Dhima ya Mwanafasihi Katika Jamii

DHIMA YA MWANAFASIHI KATIKA JAMII

Mwanafasihi ni mtu ambaye hutumia muda wake katika utungaji wa kazi za fasihi simulizi au andishi. Ipo mifano mingi ya wanafasihi, miongoni mwao ni: Shaabani Robert, Theobald Mvungi, Ardin Mtembei na wengine wengi. Mwanafasihi ana dhima nyingi katika jamii, miongoni mwazo ni:
i.             Kuielimisha jamii yake. Mwanafasihi mzuri ni yule anayelenga katika kuipatia elimu jamii yake juu ya mambo mbalimbali. Shafi Adam Shafi katika riwaya ya Vuta n’kuvute, ameielimisha jamii kwa kiasi kikubwa juu ya umuhimu wa kupigania uhuru na kujitawala wenyewe.
ii.            Kuburudisha jamii. Aghalabu mwanafasihi hulenga katika kuiburudisha jamii yake ili kuiondolea uchovu wa shughuli ngumu za uzalishaji mali. Unaposoma kazi ya fasihi, akili na mwili huburudishwa na ule ufundi wa mwanafasihi wa kusimulia mambo. Hakuna ubishi kuwa usomaji wa kazi za mwanafasihi Kezilahabi huburudisha.
iii.           Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii. Mila na desturi za jamii yetu zimehifadhiwa katika fasihi. Mfano, riwaya ya Janga Sugu la Wazawa ni miongoni mwa kazi za fasihi zinazohifadhi mambo mengi muhimu sana katika jamii. Mfano mwingine ni tamthiliya ya Kinjekitile, ambayo inaelezea kwa undani mkasa wa kuzuka kwa vita vya majimaji na jinsi ambavyo babu zetu walipambana kwa nguvu zao zote katika vita hivyo.
iv.          Kukuza lugha. Mwanafasihi ana kazi kubwa ya kuhakikisha lugha yake inakua. Mwanafasihi Shakespear wa Uingereza amefanya kazi  nzito katika kuikuza lugha ya kiingereza.  Maana yake ni kwamba, kadiri lugha inavyotumiwa na watunzi, ndivyo inavyozidi kukua na kupevuka. Shaabani Robert ni miongoni mwa wanafasihi ambao wameisaidia lugha ya Kiswahili kukua kwa kuanzisha misamiati mipya.
Katika jadi ya ushairi wa Kiswahili inadaiwa kuwa, ushairi ulikuwa ni ghala ya maneno. Washairi walitumia maneno magumu au yasiyokuwa ya kawaida makusudi ili kuyahifadhi yasipotee. Katika tamaduni nyingine, kazi hiyo hufanywa na makamusi na vitabu viitwavyo, ‘hazina za maneno:’ Kwa kuwa Waswahili hawakuwa na makamusi, kazi ya kuhifadhi maneno ilifanywa na ushairi. (Masebo&Nyangwine:7).

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne