Mtihani wa Kiswahili Kidato cha Nne | Oktoba 08 2017

pastpaper za kiswahili kidato cha nne

Maelekezo ya mtihani huu

i. Jibu maswali yote.
ii. Usifanye udanganyifu katika mtihani huu. Lengo la mtihani siyo kuuona uwezo wako wa kupata A, bali kutambua kipi kinachokusumbua katika somo hili ili uweze kusaidiwa.

Jinsi ya kufanya mtihani huu wa online na usahihishaji wake

i.  Andika majibu yako katika karatasi yoyote utakayoona inafaa kujibia.

ii. Ukimaliza kufanya mtihani, piga picha majibu yako katika karatasi zote ulizotumia kisha tuma picha hizo kwa njia ya WhatsApp kwenda namba 0754895321 ili ziweze kusahihishwa.
iii.  Karatasi zitakazosahihishwa ni zile zitakazokuwa zimelipiwa kiasi cha
shilingi 1,000 (elfu moja). Namba za malipo ni MPESA 0754 89 53 21 na TIGO PESA 0653 25 05 66. Hata hivyo kama huna uwezo kabisa wa kulipia gharama hiyo, unashauriwa ufanye mtihani huu kisha umpatie mwalimu yeyote aliyekaribu nawe asahihishe kazi yako. Kwa kuwa kiwango cha malipo ni kidogo sana, ni vizuri zaidi kama utasahihishwa na timu yetu.
iv.  Kwa kuwa lengo la mtihani huu ni kubaini matatizo yanayomsumbua mwanafunzi katika somo hili ili tuweze kuyaondoa mapema na kumsaidia mwanafunzi husika kufaulu na kupata maarifa stahiki, suala la muda halijazingatiwa, hivyo unaweza ukafanya kwa wakati wowote utakavyoona inafaa.

SASA FANYA MTIHANI WAKO: KUMBUKA KUJIBU MASWALI YOTE

SEHEMU A (Alama 10)

UFAHAMU

1. Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yatakayofuata:
Saa mbili asubuhi Wananchi wote tulikusanyika kwenye kibaraza cha mfalme kama ilivyoamriwa. Mfalme akiwa amevalia joho jeupe alisimama akasema,
          “Leo viongozi hatujalala, matatizo yaliyotokea jana yalitufanya tukeshe tukijadili mwafaka wa Dunia bila mwezi. Kijitu kilichouiba mwezi kinatoka Dunia nyingine iitwayo Vumu iliyo katika mfumo wa jua lingine. Inasemekana katika sayari yao hiyo, mwezi wao ulizimika ghafla wakati watoto waliotumwa kwenda kuusafisha walipozidisha kiasi cha mafuta. Vijitu hivi vinamaarifa mengi sana lakini havijui kitu katika elimu ya kuukarabati mwezi, hivyo suluhisho lao lilikuwa kuiba mwezi mwingine. Sasa basi anatakiwa atumwe mtu kwenda katika sayari ya Vumu kuurejesha mwezi wetu. Hatutaki uhasama wala vita tena katika nchi hii… hivyo atakayekwenda huko aende kutatua matatizo kwa njia ya Amani.” Mfalme alikohoa kidogo kisha akaendelea kuzungumza kwa sauti kubwa zaidi,
          “Kama mjuavyo chombo chetu cha masafa ya mbali huwa hakiwezi kupandwa na mtu mzima ila mtoto mdogo tu kwa sababu ya nguvu ya mvutano ya Dunia, hivyo anatakiwa apatikane mtoto mdogo asiyezidi miaka 15 na asiyepungua miaka minane…”
Kabla mfalme hajaendelea kuzungumza, nilipaaza sauti huku nikisogea mahala aliposimama,
          “Mimi Nkenye, nitakwenda Vumu kuusaka mwezi, nina umri wa miaka tisa, nimekuwa nikifanya kazi ya kuusafisha mwezi pale unapochafuka na kutoa mwanga hafifu, pia mimi ni mtoto wa shujaa Mako aliyemwangamiza mfalme wa vichawi vya anga kwa kipande cha sindano butu!”
a.   Kipi kinafaa kuwa kichwa cha habari uliyosoma?
b.   Unadhani hadithi hii ina ukweli wowote? Eleza.
c.   Ni ipi sababu ya chombo cha masafa ya mbali kupandwa na mtoto mdogo?
d.   “Shujaa Mako aliyemwangamiza mfalme wa vichawi vya anga kwa kipande cha sindano butu!” Usemi huu una maana gani?
2. Andika ufupisho wa hadithi hiyo kwa maneno yasiyozidi 60.

SEHEMU B (Alama 25)

SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA

3. Taja tofauti mbili kati ya mofimu huru na mofimu tegemezi.
4. Eleza maana ya vidahizo vifuatavyo kisha tunga sentensi moja kwa kila kidahizo: Chapuo, Funganyumba, Ghariki, Harabu, Kifuku.

SEHEMU C (Alama 10)

UANDISHI

5. Andika insha yenye maneno 250 kuhusu mada isemayo: ELIMU YA MSINGI INA UMUHIMU WAKE KATIKA JAMII.

SEHEMU D (Alama 10)

MAENDELEO YA KISWAHILI

6. Huku ukitoa mifano ya kutosha, fafanua mchango wa Waarabu katika kukuza lugha ya Kiswahili.

SEHEMU E (Alama 45)

FASIHI KWA UJUMLA

7. Jadili jinsi washairi walivyoishauri jamii yao.
8. Mandhari ni kitu pekee ambacho humsaidia mwandishi wa riwaya kuweza kueleza yalikofanyika matukio ya kazi yake. Tumia riwaya mbili kujadili mandhari yalivyotumiwa na mwandishi.
9. Kuna wakati waandishi wa tamthiliya hufaulu wakapongezwa. Na kuna kipindi hushindwa wakakosolewa. Jadili kufaulu na kutofaulu kwa waandishi wawili wa tamthiliya uliowasoma.
10. Tunga ngonjera yenye beti nne kuhusu umuhimu wa kumsomesha mwanamke.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1