Nadharia Mbalimbali Zinazoeleza Maana ya Fasihi

NADHARIA MBALIMBALI ZINAZOELEZEA MAANA YA FASIHI

Tunapouliza maana ya fasihi, tunakutana na maana nyingi kinzani. Maana yake ni kwamba kila mmoja aliifasiri fasihi kwa mtazamo wake. Kutokana na maana hizo kuwa nyingi na kutofautiana, kundi la nadharia hizi lilionekana kuwa na nguvu na ushawishi kiasi juu ya nini hasa maana ya fasihi.

Nadharia mbalimbali zinazojaribu kueleza maana ya fasihi ni:

1.   fasihi ni kioo

Maana yake ni  kwamba, fasihi ni kioo ambacho mtu anaweza akajitazama na kuona taswira yake.
Nadharia hii inakumbana na changamoto mbili:
Kwanza, kioo hakiwezi kumweleza mtu ni wapi anatakiwa ajirekebishe.
Pili, huwezi ukajiona sehemu zote katika kioo.

2.   Fasihi ni hisi

Hii ina maana kwamba, ni lazima mwandishi au mhusika wa kazi yoyote ya fasihi apate mguso fulani ndipo aweze kuandika au kuitoa kazi yake.
Nadharia hii inaibua maswali mengi. Je ni lazima mtunzi wa kazi ya fasihi aguswe ndipo aweze kutoa kazi yake? Bila hisi hakuna kazi ya fasihi? Waandishi wa kazi za fasihi kama Penina Mhando, Kezilahabi, Shaaban Robert na wengineo waliguswa mara ngapi? Maswali haya yanakosa majibu hivyo nadharia hii haijitoshelezi.

3.   Fasihi ni mwamvuli

Kama ambavyo mwamvuli huweza kumkinga mtu dhidi ya mvua na jua kali, ndivyo fasihi ilivyo na uwezo wa kuzikinga amali za jamii zisiharibike.
Hata hivyo nadharia hii inakosa mashiko kwani jamii hubadilika mara kwa mara. Mfano zipo mila na desturi zilizohifadhiwa na makabila mengi na hazina nafasi hii leo. Hivyo, mwamvuli utatoboka kwani hautaweza kuhimili vishindo vya mabadiliko yanayotokea katika jamii.

4. Fasihi ni Sanaa ya Uchambuzi wa Lugha Inavyosemwa, Inavyoandikwa na Kusomwa

Maana hii ina ukweli kwa kiasi fulani kwani ni kweli fasihi msingi wake mkubwa ni lugha na hakuna kazi ya fasihi bila lugha. Hata hivyo si kweli kwamba, fasihi inahusu uchambuzi wa lugha pekee, vipo vipengele vingi kama, dhamira, ujumbe, migogoro, wahusika na vipengele vingine kadha wa kadha.

Nini maana ya fasihi?

Baada ya kutazama nadharia hizo, sasa tutazame maana ya fasihi ambayo inaelekea kukubalika.
Fasihi ni sanaa inayotumia lugha katika kufikisha ujumbe wake. Fasihi huipa jamii maarifa na mbinu za kupambana na mazingira ili kuondoa uozo katika jamii kwa lengo la kuleta haki na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Marejeo:

Nkwera, F. (1978) Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. TPH: Dar es Salaam.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1