Past Paper | Mtihani wa Kiswahili | Kidato cha Nne 2011
SEHEMU A (Alama 10)
UFAHAMU
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
1. Soma
kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata: Misitu
ya nchi ni mingi sana hata wakati mwingine tunadanganyika kuwa haitakwisha
kamwe. Tunaamini kwamba tunaweza kuendelea kuitumia miti yake na kuikata kwa
ajili ya kupata mashamba na malisho ya wanyama wetu bila kujishughulisha
kupanda au kuhifadhi mingine kwa ajili ya siku za mbele.
Fikiria tulivyo
na mawazo potofu. Fikira mbaya kama hizo wanazo watu wengi nchini mwetu. Kwa
hiyo imenilazimu kuwaonesheni kuwa misitu ni lazima ilindwe na haitalindwa kwa
manufaa ya kizazi chetu cha sasa tu, bali pia kwa ajili ya vizazi vyetu
vijavyo.
Basi mjue kuwa
kama misitu yote itakatwa patakuwa na upungufu mkubwa wa mbao na pia upungufu
wa maji ambao ni mbaya zaidi. Ubaya kama huu hautakiwi utokee katika Taifa letu
linalosonga mbele. Hatuwezi kuruhusu uharibifu wa misitu yetu uendelee
kufanyika kwa sababu unarudisha nyuma hali ya maisha yetu na unazuia ustawi wa
nchi yetu.
Hebu fikiria
kwanza maisha yetu yatakuwaje iwapo miti itakosekana - taabu ya kupika, gharama
ya kujenga kwa chuma, mawe au udongo ulaya badala ya miti. Gharama ya viti,
vitanda na meza ikiwa vitatengenezwa kwa chuma tu. Halafu fikiria kama maji
yote yakikauka, ninyi nyote mwajua shida zitakazotokea, kwa hiyo hatutaki
kabisa shida kutokea.
Kwa nini tuwe na
shida ya kukosa maji katika sehemu ambazo zina maji ya kutosha? Basi inatupasa
kuona kwamba kuna ulazima wa kuhifadhi misitu kwa ajili ya matumizi ya leo na
kesho.
Bila shaka sasa
utajiuliza mwenyewe. Je, siwezi kukata kabisa misitu ili niweze kulima? Jibu ni
kwamba unaweza kabisa, lakini ni katika sehemu zile ambazo hazikuhifadhiwa.
Tena ifahamike kwamba sehemu ambazo zimehifadhiwa ni chache sana ukilinganisha
na mapori makubwa yaliyobaki wazi kwa ajili ya kilimo. Sasa nataka kusisitiza
hasa juu ya misitu iliyohifadhiwa.
Hizi ndizo
sehemu za misitu ambazo ni za lazima sana, na inatakiwa zihifadhiwe daima kwa
matumizi ya faida ya Taifa. Misitu iliyohifadhiwa ni misitu inayotazamiwa
kudumu daima nchini. Inatunzwa ili itumiwe kwa utaratibu ulio bora kwa kizazi
hata kizazi.
Kwa wakati ujao
misitu hiyo itatoa mbao za kujenga nyumba, shule, hospitali na majengo mengine,
pia kutengeneza viti, meza, makabati, milango, madirisha na masanduku. Hata
sasa, mbao nyingi zitumikazo hutokana na miti iliyoota katika misitu
iliyohifadhiwa.
Lakini kwa
sababu ardhi yenye misitu ya aina hiyo inahitajiwa sana kwa kilimo, itatubidi
kuanza kuotesha misitu mipya kwa ajili ya mahitaji yetu. Basi ni lazima
niwakumbushe wananchi kuwa miti iliyomo katika misitu iliyohifadhiwa haitatosha
kufanyia kazi zetu zote ili kuinua maisha ya watu na kuinua uchumi wa nchi.
Misitu
iliyohifadhiwa lazima iongezwe kwa kupanda miti mingine, kwa mfano hivi sasa
Idara ya misitu inapanda miti kati ya eka elfu nne na tano kila mwaka na pia
inaangalia miti ya asili katika sehemu kubwa kabisa ya nchi hii.
Maswali
(a) Kwa mujibu
wa habari uliyosoma watu wengi hufikiria nini juu ya misitu?
(b) Mwandishi wa
habari hii anasema ni jambo gani huleta uharibifu wa misitu?
(c) Mwandishi
anashauri misitu ikatwe katika sehemu gani?
(d) Je, ni
madhara gani yatatokea endapo misitu itatoweka kabisa?
(e) Je, ni
sahihi kusema kuwa kwa vile kuna misitu iliyohifadhiwa hakuna haja ya
kushughulika na kupanda miti nchini? Kwa nini? 2.
2. Fupisha aya
tatu (3) za mwisho za habari uliyosoma kwa maneno themanini (80).
SEHEMU B (Alama 25)
SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA
Jibu maswali
yote katika sehemu hii.
3. Tumia
kiambishi “KA” kuonesha matukio kumi (10).
4. “Kila lugha ina tabia ya kuchukua maneno
kutoka lugha nyingine ili kukidhi mahitaji yake kimsamiati.” Fafanua kauli hii
ukitumia maneno kumi (10) ya Kiswahili.
5. Yapange
maneno yafuatayo kama yanavyoonekana katika kamusi, kisha eleza maana ya kila
neno kwa kutoa mfano mmoja (1) wa sentensi.
(a) Falsafa (b)
Barizi (c) Anuwai(d) Barubaru (e) Kinda (f) Ajuza (g) Fanusi (h) Ghaibu (i)
Goigoi (j) Kinanda
6. Eleza maana
ya upatanisho wa kisarufi. Fafanua jibu lako kwa kutoa mifano minne.
7. “Misemo mingi
hutumika kwa madhumuni ya kulinda heshima na kuvuta makini ya watu.” Fafanua
usemi huu kwa kutumia misemo mitano (5).
SEHEMU C (Alama 10)
UANDISHI Jibu swali moja (1) kutoka sehemu hii.
8. Andika insha
isiyo ya kisanaa yenye maneno mia mbili na hamsini (250) kuhusu mandhari ya
shule yenu.
9. Andika
kumbukumbu za kikao cha wanafunzi kuhusu sherehe ya kumuaga mkuu wenu wa shule
aliyepata wadhifa wa kuwa Afisa Elimu wa Mkoa.
SEHEMU D (Alama 10)
MAENDELEO YA KISWAHILI
Jibu swali la kumi (10)
10. Fafanua
athari ya Waarabu katika lugha ya Kiswahili kwa kutoa hoja nne (4).
SEHEMU E (Alama 45)
FASIHI KWA UJUMLA
Jibu maswali matatu (3) kutoka katika sehemu hii. Swali la 15 ni la lazima.
11. Sifa muhimu
mojawapo ya methali ni kujenga picha au taswira ambazo huchotwa katika
mazingira yanayoizunguka jamii.” Thibitisha hoja hii kwa kutumia methali tano
(5).
12. “Maelekezo
yanayotolewa na msanii wa fasihi hukidhi matarajio ya jamii yake.” Kwa kutoa
hoja tatu (3) kwa kila mchairi, jadili kauli hii kwa kuwatumia washairi wawili
(2) kati ya walioorodheshwa.
13. “Nyimbo ni
mbinu ya kifani ambayo wasanii wengi huitumia ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa
kwa hadhira.” Thibitisha usemi huu kwa kutumia waandishi wawili (2) wa riwaya
kati ya waliorodheshwa.
14. Jadili jinsi
wasanii wawili (2) wa tamthiliya mbili (2) ulizosoma walivyotumia mbinu ya
kicheko kutoa ujumbe walioukusudia kwa jamii.
15. Eleza muundo
wa soga. Tunga soga ya kusisimua kuhusu kisa cha kubuni.
ORODHA YA VITABU
Ushairi
Wasakatonge - M.S. Khatibu (DUP)
Malenga wapya -
TAKILUKI (DUP)
Mashairi ya
Chekacheka - T.A. Mvungi (EP & D. LTD)
Riwaya Takadini - Ben Hanson (MBS)
Watoto wa Mama
N’tilie - E. Mbogo (H.P)
Joka la Mdimu -
A.J. Safari (H.P)
Tamthiliya
Orodha - Steve Raynolds (MA)
Ngoswe Penzi
Kitovu cha Uzembe - E. Semzaba (ESC)
Kilio Chetu - Medical Aid Foundation (TPH)