Riwaya| Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (24)

Riwaya| Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (24)

Wakati naendelea kushangaa, alinipiga na yale manyoya ya bundi utosini. Nikapoteza fahamu.
Niligutuka nikiwa katikati ya msitu mnene. Ilikuwa asubuhi. Kabla sijafanya lolote, nikasikia sauti kali, “Upo katika nchi ya Matumbawe!” niliitambua sauti ile. Ilikuwa sauti ya Mzee. Sauti iliyojaa kitetemeshi!
Matumbawe yaliyosemwa sikuyaona. Niliona msitu mnene hata nikahofia kama nitapata njia ya kupita. Nilijizoa taratibu nikasimama. Nikawaza nielekee wapi, nikaamua kuelekea mashariki.
Sikujua nilikokwenda, ila nilitambua kilichonifikisha hapo ni msako wa mjuu wa Mzee Samike, Chimota. Nilitembea hovyo kama nyumbu aliyeridhika na unyumbu wake katika msitu wa ujinga. Hakukuwa na njia, maana yake ni kwamba, mahali hapo hakuwahi kupita mwanadamu.
Nilitembea kwa mwendo mrefu, jua lilikuwa kali lakini halikunichoma kwa sababu ya wingi wa miti. Muda wote nilikuwa chini ya kivuli nikivuta hewa safi katika nchi hii ya Matumbawe.
Safari yangu ilichukua masaa mengi hata jua likazama na kuifanya dunia ipoteze nuru. Hapo nikawaza nitawezaje kuwa katika msitu mnene peke yangu? Vipi kama nitapatwa na madhara? Vipi nikishambuliwa na wanyama wakali. Sikupata jibu na sikuwa na namna nyingine isipokuwa kulala chini ya miti ili kukikucha niendelee na safari. Nilikuwa mpweke nikijipa moyo kuwa Samike angenisaidia muda wowote nitakapopatwa na tatizo.

Kuna jambo lilinishangaza, japo nilitembea kwa zaidi ya masaa 12, sikuhisi njaa, sikuhisi kiu, tumbo langu lilikuwa limejaa vyema. Nilishangazwa na uwezo huu mpya.
Nilikaa chini ya mti mkubwa. Giza lilikwisha tanda nami sikuwa na uwezo wa kuendelea na safari. Kitendo cha kukaa, kiliamsha jambo jingine. Usingizi mnono ulinivamia nikalala bila kuota.
Niliamshwa asubuhi na ndege mmoja mdogo mwenye mseto wa manyoya mekundu na meupe. Alinidonoa donoa miguu mpaka nikaamka. Nilimtazama rafiki huyu mpya nikitabasamu. Naye alijibu kwa kupiga kelele za furaha, “Jiuuuh! Jiuuuuh! Jiuuuuh!”
Sikuwa na muda wa kupoteza, nilifuta vumbi suruali yangu ambayo hapo zamani katika upya wake ilikuwa nyeupe, lakini sasa haikuwa na rangi iliyoeleweka kutokana na kuvaliwa mara kwa mara.
Nilitembea mwendo wa kawaida kwa sababu nilikokwenda sikupajua na sikuwa na haraka. Kuna wakati mbele yangu niliona simba, nikabadili njia ili nisigeuzwe kitoweo. Nikaendelea kutembea kwa kujiamini kama nilikuwa mmiliki wa msitu ule na vyote vilivyomo.
Huku nikiendelea kutembea, ndege mdogo aliyeniamsha aliruka juu akinifuata. Nadhani kwa sababu ya umri wake mdogo hakuijua siri ya dunia kuwa maisha yamejaa uhasama na kuwindana. Masikini alidhani kila kiumbe ni rafiki. Hata hivyo alikuwa katika mikono salama. Mimi nilitembea, yeye akapaa juu yangu.

Wakati nikiendelea kutembea, nilisikia ngurumo mbele yangu. Hata yule ndege aliogopa akaruka mbali  nisiweze kumwona. Ngurumo zile zilikatika, nikaona kitu cha kuogofya.
Lilisimama joka kubwa sana mbele yangu. Niligeuka nyuma haraka ili nikimbie, nyuma yangu napo palisimama joka kubwa kama lile la mbele. Nikajaribu kupenya kushoto, njia haiupitika, palikuwa na mti mkubwa wa mbuyu. Kulia nako vivyo hivyo, hapakupitika kwa sababu ya mti mnene uliojaa miba  mikali.
Basi nikawa nimesimama katikati ya majoka yale makubwa yaliyojaa hasira nisiyejua la kufanya.
Wakati nikiendelea kushangaa kwa hofu, joka la mbele lilifungua kinywa chake likatema moto. Joka la nyuma nalo likajibu mashambulizi. Sikuwa na ujanja tena. Nikakaa chini kusubiri hukumu yangu. Nilikiona kifo kibaya kabisa kikininyemelea, kifo cha kumezwa na majoka mawili yanayotema moto!
Itaendelea Jumapili…
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21

Shusha maoni yako mdau!

TAZAMA POVU LA MWALIMU MAKOBA KWA WASANII WAVAA HOVYO...

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne