Historia na Maendeleo ya Fasihi ya Kiswahili

Vitabu vya fasihi


Fasihi ya Kiswahili ni ile iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili tu. Iwapo inazungumzia utamaduni wa Kiswahili au utamaduni mwingine. (Masebo & Nyangwine; 2007).
Historia ya fasihi ya Kiswahili inajadiliwa kwa kugawanywa katika vipindi vinne:
-      Kabla ya wageni
-      Wakati wa waarabu
-      Wakati wa ukoloni
-      Baada ya uhuru mpaka hivi sasa

Historia ya Fasihi ya Kiswahili Kabla ya Wageni

Katika kipindi hiki, fasihi haikuandikwa. Kulikuwa na fasihi simulizi pekee. Fasihi hii ilijumuisha ngano, methali, vitendawili, nyimbo, mashairi, majigambo n.k.
Fasihi hii ilipambwa na wahusika wanyama na mizimu, na ilisimuliwa jioni baada ya watu kumaliza kufanya kazi.
Katika kipindi hiki, fasihi ilitumiwa kama chombo cha kuelimisha jamii na kukemea maovu yote.

Wakati wa Waarabu

Wakati wa waarabu fasihi ya Kiswahili ilianza kuandikwa kwa hati za kiarabu. Kazi nyingi za Kiarabu zikafasiliwa na kuwekwa katika Kiswahili. Kwa mfano: hadithi za Alfu Lela Ulela, Hekaya za Abunuwasi na mashairi yaliyokuwa na urari wa vina na mizani.
Fasihi ya Kiswahili kwa mara ya kwanza ikapata nafasi ya kuhifadhiwa katika maandishi. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kuibuka kwa fasihi andishi.

Wakati wa Ukoloni

Katika wakati huu wazungu walikuja na hati zao za Kilatini. Fasihi ya Kiswahili ikaanza kuandikwa kwa hati ya Kilatini mpaka hii leo.
Hali hii ilikwenda sambamba na kuibuka kwa kazi nyingi za fasiri. Safari za Gulliver, Mashimo ya Mfalme Suleiman na Kisiwa Chenye Hazina ni mfano wa kazi hizo.
Kazi hizo za tafsiri zilijaa propaganda nyingi ili kuwafanya waafrika wajione wanyonge mbele ya wazungu. Hazikuzungumzia mambo yoyote yaliyowafaidisha waafrika.
Waandishi wa Kiafrika kama, Shaaban Robert na Mussa Said Abdallah waliibuliwa na mashindano ya uandishi yaliyoendeshwa na wakoloni.

Baada ya Uhuru Mpaka Hivi Sasa

Baada ya uhuru vitabu vya awali viliandikwa kwa lengo la kupongeza kupata uhuru huo.
Mara baada ya uhuru kuwa umekwisha patikana na hakuna jipya lolote lililoletwa na serikali za Kiafrika, fasihi ya kichokozi iliyosema na kuuhoji ukweli ikaibuka. Vitabu kama, Rosa Mistika, Nagona, Mzingile, Fungate ya Uhuru, Wasakatonge, Lina Ubani, n.k ni mfano wa vitabu ambavyo  vinaonyesha kutokuridhishwa na hali ya mambo hata baada ya uhuru kuwa umepatikana.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie