Riwaya| Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (23)
Wimbi lile lilituzoa na
kutupeperusha juujuu kabla halijatushusha na kutufanya tupige ukelele wa
katikati ya hofu na mashaka. Ukelele wetu ulikatwa na sauti kali iliyotuamuru
tunyooshe mikono juu. Aliyesema hayo alisimama upande wa kulia, ndipo
tulipogundua tulikuwa karibu na meli kubwa ya mizigo iliyokuwa ikienda nchini
kwetu.
Tulitii amri tukanyoosha mikono
juu kama mateka wa kivita. Kamba kubwa ikarushwa na kuunasa mtumbwi wetu na
kuanza kuvutwa kuelekea iliko meli. Tulifika karibu na meli hiyo tukapatiwa
ngazi huku tukiamriwa tupande juu. Tulipanda bila kupinga.
Tulipofika juu mimi na mzee,
tulishuhudia watu wengi ambao walibeba silaha za moto. Bila shaka watu hawa
walikuwa ni askari binafsi waliofanya kazi ya kulinda meli dhidi ya maharamia.
Nilimnong’oneza mzee, “Mzee tumefananishwa na maharamia!” naye akazungumza na
watu wale kwa sauti:
“We are not Somalis,” nilishangaa
kumsikia mzee akibonga Kiingereza.
Niliweza kuwatambua walinzi wale
kuwa ni raia wa Marekani kutokana na bendera zilizokaa juu ya mikono ya magwanda yao. Hawakujishughulisha
na kumjibu mzee, bali kijana mmoja alitusogelea na kutukagua kama tulibeba
siraha yoyote. Hakupata alichokitafuta.
“They are not!” alisikika kijana
aliyetukagua akiwaambia wenzake. Walipojiridhisha wakatuamuru tushuke chini
mpaka kwenye mtumbwi ili twende zetu.
Tulifika chini ya mtumbwi tukakaa
taratibu tayari kwa kupiga kasia. Mzee hakuwaacha salama, akapasua yai kwa
sauti kuu, “Hey fuc*, ur lucky today im in a good mood, if not I was going to
destroy this fuc*ed ship with my own hand.” Hawakuyajali maneno ya mzee wala
kutetemeshwa naye, waliendelea na hamsini zao nasi tukaendelea na sabini zetu.
XX XX XX
Niliishi na mzee kwa amani na
furaha. Taratibu akaanza kunifundisha fani mpya. Haukuwa ulozi, ila
alinifundisha fani ya kupambana na walozi. Tulitumia muda wetu kwa kuvua samaki
na kufundishana fani hii. Kila mahali palikuwa ni darasa. Tulipokuwa baharini
katika kina kirefu alinifundisha mengi hata nikawa na uwezo wa kuwaita samaki
niwatakao wakanifuata. Somo hili lilinifanya niigundue siri ya mzee kuvua bila
nyavu.
Ni kweli katika mtumbwi tulikuwa
tukiondoka na nyavu, lakini hatukuwahi kuzishusha kamwe. Mzee alinionya
niitunze siri hii. Akanieleza siri hii ndiyo humanya apende kuvua katika eneo
la peke yake ambako wavuvi wenzake huwa hawafiki. Eneo alilopenda kuvua mzee
ndipo zilipopita zile meli kubwa kubwa za mizigo zilizojaa walinzi tele.
Tulipokuwa nchi kavu
alinifundisha aina za miti na matumizi yake. Hakuisha kuniambia aina hii ya mti
inatibu hiki, hii inatibu kile. Wakati mwingine akisisitiza, ukitaka mchawi
asiingie kwako, weka mzizi wa mti wa mzaituni pembezoni mwa chumba, hataweza.
Basi nilipewa elimu ninayoizungumza hapa na nyingine ambayo sitaweza kuisema.
Yote hii alifanya kuniandaa kwa mapambano makali ambayo bila shaka yalikuwa
karibuni kuanza.
Siku moja usiku saa nne, nikiwa nimekaa
na mzee pembezoni mwa kijinga cha moto tukipiga soga za maisha. Alitua bundi
mkubwa mkononi kwa mzee. Mzee alimtoa manyoya ya kichwa kisha akamwacha aende
zake.
“Wakati umefika Mako!” alisema
akinikazia jicho. Nilibaki nikimtazama nikiwa sielewi ni wakati gani hasa mzee
alimaanisha.
“Wakati wa kumkomboa mkombozi
umefika Mako!” aliendelea kuzungumza akizidi kunichanganya kabisa.
“Mako! Itakapofika saa nane na
nusu usiku, utasafiri kwenda nchi ya Matumbawe kumtafuta Chimota.” Mzee
alisema, nikayaona macho yake yaking’aa isivyokawaida. Niliogopa kwa sababu
nilikuwa bado sijafanya maandalizi ya kupambana na wachawi waliobobea, katika
eneo ambalo hata sikulifahamu.
Itaendelea Jumapili…
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21
Shusha maoni yako mdau!