Nadharia ya Fasihi | Fasihi Simulizi

Fasihi Simulizi

Kwa kuwa fasihi simulizi ni dhana pana, wataalamu wengi wameeleza maana yake:
Fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake. (Matteu; 1983).
Fasihi simulizi ni masimulizi tunayopokea mdomo kwa mdomo, si masimulizi yaliyoandikwa tangu awali, kwa ajili hii basi, tutaona kuwa katika fasihi simulizi mna utumiaji wa ulumbi. (Kirumbi; 1975).
Kwa ujumla, fasihi simulizi ni fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya masimulizi yatumiayo mdomo.

Vipera vya Fasihi Simulizi

i.             Hadithi
ii.            Ushairi
iii.           Semi
iv.          Sanaa za maonyesho

1.   Hadithi

Hadithi ni tungo za fasihi za masimulizi zitumiazo lugha ya nathari.

Hadithi ina tanzu zifuatazo:
i.             Ngano
ii.            Tarihi/ visakale
iii.           Visasili
iv.          Vigano
v.           Soga

Ngano

Ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kueleza au kuonya kuhusu maisha. (Masebo & Nyangwine; 2007).

Tarihi/ Visakale

Ni hadithi ambazo husimulia kuhusu matukio ya kale. Matukio haya huenda yakawa ya kweli au ya kibunifu.

Visasili

Ni hadithi ambazo husimulia kuhusu asili ya vitu fulani. Kwa mfano, asili ya fisi kuwa na miguu mifupi ya nyuma, asili ya mbuzi kuwa na mkia mfupi… n.k

Vigano

Ni hadithi zinazoeleza makosa au uovu wa watu ili kusaidia kurejesha maadili yaliyopotea. Nahau na methali hutumiwa na vigano kama nyenzo ya kuufikisha ujumbe huo.

Soga

Ni hadithi ambazo hueleza mambo kwa njia ya ucheshi.

2.   Ushairi

Ushairi ni fungu linalojumuisha tungo zote zenye kutumia mapigo kwa utaratibu maalum.

Vipera vya Ushairi

-      Mashairi
-      Nyimbo
-      Ngonjera
Mashairi ni mtungo wa kisanaa wenye mpangilio maalumu wa lugha ya mkato, unaoelezea hisia kwa kufuata na kuheshimu utaratibu wa urari na muwala maalumu.
Nyimbo ni tungo zenye mahadhi ya kupanda na kushuka kwa sauti.
Ngonjera ni mashairi ya kujibishana baina ya watu wawili.

3.   Semi

Semi ni fungu la tungo la fasihi simulizi ambazo ni fupi fupi zenye kutumia picha, tamathali za semi na ishara.
Vipera vya semi ni;

Methali

Methali ni usemi wa kisanii wa kimapokeo unaofikiriwa na jamii kuwa kweli na unaotumiwa kufumbia au kupigia mfano na huwa umebeba maana pana kuliko maneno yenyewe yanayotumiwa k.m. ‘hasira za mkizi furaha ya mvuvi.’ (TUKI; 2010).

Misemo

Ni fungu au mafungu ya maneno ambayo hutumiwa na jamii ya watu kwa namna maalumu ili kutoa mafunzo. Kwa mfano, ‘Mpaji ni Mungu.’

Nahau

Ni fungu la maneno lenye maana maalumu isiyotokana na maana za kawaida za maneno hayo. Kwa mfano, ‘Tia chumvi.’

Vitendawili

Ni maneno yanayoficha maana ya kitu isijulikane kwa urahisi.

4.   Sanaa za maonyesho


Sanaa za maonyesho zinajumuisha: Michezo, majigambo, ngoma, miviga, michezo ya watoto, ngojera  na vichekesho.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne