Jinsi ya Kuandika Hotuba
Hotuba ni maelezo ambayo hutolewa
na mtu mbele ya watu kuhusu mada fulani.
MUUNDO WA HOTUBA
-
Mwanzo.
Huu huambatana na salamu.
-
Utangulizi.
Hutaja watu na kuwatambulisha kulingana na vyeo vyao.
-
Kati.
Hiki ni kiini cha hotuba. Mawazo yote makuu hukaa hapa.
-
Mwisho.
Muhtasari wa yale yaliyoelezwa. Pia, msemaji hupata nafasi ya kuaga na
kushukuru.
Sasa tazama mfano halisi wa hotuba ambao umeandikwa kama majibu ya swali
la nane mtihani wa kumaliza kidato cha nne 2010.
Eleza tofauti iliyopo kati
ya hotuba na risala. Andika hotuba kuhusu “Maji ni Uhai.”
Kwa
kuwa mjadala wetu ni hotuba, risala haitazungumziwa, bali nitajikita katika
kuonyesha mfano wa hotuba.
MAJI NI UHAI
Wanakijiji
oyeeeeeeh!
Ndugu
Mwenyekiti wa Kijiji, ndugu Katibu wa Kijiji, Ndugu Wanakijiji wote mabibi na
mabwana. Ninafurahi kusimama mbele yenu na kuzungumza. Nikiwa kama
mwanaharakati wa muda mrefu wa utunzaji wa vyanzo vya maji, leo nasimama tena
kuwaeleza na kuuthibitishia umma huu kuwa maji ni uhai.
Asilimia
sabini ya miili yetu ni maji. Hivyo bila maji mwanadamu hawezi kuishi lau kwa
mwaka mmoja. Sisi ni maji, lazima tuishi kwa tahadhari kubwa kuyanusuru maji
haya yasipotee tukaadhirika.
Laiti
kama tungepata nafasi ya kutembelea watu waishio jangwani, tukawaona jinsi wanavyopata
shida ya maji, tungejifunza kitu. Kuna visa kadhaa vimekuwa vikiripotiwa katika
vyombo vya habari kuhusu watu na wanyama waliokufa kwa ukosefu wa maji.
Ukiachilia
mbali matumizi yetu, hata viumbe wengine kama mamba, samaki, viboko na pweza
wanategemea maji hayahaya ili waendelee kuishi. Ndugu zangu lazima sasa
tukubaliane kuwa, maji ni uhai.
Ni
kipi hakihitaji maji? Hata viwanda hivi tunavyovitegemea kwa uzalishaji wa
bidhaa, bila maji ya kupozea mitambo yake haviwezi kufanya kazi. Mwaka jana
nikiwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kijiji hiki tulikumbwa na kasheshe ya
kuharibikiwa na injini ya gari letu, tulipochunguza tukagundua ilichemka kupita
kiasi kwa kukosa maji!
Wanyama
na mimea tunaowategemea kwa chakula ili tuendelee kuishi, wanategemea maji. Kilimo
bila maji hakuna kitu. Bila maji wote tutakwisha na kusahaulika mara moja.
Niwaombe
ndugu zangu, tuiache mara moja hii tabia mpya iliyozuka. Tabia ya kunywesha
mifugo katika vyanzo vya maji itatuletea balaa. Pia, kuna mkasa mwingine wa
watu kukata miti hovyo. Hatukatazi kukata miti, lakini hakikisha unapokata mti
uwe na kibali maalumu na pia, kata mti panda mti. Vijana wa siku hizi
wamebadili msemo huu, wanasema panda mti ndipo ukate mti! Nawaunga mkono.
Ni
matumaini yangu makubwa mtayafanyia kazi yote niliyoyasema. Msingi zaidi,
tuhakikishe tunaepuka tabia zote ambazo zitatuharibia vyanzo vyetu vya maji.
Mwisho niwashukuru wote kwa kunisikiliza, nasema asanteni sana.