Uhuru wa Mwandishi wa Kazi za Fasihi Dhidi ya Tabaka Tawala
Uhuru wa mwandishi ni hali ya
mwandishi kuwa huru katika uandishi wa kazi zake.
Kuna uhuru wa mwandishi?
Uhuru wa mwandishi huamliwa na
tabaka tawala. Mwandishi anapojaribu kulisema tabaka tawala huenda akanyanyaswa
na kufungiwa kwa kazi zake. Endapo ataamua kuwa kasuku kwa kupongeza kila
kinachofanywa na watawala, kazi zake zitapongezwa na kupigiwa debe.
Ipo mifano mingi ya waandishi
ambao kazi zao zilipigwa marufuku baada ya kulisema bila woga tabaka tawala.
Tamthiliya ya ‘I Will Marry When I Want’ ya Ngugi Wa Thion’go ilikumbana uso
kwa uso na rungu la mdhibiti baada ya kulisema tabaka tawala.
Rosa Mistika ya Kezilahabi nayo
ilifungiwa na mdhibiti kwa sababu watumishi wa serikali walisemwa waziwazi.
Huko Afrika ya Kusini, nguvu
kupita kiasi zilitumika dhidi ya waandishi ambao walikwenda kinyume na tabaka
tawala. Waandishi hao walinyanyaswa mpaka wakahama nchi yao.
Mwaka 1975 na 1976, vitabu vyote
vya David Mailu vilipigwa marufuku nchini kwa madai kuwa, vilieleza mambo ya
aibu waziwazi. Ilikuwa ni ajabu mno kuzuiwa kwa vitabu hivi na kuachwa vitabu
kama ‘Kama Sutra’ vilivyozungumzia masuala ya ngono bila kificho.
Kutokana na watawala kutopenda
kusemwa waziwazi, mbinu ya waandishi wengi imebadilika na kuwa ile ya kutumia
mafumbo kwa lengo la kukwepa udhibiti wa kazi zao.
Kezilahabi baada ya riwaya yake
kufungiwa kwa sababu zisizoeleweka, alimua kuja na mtindo mpya katika riwaya
zake mbili, Nagona na Mzingile. Katika riwaya hizo, ametumia mtindo wa uandishi
ambao umejaa mafumbo na si rahisi kuelewa kilichoandikwa hasa maana yake nini?
Faida ya mwandishi kuwa huru
i.
Mwandishi
atakuwa huru kuikosoa jamii yake na tabaka tawala bila woga. Mwandishi atakuwa
huru kuonyesha maovu yote yanayotendeka katika jamii.
ii.
Mwandishi
atakuwa na msimamo. Msimamo huu utaendana
na kuwa na falsafa moja inayoeleweka na kumwepusha na uandishi wa
kutazama watawala wanataka nini!
iii.
Unafiki
na ukasuku wa waandishi utakwisha. Mwandishi ambaye hana uhuru wake hugeuka
kasuku wa watawala. Hujipendekeza na kujikomba kwao ili kumwepusha na rabsha za
watawala.
iv.
Fasihi
inakuwa chombo cha kuikomboa jamii. Lengo la fasihi ni kuleta ukombozi katika
jamii. Mwandishi huru ni nyenzo muhimu katika kuifikia jamii imara.