Chimbuko la Fasihi na Sanaa, Mtazamo wa Kiyakinifu na Kidhanifu

CHIMBUKO LA FASIHI NA SANAAMitazamo miwili inaeleza kuhusu chimbuko la fasihi: Wa kwanza ni ule wa kidhanifu na wa pili ni mtazamo wa kiyakinifu.

Mtazamo wa Kidhanifu

Mtazamo huu hoja zake zimo katika kudhani tu na kamwe hoja hizo haziwezi kuthibitika kisayansi.
Mtazamo huu unaeleza kwamba, fasihi hutoka kwa Mungu na mwanadamu huipokea fasihi kutoka kwa Mungu huyo.
Wataalamu ambao maandiko yao yanakubaliana na mtazamo huu miongoni mwao ni F. Nkwera na John Ramadhani.
Mfano Nkwera anakubaliana na nadharia hii kwa kusema: “Matengenezo ya sanaa huonekana kuwa ni shughuli ya kiungu yenye kumwiga Mungu ambaye ndiye msanii wa kwanza.”
Ukiuchunguza kwa undani mtazamo huu unaelekea kuamini kuwa, mwanadamu hahusiki katika utengenezaji wa fasihi, bali hupewa fasihi hiyo ikiwa tayari imetengenezwa. Haya ni mawazo yaliyochakaa na yanayoibua maswali mengi kuliko majibu.
Pia, mtazamo huu unamtenga msanii na jamii yake na kumpa uwezo mkubwa mno wa kuwa karibu na Mungu kuliko watu wengine wa kawaida.
Mtazamo huu umewaathiri zaidi waandishi wengi wa mashairi. Mara nyingi katika beti zao huanza kwa kumshukuru Mungu kwa kuwapa uwezo wa kuandika na humaliza kwa kumshukuru Mungu tena kwa kuwajaalia uwezo huo wa kuzipanga beti zikasomeka.

Mtazamo wa kiyakinifu

Mtazamo huu unakuja na hoja ambazo angalau zinaweza kuthibitika kisayansi. Unaeleza kuwa, chanzo cha fasihi ni mwanadamu mwenyewe na mazingira yake.
Hadithi, methali, vitendawili, nyimbo, tenzi, majigambo, mafumbo n.k vilitungwa na kusimuliwa kwa lengo la kufunza, kukosoa, kuadibu, kuamsha fikra, na kuiburudisha jamii baada ya kazi ili kuipunguzia uchovu.
Sanaa hii ilirithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kwa njia ya masimulizi. Baadaye mwanadamu kaendelea sana kiteknolojia na ameweza kuhifadhi na kusambaza fasihi kwa njia za haraka zaidi. Njia zinazotumika leo hii ni: kanda za kunasia sauti, kanda za video, runinga, kompyuta na intanenti. Hivyo hoja ya kuwa chanzo cha fasihi ni mwanadamu mwenyewe inakubalika.

Marejeo:

Nkwera, F. (1978) Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. TPH: Dar es Salaam.
J.A Masebo & N. Nyangwine. (2007). Fasihi kwa Ujumla: Nadharia ya Fasihi. Nyambari Nyangwine Publishers: Dar es Salaam.

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne