiti zilizofanyika hivi
karibuni zimeeleza sababu mojawapo inayopelekea wanawake kujifungua kwa upasuaji ni uzito kupita kiasi. Uzito kupita kiasi mara nyingi ni matokeo ya
mitindo ya maisha ya mwanamke mwenyewe. Mitindo hii ni pamoja na kuepuka
kufanya mazoezi na kushindwa kabisa kujizuia ulaji wa vyakula vyenye wingi wa
mafuta na sukari.
Nini Kifanyike Kumwepusha Mwanamke Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji?
Jambo kubwa la msingi ni
kuhakikisha mwanamke hana uzito kupita kiasi. Njia mojawapo inayotumika kupima
kama una uzito kupita kiasi ni kipimo cha BMI. Endapo utakutwa na uzito kupita
kiasi, basi ni vyema ukaanza mazoezi mapema ili kukwepusha na madhara
yatakayokupata hapo baadaye.
Njia sahihi ya kupunguza uzito ni
mazoezi ya viungo kama kukimbia, kuruka kamba na mazoezi mengine mepesi.
Kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30 kwa siku kunatosha kabisa kukufanya
mwenye afya njema.
Baada ya kuanza ratiba ya ufanyaji
wa mazoezi, jambo linalofuata ni kuepuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi
na sukari. Hapo utajihakikishia kuwa na mwili bora na imara.
Pia, ili kumwepusha mama mjamzito
kujifungua kwa njia ya upasuaji ni kuhakikisha anahudhuria ‘kliniki’ ili aweze
kupewa msaada wa kiafya na endapo atakutwa na dalili zozote za hatari aweze
kusaidiwa.
Hata hivyo kumeibuka imani potofu
kwa baadhi ya wanawake kulazimisha wajifungue kwa njia ya upasuaji hata pale
wanapokuwa hawana tatizo lolote. Sababu kubwa inayopelekea hali hii, ni kudhani
kuwa endapo watajifungua kwa njia ya kawaida, viungo vyao vya uzazi
vitaongezeka ukubwa na kuwafanya wapoteze mvuto katika tendo la ndoa. Imani hii
ni finyu na haipaswi kuaminika kwani haina ukweli wowote zaidi ya kumuumiza
mwanamke mwenyewe.